Jitihada ya Kutokeza Jamii Kamilifu
Jitihada ya Kutokeza Jamii Kamilifu
LINGEKUWA jambo zuri kama nini kuona ulimwengu bora, uliojaa watu wasio na maumivu, magonjwa, na ulemavu! Jamii ya ulimwenguni pote isiyo na uhalifu wala migogoro. Familia ya kibinadamu isiyokumbwa na kifo.
Pasipo shaka, kutimiza miradi hiyo kungehitaji mabadiliko makubwa katika wanadamu wenyewe. Dhana kuhusu namna ya kuboresha jamii ya kibinadamu si ngeni. Miaka 2,300 iliyopita, mwanafalsafa Mgiriki Plato aliandika hivi: “Wanaume bora wapaswa kuoa wanawake bora kwa wingi iwezekanavyo, na wale wa hali ya chini waoane mara haba iwezekanavyo.” Lakini, ni hivi majuzi tu ndipo jitihada za kuboresha familia ya kibinadamu zilipopamba moto. Taaluma hiyo iliitwa yujeniki (sayansi ya uzalishaji wa watoto bora).
Neno “yujeniki” lilitungwa mnamo mwaka wa 1883 na Sir Francis Galton, mwanasayansi Mwingereza aliye binamu ya Charles Darwin. Neno hilo latokana na maneno ya Kigiriki yanayomaanisha “uzao wa pekee” au “urithi bora.” Galton alijua kwamba maua na wanyama mbalimbali wangeweza kuboreshwa kupitia kwa uzalishaji wa jamii bora. Je, wanadamu hawawezi kuboreshwa kwa kutumia mbinu kama hizo? Galton aliamini kwamba inawezekana. Alisababu kwamba endapo kiasi kidogo cha gharama na jitihada zitumiwazo kuzalisha farasi na ng’ombe zingetumiwa “kuboresha jamii ya kibinadamu,” “kikundi cha watu bora wenye akili sana,” kingetokezwa.
Galton aliyeathiriwa na maandishi ya Darwin, alisababu kwamba wakati wa wanadamu kuelekeza mageuzi yao wenyewe ulikuwa umewadia. Katika miongo ya mapema ya karne ya 20, dhana za Galton zilipendwa mno na wanasiasa, wanasayansi, na wataalamu huko Ulaya na Marekani. Kiongozi wa taifa moja lenye nguvu alidhihirisha dhana zilizopendwa wakati huo alipoandika hivi: “Jamii haina wajibu wa kuruhusu watu wasiofaa kuzaana. . . . Kikundi chochote cha wakulima watakaozuia mifugo yao bora kuzaana, na kuruhusu mifugo yenye kasoro kuongezeka kwa wingi, watashughulikiwa kama wenye kichaa. . . . Siku moja tutang’amua kwamba wajibu wa msingi wa raia mwema
wa jamii inayofaa ni kuzaa wazao wa jamii hiyo duniani, na kwamba hatuna sababu ya kuruhusu raia wenye kasoro kuzaana.” Maneno hayo yaliandikwa na rais wa 26 wa Marekani, Theodore Roosevelt.Katika maonyesho ya bidhaa na minada huko Uingereza na Marekani, sheria za urithi wa chembe kwa kawaida zilionyeshwa kwenye ubao ulio wima uliokuwa na nungubandia waliokufa na kujazwa vitu ngozini. Walipangwa ili kuonyesha urithi wa rangi ya manyoya kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Somo lilidhihirishwa waziwazi na maandishi yaliyoambatana na maonyesho hayo. Chati moja ilisema: “Hali za wanadamu zisizofaa kama vile akili punguani, kifafa, uhalifu, kichaa, ulevi, ufukara na tabia nyinginezo nyingi husitawi katika familia mbalimbali nazo hurithiwa kama rangi inavyorithiwa na nungubandia.” Bango jingine la maonyesho liliuliza hivi: “Sisi Wamarekani tutakuwa waangalifu kuhusu ukoo bora wa nguruwe na kuku na ng’ombe wetu hata lini—huku tukiacha urithi wa watoto wetu uamuliwe na nasibu?”
