Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Ni Hekima Kutega Uchumi Katika Soko la Hisa?

Je, Ni Hekima Kutega Uchumi Katika Soko la Hisa?

Je, Ni Hekima Kutega Uchumi Katika Soko la Hisa?

“Watu wengi sasa wanatega uchumi katika soko la hisa.”—Newsweek, la Julai 5, 1999.

SOKO la kawaida la hisa sasa ni lenye mchafuko kama tu soko la bidhaa nyingine. Ishara za mikono zisizoeleweka (kwa mgeni) hutumika, habari za siri za kielektroni hutokea na kubadilika kwa kasi sana, na madalali wanashindana kila mmoja asikizwe kwanza katika pilikapilika hizo.

Hata hivyo, watu wengi ambao hapo mbeleni walitatanishwa na soko la hisa, sasa wanatega uchumi katika hisa. Mbona? Kwanza, kupitia Internet watega-uchumi wanaweza kupata mara moja habari za mambo ya fedha, ushauri wa kutega uchumi, na kuwasiliana na madalali. Paul Farrell, mhariri mkuu wa gazeti la Wall Street News, aandika hivi: “Kwa [watega-uchumi mmoja-mmoja], kutega uchumi kupitia Internet ni njia mpya ya kujitajirisha kwa haraka, kujipatia uhuru wa kibinafsi, na kujitegemea kifedha huku wakifanyia kazi hiyo nyumbani mwao.”

Kwa upande mwingine, baadhi ya wataalamu wa mambo ya fedha wana wasiwasi wanapoona watu wenye hamu kubwa ya kutega uchumi katika soko wasilolifahamu vyema. Muuzaji mmoja wa hisa ambaye amefanya kazi hiyo kwa miaka 38 aliliambia Amkeni! hivi: “Watu walio wengi wananunua hisa wakitazamia kuziuza kwa faida, lakini si kutega uchumi. Huenda baadhi yao wakadhani wanatega uchumi, lakini hawajui lolote kuhusu hali ya kampuni wanamonunua na kuuza hisa.”

Ni mambo gani ya kufikiriwa kabla ya kutega uchumi na pesa zako? Kwa kuwa kuna kiasi fulani cha kujasiria katika biashara ya hisa, je, ni sawa na kucheza kamari? Acheni kwanza tuchunguze utendaji katika soko la hisa.

Kununua Hisa

Ili makampuni yaweze kutekeleza wajibu wake wa kifedha, rasilimali au pesa zilizotegwa uchumi zinahitajika. Iwapo kampuni yasitawi sana na rasilimali nyingi zahitajika, huenda wasimamizi wakaamua kuuza hisa zake kwa umma. Kichapo kimoja cha kutoa mwongozo kwa biashara hiyo chaeleza hivi: “Hisa ni sehemu ndogo ya mali ya kampuni. Kwa hiyo unaponunua hisa unamiliki sehemu ya mali ya kampuni hiyo.”

Kwenye soko la kawaida, wauzaji na wanunuzi hukutana na huanza biashara. Vivyo hivyo, soko la hisa ni soko la wanunuzi na wauzaji wa hisa. Kabla ya soka la hisa kuanzishwa, hisa ziliuzwa kupitia madalali kwenye mikahawa na pembeni mwa njia. Uuzaji wa hisa chini ya mti katika barabara iitwayo 68 Wall Street ulikuwa mwanzo wa Soko la Hisa la New York. * Masoko ya hisa sasa yanapatikana katika nchi nyingi. Siku yoyote, na saa yoyote ile, kuna soko la hisa linaloendesha biashara mahali fulani ulimwenguni.

Lazima mtega-uchumi anayenuia kufanya biashara ya hisa afungue akaunti na dalali na kufanya agizo. Leo maagizo ya kununua na kuuza hisa yaweza kufanywa kupitia simu, Internet, au ana kwa ana. Baada ya hapo dalali aweza kuuza au kununua hisa kwa niaba ya mtega-uchumi. Iwapo biashara inafanywa kwenye soko la kawaida, dalali hutuma mfanyakazi ili anunue au auze hisa za mtega-uchumi huyo. Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya masoko ya hisa yanafanya biashara zake zote kupitia kompyuta, ikiwezesha maagizo kutekelezwa muda mfupi sana baada ya dalali kuyapokea. Maagizo yote huwekwa kwenye ubao wa kielektroni—wenye kuonyesha orodha ya bei na habari ya karibuni ya hisa.

