Kitabu cha Kwanza cha Wafalme 1:1-53
1 Sasa Mfalme Daudi alikuwa amezeeka,+ umri wake ulikuwa umesonga,* na ingawa walimfunika kwa nguo, hakuweza kupata joto.
2 Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia: “Bwana wetu mfalme turuhusu tukutafutie msichana bikira atakayekuhudumia na kukutunza. Atalala mikononi mwako ili bwana wetu mfalme upate joto.”
3 Wakatafuta msichana mrembo katika eneo lote la Israeli, wakampata Abishagi,+ Mshunamu,+ wakamleta kwa mfalme.
4 Msichana huyo alikuwa mrembo sana, naye alimhudumia mfalme na kumtunza, lakini mfalme hakufanya naye ngono.
5 Wakati huo, Adoniya+ mwana wa Hagithi alikuwa akijikweza, akisema: “Nitakuwa mfalme!” Alijitengenezea gari, naye akawa na wapanda farasi na wanaume 50 waliokimbia mbele yake.+
6 Lakini baba yake hakuwahi kamwe kumkemea* kwa kumuuliza: “Kwa nini umefanya hivi?” Alikuwa pia na sura nzuri sana, na mama yake alimzaa baada ya Absalomu.
7 Alishauriana na Yoabu mwana wa Seruya na kuhani Abiathari,+ nao wakajitolea kumsaidia Adoniya na kumuunga mkono.+
8 Lakini kuhani Sadoki,+ Benaya+ mwana wa Yehoyada, nabii Nathani,+ Shimei,+ Rei, na wale mashujaa hodari wa Daudi+ hawakumuunga mkono Adoniya.
9 Mwishowe Adoniya akawatoa dhabihu+ kondoo, ng’ombe, na wanyama waliononeshwa, kando ya jiwe la Zohelethi, lililo karibu na En-rogeli, akawaalika ndugu zake wote wana wa mfalme, na wanaume wote wa Yuda watumishi wa mfalme.
10 Lakini hakumwalika nabii Nathani, Benaya na wale mashujaa hodari, wala Sulemani ndugu yake.
11 Ndipo Nathani+ akamuuliza Bath-sheba,+ mama ya Sulemani:+ “Je, hujasikia kwamba Adoniya+ mwana wa Hagithi amekuwa mfalme, na bwana wetu Daudi hajui lolote kuhusu jambo hilo?
12 Sasa, njoo tafadhali, nikupe ushauri, ili uokoe uhai wako mwenyewe na uhai wa* mwana wako Sulemani.+
13 Nenda kwa Mfalme Daudi ukamuulize, ‘Je, bwana wangu mfalme, hukuniapia mimi kijakazi wako, ukisema: “Sulemani mwana wako atakuwa mfalme baada yangu, naye ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme”?+ Basi kwa nini Adoniya amekuwa mfalme?’
14 Utakapokuwa ukiendelea kuzungumza na mfalme, nitaingia na kuthibitisha maneno yako.”
15 Kwa hiyo Bath-sheba akaingia kwa mfalme, katika chumba chake cha faragha. Mfalme alikuwa amezeeka sana, na Abishagi,+ Mshunamu, alikuwa akimhudumia mfalme.
16 Kisha Bath-sheba akainama na kumsujudia mfalme, mfalme akamuuliza: “Una ombi gani?”
17 Akajibu: “Bwana wangu, wewe ndiye uliyeniapia mimi kijakazi wako kwa jina la Yehova Mungu wako uliposema, ‘Sulemani mwana wako atakuwa mfalme baada yangu, na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme.’+
18 Lakini tazama! Adoniya amekuwa mfalme, na bwana wangu mfalme hujui lolote kuhusu jambo hilo.+
19 Aliwatoa dhabihu ng’ombe dume, wanyama waliononeshwa, na kondoo wengi sana na kuwaalika wana wote wa mfalme na kuhani Abiathari na Yoabu mkuu wa jeshi;+ lakini hakumwalika Sulemani mtumishi wako.+
20 Na sasa, bwana wangu mfalme, macho yote ya Waisraeli yanakutazama uwaambie ni nani atakayeketi kwenye kiti chako cha ufalme baada yako bwana wangu mfalme.