Sayansi ya Uzalishaji wa Watoto Bora Yatumiwa
Mambo hayo hayakuwa tu ya kinadharia. Makumi ya maelfu ya “watu wasiofaa” huko Amerika Kaskazini na Ulaya walifungwa uzazi. Bila shaka, kubainisha ni nani au ni nini kisichofaa kulitegemea hasa maoni ya watu wenye mamlaka ambao waliamua kufunga watu uzazi kwa nguvu. Mathalani, katika jimbo la Missouri, Marekani, kulikuwa na pendekezo la kutungwa kwa sheria ya kufunga uzazi “wale wanaopatikana na hatia ya kuua, kubaka, unyang’anyi, wizi wa kuku, ulipuaji wa bomu, au wizi wa magari.” Ujerumani ya Nazi ilifanya mengi zaidi katika jitihada yake potovu ya kuwa na jamii bora kupita zote. Baada ya kuwafunga uzazi kinguvu watu wapatao 225,000, mamilioni wengine—Wayahudi, Wajipsi, walemavu, na watu wengine “wasiofaa”—waliangamizwa kwa kisingizio cha uzalishaji wa watoto bora.
Kwa sababu ya ukatili wa enzi za Wanazi, sayansi ya uzalishaji wa watoto bora ikawa na sifa mbaya, na wengi walitumaini kwamba taaluma hiyo ilikuwa imekomeshwa kabisa, na kusahaulika kana kwamba ilizikwa pamoja na mamilioni ya watu waliouawa kwa sababu yake. Hata hivyo, katika miaka ya 1970, ripoti kuhusu maendeleo katika taaluma mpya ya biolojia ya molekuli zilisambaa kote. Baadhi
ya watu walihofu kwamba maendeleo hayo yangerejesha tena dhana zilizopotosha Ulaya na Amerika Kaskazini mwanzoni mwa karne. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1977 mwanabiolojia mmoja mashuhuri aliwaonya hivi wafanyakazi wenzi kwenye mkutano wa umma wa Taasisi ya Kitaifa ya Sayansi uliohusu DNA yenye mchanganyo: “Utafiti huu utatuleta karibu zaidi na sayansi ya kurekebisha chembe za urithi za watu. Watafiti hujaribu kutafuta njia ya kutokeza watoto wenye sifa zinazofaa kwa kutumia sayansi hiyo. . . . Katika kampeni ya Wanazi watoto waliofaa walikuwa na nywele zenye rangi ya kimanjano, macho ya samawati na chembe za urithi za Waarya.”Kulinganisha maendeleo katika sayansi ya kurekebisha chembe za urithi na mpango wa Hitler wa kuzalisha watoto bora kwaweza kuonwa na wengi leo kuwa jambo la kipumbavu. Miaka 60 iliyopita, watu walitaka mno jamii bora. Siku hizi watu hunena juu ya kuboresha afya na hali ya maisha. Sayansi ya kale ya kuzalisha watoto bora ilitokana na siasa na kuchochewa na ushupavu na chuki. Maendeleo mapya katika utafiti wa chembe za urithi huchochewa na faida ya kibiashara na tamaa ya watu ya kuwa na afya bora. Ijapokuwa mambo hayo yanatofautiana sana, mradi wa kubadili watu wapatane na upendezi wetu binafsi wa sifa za urithi walingana sana na sayansi ya kale ya kuzalisha watoto bora.
Kubadili Jamii Kupitia kwa Sayansi
Hata sasa hivi, kompyuta zenye uwezo mkubwa zinachunguza umbile la chembe za urithi za mwanadamu hatua kwa hatua—maagizo kamili yaliyo katika chembe zetu za urithi yanayoelekeza ukuzi wetu na sehemu kubwa ya utu wetu. Kompyuta hizo zinaorodhesha kwa uangalifu makumi ya maelfu ya chembe za urithi zilizo katika DNA ya mwanadamu. (Ona sanduku “Wachunguzi wa DNA.”) Wanasayansi wanatabiri kwamba baada ya kukusanya na kuhifadhi habari hizo zote, zitatumiwa wakati ujao kuwa msingi wa kuelewa umbile na tiba ya mwanadamu. Na wanasayansi wanatumaini kwamba mafumbo ya chembe za urithi za mwanadamu yanapoeleweka, itakuwa rahisi kurekebisha au kuondoa chembe za urithi zenye kasoro.
