Mke wa Kaini Alikuwa Nani?
Jibu la Biblia
Kaini, mtoto wa kwanza wa mwanamume na mwanamke wa kwanza, alioa mmoja wa dada zake au mtu mwingine wa karibu wa ukoo. Mkataa huo unaweza kufikiwa kwa kufikiria kile ambacho Biblia inasema kumhusu Kaini na familia yake.
Mambo hakika kuhusu Kaini na familia yake
Wanadamu wote walitoka kwa Adamu na Hawa. Mungu “alifanya kutoka kwa mtu mmoja kila taifa la watu, ili wakae juu ya uso wa dunia nzima.” (Matendo 17:26) Hawa, mke wa Adamu, akawa “mama ya kila mtu anayeishi.” (Mwanzo 3:20) Kwa hiyo, lazima Kaini awe alioa mtu ambaye pia alitoka kwa Adamu na Hawa.
Kaini na ndugu yake Abeli walikuwa wa kwanza kati ya watoto kadhaa waliozaliwa na Hawa. (Mwanzo 4:1, 2) Kaini alipofukuzwa kwa kumuua ndugu yake, alilalamika hivi: “Yeyote atakayenikuta ataniua.” (Mwanzo 4:14) Kaini alikuwa akiogopa nani? Biblia inasema kwamba Adamu “akazaa wana na mabinti.” (Mwanzo 5:4) Ni wazi kwamba wazao hao wengine wa Adamu na Hawa wangeweza kumshambulia Kaini.
Mapema katika historia ya wanadamu, lilikuwa jambo la kawaida kuoa mtu wa karibu wa ukoo. Kwa mfano, mwanamume mwaminifu Abrahamu alimwoa binti ya baba yake aliyezaliwa na mama mwingine. (Mwanzo 20:12) Sheria ya Musa ndiyo iliyokataza kwa mara ya kwanza ndoa kama hizo. Sheria hiyo ilitungwa karne nyingi baada ya siku za Kaini. (Mambo ya Walawi 18:9, 12, 13) Inaonekana kwamba nyakati hizo watoto waliozaliwa kutokana na watu wa ukoo wa karibu hawakuwa na madhara ya kuzaliwa kama ilivyo leo.
Biblia inaonyesha simulizi la Adamu, Hawa, na familia yao kuwa historia sahihi. Nasaba zinazorudi nyuma hadi kwa Adamu zinapatikana katika kitabu cha Mwanzo, kilichoandikwa na Musa na pia katika maandishi ya wanahistoria wengine kama vile Ezra na Luka. (Mwanzo 5:3-5; 1 Mambo ya Nyakati 1:1-4; Luka 3:38) Waandikaji wa Biblia wanataja hadithi ya Kaini kuwa tukio halisi la kihistoria.—Waebrania 11:4; 1 Yohana 3:12; Yuda 11.