21 Usipofanya hivyo, mara tu utakapokufa na kuzikwa pamoja na mababu zako bwana wangu mfalme, mimi na mwanangu Sulemani tutaonwa kuwa wasaliti.”
22 Na alipokuwa akiendelea kuzungumza na mfalme, nabii Nathani akaingia.+
23 Mara moja mfalme akaambiwa hivi: “Nabii Nathani amefika!” Akaingia mbele ya mfalme na kumsujudia mfalme mpaka ardhini.
24 Kisha Nathani akasema: “Bwana wangu mfalme, je, ulisema hivi: ‘Adoniya atakuwa mfalme baada yangu, na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme’?+
25 Kwa maana leo ameshuka kwenda kuwatoa dhabihu+ ng’ombe dume, wanyama waliononeshwa, na kondoo wengi sana, naye amewaalika wana wote wa mfalme na wakuu wa jeshi na kuhani Abiathari.+ Wako huko wakila na kunywa pamoja naye, nao wanaendelea kusema, ‘Mfalme Adoniya na aishi muda mrefu!’
26 Lakini hakunialika mimi mtumishi wako, wala kuhani Sadoki, wala Benaya+ mwana wa Yehoyada, wala Sulemani mtumishi wako.
27 Je, bwana wangu mfalme umeidhinisha jambo hili bila kuniambia mimi mtumishi wako ni nani anayepaswa kuketi kwenye kiti chako cha ufalme baada yako?”
28 Ndipo Mfalme Daudi akajibu: “Niitieni Bath-sheba.” Basi akaingia na kusimama mbele ya mfalme.
29 Kisha mfalme akaapa hivi: “Kwa hakika kama Yehova anavyoishi, aliyeniokoa* kutoka katika mateso yangu yote,+
30 kama nilivyokuapia kwa jina la Yehova Mungu wa Israeli, nikisema, ‘Sulemani mwana wako atakuwa mfalme baada yangu, na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme baada yangu!’ hivyo ndivyo nitakavyofanya siku ya leo.”
31 Ndipo Bath-sheba akainama mpaka ardhini na kumsujudia mfalme na kusema: “Bwana wangu Mfalme Daudi na aishi milele!”
32 Mara moja Mfalme Daudi akasema: “Niitieni kuhani Sadoki, nabii Nathani, na Benaya+ mwana wa Yehoyada.”+ Basi wakaja mbele ya mfalme.
33 Mfalme akawaambia: “Nendeni na watumishi wangu, mkampandishe Sulemani mwanangu juu ya nyumbu* wangu mwenyewe,+ mteremsheni hadi Gihoni.+
34 Kuhani Sadoki na nabii Nathani watamtia mafuta+ huko awe mfalme wa Israeli; kisha pigeni pembe na kusema, ‘Mfalme Sulemani na aishi muda mrefu!’+
35 Kisha mfuateni anaporudi, naye atakuja na kuketi kwenye kiti changu cha ufalme; atakuwa mfalme baada yangu, nami nitamweka rasmi kuwa kiongozi wa Israeli na wa Yuda.”
36 Mara moja Benaya mwana wa Yehoyada akamwambia mfalme: “Amina! Yehova Mungu wako bwana wangu mfalme na athibitishe jambo hilo.