Madaktari wanatarajia kwamba utafiti wa chembe za urithi utatokeza dawa mpya salama zenye nguvu zaidi za kuzuia na kutibu magonjwa. Yamkini tekinolojia hiyo itamwezesha daktari kuchunguza maagizo ya chembe zako za urithi na kuamua mapema dawa inayoweza kukutibu.
Mbali na manufaa hayo ya kitiba, wengine wanaiona sayansi ya kurekebisha chembe za urithi kuwa njia ya kutatua matatizo ya kijamii. Tangu vita ya ulimwengu ya pili hadi katikati ya miaka ya 1990, wataalamu walisisitiza kwamba matatizo ya kijamii yangeweza kupunguzwa kwa kurekebisha uchumi na vyuo na kuboresha mazingira wanamoishi watu. Lakini, matatizo ya kijamii yamezidi sana katika miaka ya karibuni. Watu wengi wanaamini kwamba chembe za urithi ndizo chanzo cha matatizo hayo. Na sasa wengine huamini kwamba chembe za urithi huathiri sana tabia za mtu mmoja-mmoja na za vikundi vya watu kuliko mazingira.
Vipi kifo? Kulingana na watafiti, hata utatuzi wa tatizo hilo hutegemea kurekebisha DNA zetu. Tayari wanasayansi wamerefusha maradufu maisha ya nzi-tunda na ya minyoo, kwa kutumia mbinu wanazodai huenda zikatumiwa kwa wanadamu siku moja. Msimamizi wa shirika la Human Genome Sciences Inc. alisema: “Hii ndiyo mara ya kwanza kwetu kuwazia kutokufa kwa mwanadamu.”
Je, Ni Watoto Waliobuniwa Kulingana na Mapendezi ya Wazazi?
Ripoti za kusisimua kuhusu mambo yanayofanywa na yale yatakayofanywa miaka ijayo hufanya iwe rahisi kupuuza mipaka iliyopo na matatizo yanayoweza kusababishwa na tekinolojia hizo mpya. Kwa kielezi, acheni turejelee habari ya watoto wachanga. Kuchunguza chembe za urithi tayari ni zoea la kawaida. Njia inayotumiwa kwa kawaida ilibuniwa miaka ya 1960. Daktari huchoma sindano tumbo la uzazi la mwanamke mjamzito na kutoa kiasi kidogo cha maji ya mimba yanayozingira kijusu. Maji hayo yaweza kuchunguzwa kuona iwapo kijusu kina mojawapo ya kasoro nyingi za chembe za urithi, kutia ndani upunguani wa kuzaliwa na kichwa bapa na ulemavu wa uti wa mgongo. Kwa kawaida uchunguzi huo hufanywa baada ya juma la 16 la mimba. Uchunguzi wa karibuni zaidi huonyesha kindani umbile la chembe za urithi za kiinitete kati ya juma la sita na la kumi la mimba.
Uchunguzi huo huwawezesha madaktari kugundua kasoro nyingi, lakini ni takriban asilimia 15 tu ya kasoro hizo ziwezazo kurekebishwa. Uchunguzi unapofunua kasoro ya urithi
au unapotatanisha, wazazi wengi hukabili uamuzi mzito sana—je, watoe mimba hiyo, au wamzae mtoto? Kichapo The UNESCO Courier chasema: “Licha ya uchunguzi chungu nzima wa DNA—kila uchunguzi ukiwa umeidhinishwa na ukiwa unaleta faida—hadi sasa elimu ya chembe za urithi imeshindwa kutimiza ahadi ya kuvumbua tiba ya chembe za urithi iliyojivunia. Madaktari wanachunguza hali na kasoro wasizoweza kutibu. Kwa hiyo mara nyingi wao hupendekeza utoaji-mimba kuwa suluhisho.”Bila shaka, kadiri sayansi ya kurekebisha chembe za urithi inavyokuwa na matokeo, ndivyo madaktari wanavyotarajia kuwa na uwezo zaidi wa kugundua na kurekebisha kasoro za chembe za urithi ambazo husababisha au huelekea kuwaletea wanadamu magonjwa mbalimbali. Pia wanasayansi wanatumaini kwamba hatimaye wataweza kutia chembeuzi zisizo za asili kwenye kiinitete cha mwanadamu ili kukilinda dhidi ya magonjwa kama vile ugonjwa wa kutetemeka, UKIMWI, ugonjwa wa sukari, na kansa ya tezi-kibofu na ya matiti. Hivyo mtoto atazaliwa akiwa na mfumo wa kinga wenye nguvu. Pia wanatarajia kubuni dawa “zitakazoboresha” kiinitete kinachokua, labda kwa
kurekebisha chembe za urithi ili kuzidisha uwezo wake wa akili au kuboresha kumbukumbu lake.Ingawa wanasayansi wenye matumaini makubwa hung’amua kwamba itachukua muda mrefu kabla ya wazazi kuweza kuchagua mtoto wanayemtaka kutoka kwenye orodha, watu wengi huvutiwa sana na taraja la kuzaa mtoto anayewafaa kabisa. Baadhi ya watu hubisha kwamba kutotumia tekinolojia kuondoa kasoro za chembe za urithi ni jambo lisilofaa kabisa. Wao husababu kwamba ikiwa si kosa kumpeleka mtoto wako kwenye shule bora na kwa madaktari bora, mbona usijaribu kupata mtoto bora iwezekanavyo?
