JE, DUNIA YETU ITAOKOKA?
Misitu
MISITU imeitwa kwa kufaa “mapafu na mfumo unaotegemeza uhai duniani.” Miti hufyonza kaboni dioksidi ambayo inaweza kutuletea madhara. Pia, inatoa oksijeni ambayo ni sehemu muhimu sana ya hewa tunayopumua. Asilimia 80 hivi ya mimea na wanyama wanaishi misituni. Kusingekuwa na uhai bila misitu.
Kwa Nini Tunahitaji Kulinda Misitu Yetu
Kila mwaka, mabilioni ya miti hukatwa ili maeneo hayo yatumiwe kwa ajili ya kilimo. Tangu mwishoni mwa miaka ya 1940, nusu ya misitu duniani imetoweka.
Msitu unapoharibiwa, mimea na wanyama walio ndani yake huangamizwa pia.
Dunia Yetu Imeumbwa Ikiwa na Uwezo wa Kuokoka
Baadhi ya misitu ambayo imekatwa imeonyesha uwezo wake wenye kustaajabisha wa kurudia hali yake ya awali na hata kuongezeka. Hivi karibuni, wataalamu wa mazingira wameshangazwa na jinsi ambavyo miti iliyokatwa imekua haraka na kufanyiza misitu maridadi tena. Fikiria mifano ifuatayo:
-
Watafiti wamechunguza ardhi ya misitu iliyokatwa kwa ajili ya kilimo na kisha kutelekezwa. Utafiti katika maeneo 2,200 ya Amerika na Afrika Magharibi, ulionyesha kwamba udongo wa maeneo hayo ungeweza tena kuwa na misitu ndani ya miaka kumi.
-
Kulingana na utafiti uliochapishwa na gazeti la Science, watafiti wanakadiria kwamba ndani ya miaka 100, misitu hiyo inaweza kurudia hali iliyokuwa nayo kabla ya miti kukatwa.
-
Hivi karibuni, wanasayansi nchini Brazili walichunguza ikiwa misitu ya asili hukua kwa kasi zaidi inapolinganishwa na misitu inayopandwa na wanadamu.
-
Likizungumzia utafiti huo, gazeti la National Geographic linasema hivi: “Wanasayansi walifurahi walipogundua kwamba hakukuwa na uhitaji wa kupanda miti.” Baada ya miaka mitano tu, maeneo ambayo hayakuwa yamepandwa miti, “yalikuwa na miti mingi ya asili.”
Hatua Zinazochukuliwa Sasa
Ulimwenguni pote, jitihada zimefanywa ili kutunza misitu iliyopo na kurudisha ile iliyoharibiwa. Kama matokeo, kulingana na Umoja wa Mataifa, “ukataji miti umepungua kwa asilimia 50 duniani,” ndani ya miaka 25 iliyopita.
Hata hivyo, jitihada hizo hazitoshi kuokoa misitu yetu. Ripoti iliyotolewa na shirika la Global Forest Watch inasema: “Idadi ya misitu inayoharibiwa haijabadilika sana katika kipindi cha miaka michache iliyopita.”
Ukataji wa miti usio halali ni biashara inayoingiza mabilioni ya dola za Marekani, na jambo hilo ni chanzo cha uharibifu wa misitu ya mvua.
Sababu za Kuwa na Tumaini —Biblia Inasema Nini
“Yehova a Mungu akachipusha ardhini kila mti wenye kupendeza macho na unaofaa kwa chakula.”—Mwanzo 2:9.
Muumba wa misitu yote, aliiumba ikiwa na uwezo wa asili wa kujirekebisha kutokana na uharibifu unaosababishwa na wanadamu. Anataka kuitunza na kuidumisha misitu yetu pamoja na mifumo yake bora ya mazingira.
Biblia inasema kwamba Mungu hataruhusu wanadamu wenye ubinafsi waiharibu dunia yetu na viumbe walio ndani yake. Ona makala yenye kichwa “Mungu Anaahidi Kwamba Dunia Yetu Itaokoka,” katika ukurasa wa 15.
a Yehova ni jina la kibinafsi la Mungu.—Zaburi 83:18.