JE, NI KAZI YA UBUNI?
Mng’ao wa Bluu wa Beri aina ya Pollia
BERI ndogo aina ya Pollia condensata, inapatikana barani Afrika. Beri hii ina mwonekano wa bluu unaong’aa sana kuliko mmea mwingine wowote. Hata hivyo, haina rangi ya bluu. Hivyo basi, ni nini hufanya iwe na mng’ao wa bluu?
Fikiria: Chembe zilizo kwenye ngozi ya beri zina kuta zenye nyuzinyuzi nyembamba sana ambazo zimepangwa kama safu ya njiti za kiberiti. Nyuzinyuzi hizo hufanyiza matabaka, kila tabaka likiwa limepinda kidogo ukilinganisha na la chini yake, na hivyo kufanyiza umbo la springi. Nyuzinyuzi hizo hazina rangi ya bluu. Lakini huonekana kuwa za bluu kwa sababu ya jinsi zilivyopangwa. Hivyo, kinachotokeza mwonekano wenye kung’aa, unaobadilika-badilika si rangi bali ni mpangilio wa nyuzinyuzi. Chembe nyingi huonekana kuwa za bluu. Lakini zinapotazamwa kutoka pande tofauti-tofauti, zinaonekana kuwa za kijani, waridi, au njano ikitegemea matabaka hayo. Kwa kuongezea, zinapochunguzwa kwa makini, beri hizo huonekana kuwa na madoadoa kama vile rangi kwenye skrini ya kompyuta.
Kwa sababu hazina rangi, beri hizo hazipotezi mng’ao wake wa bluu hata zinapodondoka. Kwa kushangaza, beri fulani ambazo ziliokotwa karne moja hivi iliyopita bado zinang’aa kama zilizochumwa hivi karibuni! Watafiti wanasema kuwa beri hizo huvutia ndege ingawa hazina sehemu yoyote inayoweza kuliwa.
Wanasayansi wanaamini kwamba huenda wakaiga beri aina ya Pollia kutengeneza rangi zisizopauka na karatasi ambazo haiwezekani kuzighushi.
Wewe una maoni gani? Je, mng’ao wa bluu wa beri aina ya Pollia ulijitokeza wenyewe tu? Au ulibuniwa?