Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uwezo wa Kuruka wa Nzi-Tunda

Uwezo wa Kuruka wa Nzi-Tunda

 Yeyote ambaye amewahi kujaribu kumpiga nzi, anajua si kazi rahisi. Wadudu hao huruka upesi sana na kukwepa jitihada zozote za kuwakamata.

 Wanasayansi wamegundua kwamba aina moja ya nzi, nzi-tunda, anaweza kujizungusha kwa kasi angani kuliko jinsi ndege za kivita zinavyofanya. Profesa Michael Dickinson anasema kwamba mara tu wanapozaliwa “wanaweza kuruka kwa ustadi wa hali ya juu. Ni kama kumwingiza mtoto aliyetoka tu kuzaliwa katika ndege ya kivita na aiendeshe kwa ustadi wa hali ya juu.”

 Watafiti wamerekodi video ya wadudu hao wanaporuka na kugundua kwamba wanapiga mabawa yao mara 200 kwa sekunde. Hata hivyo, unapojaribu kumkamata anahitaji tu kupiga bawa hilo mara moja ili ageuze mwili wake na kutoroka.

 Anatenda kwa kasi kadiri gani anapotishwa? Watafiti wamegundua kwamba wadudu hao hutenda mara 50 haraka kuliko mwanadamu anavyoweza kupepesa macho. Dickinson anaeleza kwamba “nzi hao hufanya hesabu za hali ya juu haraka sana ili kutambua hatari inakotokea na upande unaofaa zaidi wa kutorokea.”

 Kufikia sasa watafiti hawajaweza kuelewa jinsi ubongo mdogo wa nzi huyo unavyoweza kufanya hivyo.

Nzi-tunda huepuka hatari kwa kubadili upande anaoelekea haraka sana

 Una maoni gani? Je, uwezo wa nzi-tunda wa kuruka ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?