Bei ya hisa hutegemea ‘kupiga bei’ sawa na inavyofanywa katika mnada. Bei ya hisa huathiriwa na habari za kibiashara, mapato ya kampuni, pamoja na matazamio ya wakati ujao ya kampuni. Watega-uchumi hutazamia kununua hisa kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu wakati ujao thamani yake iongezekapo. Sehemu ya faida ya kampuni huenda pia ikagawanywa miongoni mwa wenye hisa. Baadhi ya watu hununua hisa kama rasilimali; hali wengine hununua na kuuza hisa kwa ukawaida, wakitazamia kupata faida kutokana na kupanda ghafula kwa bei ya hisa.

Ingawa imekuwa desturi kwa biashara ya hisa kufanywa kupitia simu, kuuza na kununua hisa kupitia Internet kunazidi kupendwa na watu wengi. Gazeti la The Financial Post laripoti kuwa biashara ya hisa kupitia Internet katika Marekani “iliongezeka kutoka hisa 100,000 hivi kwa siku katika mwaka wa 1996 hadi hisa 500,000 kufikia mwisho wa Juni [1999] ikiwakilisha asilimia 16 ya biashara yote yenye kufanywa kwa njia ya kompyuta katika Marekani.” Katika Sweden asilimia 20 ya biashara yote ya hisa katika mwaka wa 1999 ilifanywa kupitia Internet.

Tega Uchumi kwa Hekima

Urahisi wa kufanya biashara ya hisa kupitia Internet na kupata habari ambayo hapo awali ilijulikana tu kwa madalali na mabingwa wa biashara hiyo kumewachochea watega-uchumi mmoja-mmoja kufanya biashara hii kila siku, yaani kufanya kununua na kuuza hisa kuwa kazi ya wakati wote. Watu fulani wameacha kazi zenye mshahara mkubwa ili kuuza hisa kwa wakati wote. Kwa nini? “Kivutio kiko wazi,” laeleza gazeti la Money. “Huna bwana-mkubwa wa kukusimamia, tena una uhuru kamili wa kujiamulia wakati wa kuuza au kununua, na kuna uwezekano—kama inavyodhaniwa—wa kupata pesa nyingi.” Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 35 aliyeacha kazi yenye mshahara wa dola za Marekani 200,000 kwa mwaka ili afanye biashara ya hisa nyumbani kwake alinukuliwa akisema hivi: “Ni wapi penginepo unapoweza kuwa bila orodha ya bidhaa za kuuza, bila wafanyakazi, hulipi kodi, unalotakiwa kufanya tu ni kuingiza habari kwa kompyuta na unapata pesa?”

Wataalamu wanaonya kuwa biashara ya hisa sio rahisi kama watega-uchumi wapya wanavyodhania. Daktari mmoja wa magonjwa ya akili aliye mtaalamu wa mkazo unaotokana na biashara alisema hivi: “Biashara huonekana kwa kudanganya kuwa ni rahisi, lakini mimi naona kuwa ndiyo njia ngumu zaidi ya kupata pesa.” Habari chungu nzima za kifedha na ushauri una athari mbaya pia. Paul Farrell, aliyenukuliwa awali, asema hivi: “Matokeo ya mfuriko wa daima wa habari unaoelekezwa kwa mtega-uchumi mmoja-mmoja—mtega-uchumi aliye peke yake na kampuni ya kuuza hisa—ni kwamba wote wanaathiriwa sana kiakili: kuvunjika moyo, kuvurugika hisia, na kupatwa na mikazo.”

Kuwa mwenye hakika kupita kiasi kwaweza kuwa mtego. Mwandikaji wa mambo ya kifedha Jane Bryant Quinn aonya juu ya mtazamo hatari unaoenea miongoni wa wafanyabiashara: “Unadhani kwamba mradi kazi yako inaendelea vizuri—au ungali unafanya kazi yako kwa kompyuta—hali yoyote mbaya haiwezi kutokea. Unaweza kurekebisha hali mapema.” Anaongezea kusema hivi: “Tunaanza kufikiri kwamba sisi pia ni wataalamu eti kwa sababu tunaweza kupata habari inayotumiwa na wataalamu.” Licha ya kusambazwa sana kwa habari za watu ambao wamekuwa matajiri haraka kupitia biashara ya hisa, biashara ya hisa ina hatari zake. Baadhi ya watega-uchumi wamefanikiwa sana. Wengine wamepata hasara kubwa.