37 Kama Yehova alivyokuwa pamoja nawe bwana wangu mfalme, na awe pia na Sulemani,+ na Afanye kiti chake cha ufalme kiwe kikuu zaidi kuliko kiti chako cha ufalme, bwana wangu Mfalme Daudi.”+
38 Kisha kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya+ mwana wa Yehoyada, na Wakerethi na Wapelethi+ wakateremka, nao wakampandisha Sulemani juu ya nyumbu wa Mfalme Daudi,+ wakampeleka Gihoni.+
39 Kisha Kuhani Sadoki akachukua pembe ya mafuta+ kutoka hemani+ na kumtia mafuta Sulemani,+ nao wakaanza kupiga pembe, na watu wote wakaanza kusema hivi kwa sauti kubwa: “Mfalme Sulemani na aishi muda mrefu!”
40 Kisha watu wote wakapanda wakimfuata, wakipiga filimbi na kushangilia sana, hivi kwamba dunia ikapasuka na kufunguka kwa sababu ya kelele zao.+
41 Adoniya na watu wote aliowaalika wakasikia kelele hizo walipokuwa wamemaliza kula.+ Mara tu Yoabu aliposikia sauti ya pembe, akauliza: “Kwa nini kuna kelele za vurugu jijini?”
42 Alipokuwa bado anaongea, Yonathani+ mwana wa kuhani Abiathari akaja. Kisha Adoniya akamwambia: “Ingia, kwa maana wewe ni mtu mwema,* bila shaka unaleta habari njema.”
43 Lakini Yonathani akamjibu Adoniya: “Hapana! Bwana wetu Mfalme Daudi amemweka Sulemani kuwa mfalme.
44 Mfalme alimwagiza aende pamoja na kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada, na Wakerethi na Wapelethi, nao wakampandisha juu ya nyumbu wa mfalme.+
45 Kisha kuhani Sadoki na nabii Nathani wakamtia mafuta kuwa mfalme huko Gihoni. Halafu wakapanda kutoka huko wakishangilia, nalo jiji limejaa kelele. Hizo ndizo kelele mlizosikia.
46 Isitoshe, Sulemani ameketi kwenye kiti cha ufalme.
47 Na tena, watumishi wa mfalme wamekuja kumpongeza bwana wetu Mfalme Daudi, wakisema, ‘Mungu wako na alifanye jina la Sulemani liwe na fahari kuliko jina lako, na Akifanye kiti chake cha ufalme kiwe kikuu kuliko kiti chako cha ufalme!’ Ndipo mfalme akainama kitandani.
48 Na pia mfalme akasema, ‘Yehova Mungu wa Israeli na asifiwe, ambaye leo amemchagua mtu wa kuketi kwenye kiti changu cha ufalme na ameruhusu macho yangu mwenyewe yaone jambo hilo!’”
49 Basi watu wote walioalikwa na Adoniya wakaogopa sana, na kila mmoja wao akainuka na kwenda zake.
50 Adoniya aliogopa pia kwa sababu ya Sulemani, basi akaondoka, akaenda na kuzishika kwa nguvu pembe za madhabahu.+
51 Sulemani akaletewa habari hii: “Tazama! Adoniya anamwogopa Mfalme Sulemani; naye ameshika pembe za madhabahu, akisema, ‘Mfalme Sulemani na aniapie kwanza kwamba hataniua mimi mtumishi wake kwa upanga.’”
52 Ndipo Sulemani akasema: “Akitenda kwa njia inayofaa, hakuna unywele wake hata mmoja utakaoanguka ardhini; lakini akipatikana ametenda uovu,+ lazima afe.”
53 Basi Mfalme Sulemani akaagiza aletwe kutoka kwenye madhabahu. Ndipo akaingia na kumwinamia Mfalme Sulemani, kisha Sulemani akamwambia: “Nenda nyumbani kwako.”
Maelezo ya Chini
^ Tnn., “siku zake zilikuwa zimesonga.”
^ Au “kumuumiza hisia.”
^ Au “nafsi yako mwenyewe na nafsi ya.”
^ Au “aliyeikomboa nafsi yangu.”
^ Au “nyumbu jike.”
^ Au “anayeheshimiwa.”