JE, NI KAZI YA UBUNI?
Mkono Wenye Kustaajabisha wa Pweza
Wahandisi wanajitahidi kutokeza vifaa ambavyo vitawasaidia madaktari kufanya upasuaji katika sehemu zilizobanana za mwili bila kupasua viungo vingine ili kufikia sehemu hizo. Mojawapo ya teknolojia inayobuniwa inategemea muundo wa mkono wa pweza unaoweza kujipinda kwa njia ya ajabu.
Zingatia: Pweza anaweza kukamata, kushika, na kubana vitu akitumia mikono yake mirefu minane, hata kupitia kwenye nafasi ndogo tu. Anaweza kupinda mikono yake upande wowote, na pia anaweza kukaza sehemu mbalimbali za mkono ikihitajika.
Watafiti wanaamini kwamba mkono kama huo wa roboti unaoweza kujipinda ungesaidia sana kufanya upasuaji usioathiri viungo vingine. Kifaa kama hicho kingerahisisha mbinu ya upasuaji kwa wagonjwa ambao wangelazimika kufanyiwa upasuaji tata zaidi.
Ona mikono ya pweza ikifanya kazi
Mkono kama huo wa roboti umeshatokezwa na unatumika katika upasuaji wa kuigiza. Sehemu moja ya mkono huo wenye urefu wa milimita 135 inaweza kuinua viungo laini na kuvishika bila kuviharibu, huku sehemu nyingine ikifanya upasuaji. Dakt. Tommaso Ranzani, mshiriki wa kikundi kilichotokeza kifaa hicho, alisema hivi: “Tunaamini kwamba kifaa hiki ndio mwanzo wa kutokeza mifumo mingine iliyoboreshwa na yenye visehemu bora zaidi.”
Una maoni gani? Je, mkono wa pweza ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?