Shaka Kuhusu Wakati Ujao
Lakini wengine wana shaka. Kwa mfano, kitabu The Biotech Century chasema: “Kama ugonjwa wa sukari, upungufu wa damu, na kansa zitazuiwa kwa kurekebisha chembe za urithi za watu, mbona wasianze na ‘kasoro’ nyingine ndogo kama: kutoweza kuona mbali, upofu-rangi, kutoweza kusoma vizuri, kunenepa kupita kiasi, na kutumia mkono wa kushoto? Kwa kweli, ni nini kitakachozuia jamii
kuamua kwamba rangi fulani ya ngozi ni kasoro?”Makampuni ya bima yatatafuta sana habari za chembe za urithi. Vipi ikiwa uchunguzi wa kabla ya kuzaa wafunua uwezekano wa mtoto kuwa na kasoro? Je, makampuni ya bima yatamshurutisha mama huyo atoe mimba? Na iwapo akataa, je, watamnyima bima?
Makampuni ya kemikali, madawa, na ya sayansi ya kurekebisha chembe za urithi hushindana kupata kibali cha kuchunguza viumbe na chembe za urithi vilevile njia za kuweza kuzirekebisha. Bila shaka sababu inayowachochea ni ya kifedha—kuchuma fedha kutokana na tekinolojia ya wakati ujao. Wataalamu wengi wa elimu-adili ya utafiti wa kibiolojia wanahofu kwamba jambo hilo laweza kutokeza “yujeniki ya wateja,” ambayo humaanisha kwamba wazazi watashurutishwa kuchagua watoto “wenye chembe za urithi zinazokubalika.” Ni rahisi kuwazia jinsi utangazaji utakavyotimiza fungu kubwa katika jambo hilo.
Pasipo shaka, yaelekea kwamba tekinolojia hiyo mpya haitapatikana kwa urahisi katika nchi maskini ulimwenguni. Tayari nchi nyingi ulimwenguni hazina utunzi wa msingi kabisa wa afya. Hata katika nchi zilizositawi sana, yamkini ni watu matajiri tu watakaoweza kupata tiba ya chembe za urithi.
Jamii Kamilifu
Vichapo chungu nzima vya utafiti wa sayansi ya kurekebisha chembe za urithi, hurudia-rudia msemo “kutimiza fungu la Mungu.” Kwa kuwa Mungu ndiye Mbuni na Muumbaji wa uhai, inafaa kuzingatia kusudi lake kuhusu jitihada ya kutafuta ukamilifu. Kitabu cha Biblia cha Mwanzo husema kwamba baada ya kuumba uhai duniani, ‘Mungu aliona kila kitu alichokifanya, na tazama, kilikuwa chema sana.’ (Mwanzo 1:31) Wenzi wa kwanza wa kibinadamu walikuwa na chembe za urithi kamilifu. Kwa sababu ya kumwasi Mungu, walijiletea na kuwaletea wazao wao kutokamilika na kifo.—Mwanzo 3:6, 16-19; Waroma 5:12.
