Wamefungwa kwa Sababu ya Imani Yao—Eritrea
Kwa miaka mingi, serikali ya Eritrea imekuwa ikiwakamata Mashahidi wa Yehova na kuwafunga, kutia ndani wanawake na wazee wenye umri mkubwa, bila kesi kusikilizwa mahakamani au kuzingatia utaratibu wa kisheria kwa sababu ya kushiriki utendaji wa kidini au kwa sababu zisizojulikana. Rais Afwerki alifuta uraia wa Mashahidi kupitia amri ya rais iliyotolewa Oktoba 25, 1994 kwa sababu hawakushiriki kutoa maoni yao kuhusu kupata uhuru mwaka wa 1993 na pia walikataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Kabla ya wenye mamlaka nchini Eritrea kuanza kuwalazimisha watu washiriki utumishi wa kijeshi, walitoa njia mbadala ya utumishi wa kiraia. Mashahidi wengi walishiriki utumishi huo chini ya uongozi mbalimbali. Wenye mamlaka waliwapatia “Vyeti vya Kuhitimu Utumishi wa Kitaifa” na mara nyingi waliwasifu washiriki kwa kazi nzuri waliyofanya. Lakini baada ya amri hiyo ya rais, vikosi vya ulinzi vya Eritrea vimewafunga gerezani, kuwatesa, na kuwalazimisha Mashahidi wa Yehova wakane imani yao.
Kufikia sasa kuna Mashahidi wa Yehova sitini na wanne ambao bado wapo gerezani (wanaume 34 na wanawake 30). Mashahidi wa Yehova ishirini na nane (wanaume 26 na wanawake 2) waliachiliwa huru Desemba 4, 2020, baada ya kufungwa gerezani kwa muda wa kati ya miaka 5 hadi 26 kwa sababu ya imani yao. Januari 29, 2021, mwanamume mmoja ambaye ni Shahidi aliachiliwa baada ya kufungwa gerezani kwa zaidi ya miaka 12, na kwa kuongezea Mashahidi watatu waliachiliwa Februari 1, 2021 (mwanamume mmoja na wanawake wawili). Wamefungwa kwa muda wa kati ya miaka minne hadi tisa.
Mashahidi Wanakufa kwa Sababu ya Hali Mbaya Zilizo Gerezani
Mashahidi wanne wamekufa wakiwa gerezani nchini Eritrea na wengine watatu waliokuwa na umri mkubwa wamekufa kwa sababu ya hali mbaya walizokabili wakiwa gerezani.
Mwaka 2018, Mashahidi wawili walikufa baada ya kuhamishwa kutoka gereza la awali kwenda gereza la Mai Serwa. Habtemichael Tesfamariam alikufa Januari 3 akiwa na umri wa miaka 76, na Habtemichael Mekonen alikufa Machi 6 akiwa na umri wa miaka 77. Wenye mamlaka nchini Eritrea waliwafunga wanaume hao tangu mwaka 2008 bila kuwafungulia mashtaka yoyote.
Katika mwaka 2011 na 2012, Mashahidi wawili walikufa kwa sababu walitendewa kwa njia ya kinyama katika Gereza la Kambi ya Meitir. Misghina Gebretinsae, aliyekuwa na umri wa miaka 62, alikufa Julai 2011 baada ya kufungiwa katika eneo la kuwaadhibu wafungwa lenye joto kali linalojulikana kwa jina la “chini ya ardhi.” Yohannes Haile, aliyekuwa na umri wa miaka 68, alikufa Agosti 16, 2012, baada ya kufungwa chini ya hali kama hizo kwa karibu miaka minne. Mashahidi wengine watatu wenye umri mkubwa, Kahsai Mekonnen, Goitom Gebrekristos, na Tsehaye Tesfariam walikufa baada ya kuachiliwa kutoka gerezani kwa sababu ya hali mbaya waliyokabili walipokuwa katika Kambi ya Meitir.
Mapendekezo ya Mashirika Makubwa Yanayotetea Haki za Kibinadamu Yapuuzwa
Eritrea inaendelea kupuuza viwango vya kimataifa vya haki za kibinadamu. Mashirika ya haki za kibinadamu yamepinga ukiukaji wa haki za msingi za kibinadamu na kuendelea kusihi nchi ya Eritrea iache kukiuka haki hizo.
Mwaka 2014, Baraza la Haki za Kibinadamu (HRC) lilipokea ripoti ya pekee kuhusu haki za kibinadamu nchini Eritrea. Ripoti hiyo iliwasihi wenye mamlaka waheshimu haki za wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri zao “kupatana na viwango vya kimataifa” na “kuhakikisha kwamba wafungwa wote wanatendewa vizuri; kuhakikisha kwamba walio wagonjwa wanapokea matibabu . . . na kuboresha hali magerezani kulingana na viwango vya kimataifa.” Katika azimio la mwaka 2015, HRC iliagiza serikali ya Eritrea “itambue haki za wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.”
Mwaka 2016, Tume ya Uchunguzi ya nchini Eritrea, iliona kwamba wenye mamlaka nchini Eritrea wana hatia ya “kukiuka haki za kibinadamu” kwa ‘kuwatesa Mashahidi wa Yehova na watu wengine kwa sababu za kidini na za kikabila.’
Mwaka 2017, Kamati ya Afrika ya Wataalamu wa Haki na Masilahi ya Mtoto (ACERWC) ilisema kwamba ijapokuwa kila mtoto ana haki kisheria, “watoto wa Mashahidi wa Yehova” hawapewi haki hizo na wanatendewa kwa ukatili. ACERWC ilipendekeza kwamba Eritrea “itambue na iheshimu kikamili Uhuru wa Kufikiri, Dhamiri na Dini ya mtoto bila ubaguzi.”