Wataalamu wa mambo ya kutega uchumi wanashauri watega-uchumi wapya wafikirie utendaji wa awali wa kampuni na matarajio yake ya wakati ujao, uuzaji wa bidhaa zake, ushindani na kampuni nyingine, na hali nyingine kabla ya kununua hisa za kampuni hiyo. Habari hizi zaweza kupatikana kwa madalali au mashirika mengine ya kifedha. Watega-uchumi walio wengi huwasiliana na wataalamu wa mambo ya kifedha kabla ya kununua hisa. * Akichunguza utendaji wa awali wa kampuni, mtega-uchumi anaweza kuhakikisha kwamba pesa zake hazitumiwi kutegemeza miradi isiyofaa.—Ona Amkeni! la Februari 8, 1962, ukurasa wa 21-23 [Kiingereza].

Ni Bahati-Nasibu ya Mashirika?

Kwa sababu ya hali ya kujasiria katika biashara ya hisa, je, kununua hisa ni sawa na kucheza kamari? Kiasi fulani cha kujasiria kipo katika biashara yoyote ile. Watu fulani hununua nyumba au mashamba bila kuwa na uhakika kama bei yake itapanda au kushuka wakati ujao. Wengine huweka pesa zao akiba katika benki wakitumaini kwamba pesa zao ziko salama. Ingawa soko la hisa ni lenye kutatanisha, mtega-uchumi hununua hisa za kampuni fulani akitumaini kampuni hiyo itastawi na hisa zake kuongezeka bei.

Kutega uchumi kwa jinsi hiyo ni tofauti na kucheza kamari kwa sababu mwenye hisa amenunua sehemu fulani ya kampuni hiyo. Hisa hizo zaweza kuuzwa kwa mtu mwingine au kuwekwa akiba kukiwa na matumaini ya hisa hizo kuongezeka bei. Jambo hilo si sawa na mtu anayechezea pesa zake kamari kwenye kasino au katika mchezo wa bahati-nasibu. Haidhuru hatari ya kupoteza pesa zake, mcheza-kamari hujaribu kubashiri ushindi usio na hakika.

Mtega-uchumi aweza kujasiria kwa kadiri gani? Hilo ni jambo la kuamua kibinafsi. Bila shaka si jambo la hekima kujasiria kiasi cha pesa ambacho hauko tayari kupoteza.

Mtazamo Wenye Usawaziko Kuelekea Pesa

Wakiwa na nia ya kutimiza mahitaji yao ya sasa na yale ya wakati ujao, watu fulani wameamua kutega uchumi katika soko la hisa. Kusudi la mtu kufanya maamuzi kama hayo ya kifedha ni muhimu. Jane Bryant Quinn, aliyenukuliwa awali, asema hivi: “Kuwaonea wivu watu ambao bila kutazamia wamekuwa matajiri kupitia biashara ya hisa kwaweza kutufanya tuwe watega-uchumi kwa kusudi lisilofaa.” Maneno hayo yafanana sana na ushauri ulio kwenye barua iliyoandikiwa kijana mmoja yapata miaka 2,000 iliyopita: “Wale waazimiao kuwa matajiri huanguka ndani ya kishawishi na mtego na tamaa nyingi zisizo za akili na zenye kuumiza, ambazo hutumbukiza watu ndani ya uharibifu na uangamizo. Kwa maana kupenda fedha ni mzizi wa mambo mabaya ya namna zote, na kwa kujitahidi kufikilia kupenda huku wengine wameongozwa wapotee njia kutoka kwenye imani na wamejichoma wenyewe kotekote kwa maumivu mengi.”—1 Timotheo 6:9, 10.

Jinsi mtu anavyochagua kutega uchumi kwa pesa zake ni uamuzi wa kibinafsi. Mtega-uchumi mwenye kuongozwa na akili timamu na anayeridhika na vitu vya lazima kwa maisha, ataweza kuweka mambo ya kifedha mahali pake, bila kupuuza madaraka yake ya familia wala mahitaji yake ya kiroho.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Mtajo “Wall Street” kwa kawaida sasa humaanisha masoko ya kifedha kwa ujumla.

^ fu. 17 Si ushauri wote unafaa. Watega-uchumi wapaswa kutahadhari kwamba mshauri wa mambo ya kifedha huenda akawa anaendeleza huduma zake au anaongoza kwa hila mteja wake kwa faida yake mwenyewe.