Yehova Mungu anakusudia kukomesha magonjwa, kuteseka, na kifo. Alifanya uandalizi wa kuwaokoa wanadamu kutoka kwa matatizo hayo kale sana. Kitabu cha Biblia cha Ufunuo chatabiri wakati ambapo Mungu ataingilia mambo ya wanadamu. Kuhusu wakati huo, twasoma hivi: “[Mungu] atafuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala ombolezo wala kupaaza kilio wala umivu halitakuwapo tena kamwe. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.” Mabadiliko hayo makubwa hayataletwa na mafanikio ya kisayansi ya wanadamu, kwani wengi wao hata hawakubali kwamba Mungu yupo, sembuse kumsifu. La, andiko laendelea kusema: “Na Yeye [Yehova Mungu] aketiye juu ya kiti cha ufalme akasema: ‘Tazama! Mimi ninafanya vitu vyote kuwa vipya.’”—Ufunuo 21:4, 5.
[Blabu katika ukurasa wa 5]
Baada ya kuwafunga uzazi kinguvu watu wapatao 225,000, katika Ujerumani ya Nazi, mamilioni wengine “wasiofaa” waliangamizwa kwa kisingizio cha uzalishaji wa watoto bora
[Blabu katika ukurasa wa 6]
Madaktari wanatarajia kwamba utafiti wa chembe za urithi utatokeza dawa mpya salama zenye nguvu zaidi za kuzuia na kutibu magonjwa
[Blabu katika ukurasa wa 11]
Tangu kutokezwa kwa Dolly, wanasayansi wametokeza makumi ya wanyama mbalimbali—wote kutoka kwa chembe zilizokomaa. Je, tekinolojia hiyo yaweza kutumiwa kutokeza wanadamu wakomavu kwa chembe bila kujamiiana?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Je, Wanadamu Wanaweza Kutokezwa kwa Chembe Bila Kujamiiana?
Mnamo mwaka wa 1997 kondoo aitwaye Dolly alitangazwa na vyombo vya habari kotekote ulimwenguni. Kwa nini Dolly akawa wa pekee? Alikuwa mamalia wa kwanza kutokezwa bila kujamiiana kutoka kwa chembe iliyokomaa, iliyotolewa kwa titi la kondoo jike. Hivyo Dolly akawa “pacha” mchanga wa kondoo aliyetolewa chembe hiyo. Kabla ya Dolly, kwa miongo mingi wanasayansi walikuwa wametokeza wanyama kutokana na chembe za kiinitete. Wengi hawakufikiri kwamba inawezekana kurekebisha umbile la chembe inayotoka kwa mamalia mkomavu na kutokeza mnyama mwingine mwenye umbile sawia la chembe za urithi. Kutokeza kiumbe kutoka kwa chembe iliyokomaa hufanya iwezekane kujua mapema jinsi yule mchanga atakavyokuwa.
Lengo la wanasayansi waliomtokeza Dolly kutoka kwa chembe bila kujamiiana lilikuwa kuboresha wanyama wanaofugwa ili wawe chanzo cha madawa yanayopatikana katika maziwa yao. Ripoti ya kufaulu kwa wanasayansi hao ilichapishwa kwa mara ya kwanza mwezi wa Februari 1997, katika gazeti la kisayansi Nature, chini ya kichwa “Mzao Mwenye Kujitegemea Atokezwa kwa Chembe Zilizokomaa za Mamalia na za Kijusu.” Upesi vyombo vya habari vikapendezwa mno na ripoti hiyo na maana yake. Majuma mawili baadaye jalada la gazeti Time lilikuwa na picha ya Dolly ikiambatana na kichwa kikuu “Je, Mtu Mwingine Mwenye Umbile Sawa Nawe Atawahi Kutokezwa kwa Chembe Zako Bila Kujamiiana?” Juma hilohilo, gazeti Newsweek lilichapisha mfululizo wa makala kuu yenye kichwa “Je, Tunaweza Kutokeza Wanadamu kwa Chembe Bila Kujamiiana?”
Baada ya Dolly, wanasayansi wametokeza makumi ya wanyama mbalimbali—wote kutoka kwa chembe zilizokomaa. Je, tekinolojia hiyo yaweza kutumiwa kutokeza wanadamu wakomavu kwa chembe bila kujamiiana? Ndiyo, wasema wanabiolojia fulani. Je, imefanywa? Bado. Ian Wilmut, mwanasayansi Mwingereza aliyeongoza kikundi kilichomtokeza Dolly, asema kwamba kutokeza viumbe kutoka kwa chembe bila kujamiiana kwa sasa ni “njia isiyo na matokeo kabisa,” kwani idadi ya vijusu vinavyokufa ni mara kumi zaidi ya vinavyokufa katika uzalishaji wa asili.