Mwaka 2018, Tume ya Haki za Kibinadamu na Watu kwa Ujumla ya Afrika ilipendekeza kwamba nchi ya Eritrea “ichukue hatua haraka dhidi ya ukiukaji wa haki za msingi za watu wote waliofungwa kutia ndani . . . washiriki wa imani ya Mashahidi wa Yehova” na kutaka uchunguzi ufanyike juu ya idadi ya vifo vilivyoripotiwa vya Mashahidi wa Yehova waliokuwa gerezani. Tume hiyo ilisisitiza kwamba Eritrea ihakikishe kwamba Mashahidi wa Yehova “wanaendelea kuwa na haki za kiraia.”
Mei 2019, Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (CCPR) iliisihi nchi ya Eritrea ihakikishe kwamba uhuru wa kidini na kiimani unazingatiwa na “kuwaachilia huru watu wote waliozuiliwa au kufungwa kwa kutenda kulingana na haki zao za kidini kutia ndani Mashahidi wa Yehova.” CCPR pia iliomba Eritrea “itambue haki za watu wanaokataa utumishi wa kijeshi na kuwaruhusu wafanye utumishi mbadala wa kiraia.”
Katika ripoti ya Mei 12, 2021, Katibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa aliiomba serikali ya Eritrea “iwaachilie mara moja na bila masharti wote ambao bado wamefungwa gerezani bila kushtakiwa au kufikishwa mahakamani kwa sababu ya imani yao, kutia ndani Mashahidi 20 wa Yehova,” na “ipitie upya maamuzi yake ya kuwanyang’anya uraia Mashahidi wa Yehova kwa sababu ya dini yao, iheshimu mapendekezo ya Tume ya Afrika Kuhusu Haki za Kibinadamu na Jamii ili kuhakikisha kwamba Mashahidi wa Yehova wanadumisha haki zao wakiwa raia, na kupeleleza vifo vilivyoripotiwa vya Mashahidi wa Yehova walipokuwa kifungoni.”
Vifungo vya Gerezani Visivyo na Mwisho
Mashahidi wengi wa kiume walio gerezani hawana tumaini lolote la kuachiliwa mpaka wafe au wanapokaribia kufa. Kwa kuwa haiwezekani kufanya mipango yoyote ya kisheria au kufungua kesi, kifungo chao kinaonekana kama kifungo cha maisha.
Mfuatano wa Matukio
Oktoba 17, 2024
Jumla ya Mashahidi 64 wamefungwa gerezani.
Februari 1, 2021
Mashahidi watatu wameachiliwa huru.
Januari 29, 2021
Shahidi mmoja ameachiliwa huru.
Desemba 4, 2020
Mashahidi ishirini na nane wa Yehova waachiliwa kutoka gerezani.
Machi 6, 2018
Habtemichael Mekonen, mwenye umri wa miaka 77, alikufa baada ya kuhamishwa kutoka gereza la awali kwenda Gereza la Mai Serwa.
Januari 3, 2018
Habtemichael Tesfamariam, mwenye umri wa miaka 76, alikufa baada ya kuhamishwa kutoka gereza la awali kwenda Gereza la Mai Serwa.
Julai 2017
Mashahidi wote waliokuwa katika kambi ya Meitir wanahamishiwa kwenye gereza la Mai Serwa lililo karibu na Asmara.
Julai 25, 2014
Wengi wa waliokamatwa Aprili 14 waachiliwa huru, lakini 20 kati ya wale waliokamatwa Aprili 27 bado wanazuiliwa.
Aprili 27, 2014
Mashahidi 31 hivi wakamatwa wakati wa mkutano wa kujifunza Biblia.
Aprili 14, 2014
Mashahidi zaidi ya 90 wakamatwa wakati wa mwadhimisho wa kila mwaka wa Ukumbusho wa kifo cha Yesu.
Agosti 16, 2012
Yohannes Haile, mwenye umri wa miaka 68, anakufa akitumikia kifungo chini ya hali ngumu sana.
Julai 2011
Misghina Gebretinsae, mwenye umri wa miaka 62, anakufa akitumikia kifungo chini ya hali ngumu sana.
Juni 28, 2009
Wenye mamlaka wavamia nyumba ya Shahidi wakati wa ibada na kuwakamata Mashahidi wote 23 waliohudhuria, kuanzia umri wa miaka 2 hadi 80.
Aprili 28, 2009
Wenye mamlaka wawahamisha wafungwa wote lakini mfungwa mmoja ambaye ni Shahidi wa Yehova azuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Gereza la Kambi ya Meitir.
Julai 8, 2008
Wenye mamlaka waanza kuvamia nyumba na mahali pa kazi na kuwakamata Mashahidi 24, wengi wao wana familia zinazowategemea.
Mei 2002
Serikali yafunga vikundi vyote vya kidini ambavyo si sehemu ya vikundi vinne vya kidini vilivyokubaliwa na serikali.
Oktoba 25, 1994
Rais atoa amri ya kufutilia mbali uraia wa Mashahidi wa Yehova na kuwaondolea haki za msingi za raia.
Septemba 17, 1994
Paulos Eyasu, Isaac Mogos, na Negede Teklemariam wafungwa bila kushtakiwa au kufikishwa mahakamani.
Miaka ya 1950
Mwanzo wa kuwepo kwa Mashahidi wa Yehova nchini Eritrea.