Juhabahari Samaki Mwenye Makao ya Pekee
JUHABAHARI ni kati ya samaki wachache ambao huwavutia sana watu. Huenda tunavutiwa na rangi zao maridadi, ambazo zinatukumbusha kuhusu wachekeshaji wanaovalia mavazi yenye madoido. Au huenda tunastaajabishwa na makao yao, yaani, katikati ya anemone, mimea ya baharini yenye minyiri inayochoma. Haishangazi kwamba jina jingine la juhabahari ni samaki wa anemone.
Kama tu waigizaji maarufu, juhabahari hawaogopi kupigwa picha. Wapiga-mbizi hawapati shida kuwapiga picha juhabahari kwa kuwa samaki hao hawana aibu na hupenda kuwa karibu na makao yao.
Kinachostaajabisha hata zaidi, ni kwamba juhabahari huishi katika maeneo yanayoonekana kuwa hatari. Kuishi kwenye mimea ya anemone ambayo ina minyiri yenye sumu, ni kama kuishi katika tundu la nyoka. Licha ya hali hiyo, juhabahari na anemone ni kama chanda na pete. Ni nini kinachofanya uhusiano huo wa pekee ufanikiwe?
WANAISHI KWA KUTEGEMEANA
Kama ilivyo kwa uhusiano wowote ule, juhabahari na anemone hutegemeana.
Juhabahari huitegemea mimea hiyo ili waendelee kuishi. Wataalamu wa viumbe wa baharini wamethibitisha kwamba samaki hao hawawezi kuishi peke yao bila anemone. Wao si waogeleaji stadi, kwa hiyo pasipo ulinzi wa mmea huo, wanaweza kuwa windo rahisi kwa samaki wengine. Hata hivyo, kwa kuishi katikati ya minyiri ya anemone, na kukimbilia ndani yake wanapotishwa, juhabahari wanaweza kuishi mpaka miaka kumi.Mimea hiyo huandaa makao na mahali salama pa kutagia mayai kwa juhabahari. Wao hutaga mayai kwenye mmea waliouchagua, na kisha dume na jike hushirikiana kuyalinda. Baada ya muda, samaki wachanga huonekana wakiogelea jirani ya mmea huo.
Mmea wa anemone unanufaikaje kutokana na uhusiano huo? Juhabahari huilinda mimea hiyo dhidi ya samaki kipepeo ambao wanapenda kula minyiri ya mimea hiyo. Kwa mfano, kuna jamii fulani ya anemone ambayo haiwezi kabisa kuishi bila juhabahari. Watafiti walipomwondoa juhabahari, mmea huo ulipotea ndani ya saa 24. Samaki kipepeo alikuwa ameula mmea huo.
Pia, inaonekana kwamba juhabahari huitegemeza mimea hiyo. Samaki huyo hutoa kemikali aina ya amonia ambayo huboresha ukuzi wa anemone. Kwa upande mwingine, juhabahari wanapoogelea katikati ya minyiri ya mimea hiyo, wanaisaidia kupata maji yenye hewa ya oksijeni.
KUISHI MAHALI AMBAPO WENGINE HUOGOPA
Ngozi ya juhabahari ndio siri ya ulinzi wao. Ute wenye utelezi ulio kwenye ngozi yao huwalinda ili wasichomwe na minyiri ya anemone. Ute huo huifanya mimea ya anemone ihisi kana kwamba juhabahari ni wa jamii yao. Hiyo ndiyo sababu mtaalamu mmoja wa viumbe wa baharini, anasema kwamba juhabahari ni “samaki aliyejivika mavazi ya anemone.”
Utafiti fulani unaonyesha kwamba samaki huyo hupitia hatua kadhaa anapochagua anemone mpya ili kuwa makao yake. Samaki huyo anapofika kwenye mmea huo kwa mara ya kwanza, anaugusagusa kwa saa chache. Kadiri anavyofanya hivyo, ute wake unajipatanisha na sumu ya anemone hiyo. Bila shaka, atachomwa chomwa mara kadhaa katika hatua hii ya kujipatanisha. Lakini baada ya hapo, wanapatana kabisa.
Tunaweza kujifunza mengi kuhusu ushirikiano kwa kuchunguza uhusiano huo. Watu kutoka tamaduni tofauti wanaweza kupata matokeo mazuri sana katika miradi mbalimbali ikiwa tu watashirikiana na kutegemeana. Kama juhabahari, sisi pia tunaweza kuchukua muda kuzoea kufanya kazi na wengine, hata hivyo, tutapata matokeo mazuri.