Baadhi ya watu hujiuliza, ‘Lakini namna gani ikiwa mtu ataboresha mbinu hiyo na atokeze, tuseme, Hitler wengi kutoka kwa chembe?’ Huku akijaribu kupunguza hofu hiyo, Wilmut asema kwamba ingawa mtoto aliyetokezwa kwa chembe bila kujamiiana atakuwa pacha mwenye umbile sawa la chembe za urithi na mtu ambaye kutoka kwake chembe hiyo ilitwaliwa, mwanadamu aliyetokezwa kwa chembe ataathiriwa na mazingira na atasitawisha utu wa pekee kama inavyokuwa kwa mapacha wa asili.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Wachunguzi wa DNA
Mwili wa binadamu umefanyizwa kwa takriban chembe trilioni 100. Nyingi za chembe hizo zina kiini. Ndani ya kila kiini mna visehemu 46 vinavyoitwa chembeuzi. Kila chembeuzi ina molekuli moja iliyojipinda sana, inayoshabihi uzi ambayo huitwa DNA. Inakadiriwa kwamba ndani ya DNA mna chembe za urithi zipatazo 100,000, zilizopangwa mfano wa miji na majiji pembeni mwa barabara kuu. Chembe zetu za urithi huamua hasa kila jambo mwilini mwetu—ukuzi wetu katika tumbo la uzazi, jinsia na sifa zetu za kimwili, na ukuzi wetu kufikia utu uzima. Wanasayansi wanaamini pia kwamba DNA yetu ina “saa” inayoamua urefu wa maisha yetu.
DNA ya wanyama na ya wanadamu zinafanana sana. Kwa mfano, umbile la chembe za urithi za sokwe hutofautiana na la mwanadamu kwa asilimia 1 tu. Hata hivyo, tofauti hiyo ni mara kumi zaidi ya tofauti iliyopo kati ya DNA ya wanadamu wawili. Ni tofauti hizo ndogo sana zinazoleta sifa nyingi ambazo humfanya kila mmoja wetu awe mtu wa pekee kabisa.
Karibu miaka kumi iliyopita, wanasayansi walianza mradi mgumu—wa kutafuta mpangilio barabara wa kemikali katika DNA ya mwanadamu. Mradi huo, unaoitwa Mradi wa Kuchunguza Chembe za Urithi za Mwanadamu, ni mkubwa na wenye matumaini makubwa, utagharimu mabilioni ya dola za Marekani. Habari ambazo zitakusanywa zitatosha kujaza mabuku yapatayo 200, kila buku likitoshana na kitabu cha simu chenye kurasa 1,000. Ili kupitia habari hizo zote, mtu atahitaji kuzisoma kwa muda wa saa 24 kila siku kwa miaka 26!
Mara nyingi vyombo vya habari husahau kwamba habari hizo zitahitaji kufasiriwa punde tu baada ya kukusanywa. Vifaa vipya vitahitajiwa ili kuchanganua habari hizo. Ni rahisi kutambua chembe za urithi; lakini ni vigumu sana kujua kazi yake na jinsi zinavyoungana ili kumfanyiza mwanadamu. Mwanabiolojia mmoja mashuhuri aliuita Mradi wa Kuchunguza Chembe za Urithi za Mwanadamu, kuwa “Utafiti Tata Sana wa Elimu ya Chembe za Urithi.” Lakini maelezo sahili zaidi ya mradi huo yalidokezwa na mtaalamu wa elimu ya chembe za urithi Eric Lander: “Ni kama orodha ya sehemu za mashine,” yeye asema. “Kama ningekupa orodha ya sehemu za ndege aina ya Boeing 777 yenye sehemu 100,000, sidhani ungeweza kuitengeneza wala hata kuelewa kinachoiwezesha kupaa.”
[Mchoro]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
CHEMBE
KIINI
CHEMBEUZI
DNA
MUUNGANO WA MISINGI