Je, Mazulia Yanaweza Kukudhuru?
Je, Mazulia Yanaweza Kukudhuru?
WEWE hutumia muda gani ndani ya majengo yenye mazulia yanayofunika sakafu yote? Ripoti moja katika gazeti la New Scientist inaonyesha kwamba huenda mazulia yakasababisha madhara, hasa kwa watoto.
Gazeti hilo lilisema hivi: “Tunapokuwa ndani ya jengo tunaathiriwa na vichafuzi mara 10 hadi 50 kuliko wakati tunapokuwa nje.” John Roberts, mtaalamu wa mazingira huko Marekani, anasema kwamba mavumbi ya mazulia ya nyumba yanaweza kuwa na kiasi kikubwa cha vichafuzi. Vichafuzi hivyo vinatia ndani risasi, kadimiamu, zebaki, dawa za kuua wadudu waharibifu, na kemikali zinazosababisha kansa zinazoitwa polychlorinated biphenol (PCB) na polycyclic aromatic hydrocarbon (PAH).
Inasemekana kwamba dawa za kuua wadudu waharibifu zinazoingizwa nyumbani kwa viatu na miguu ya wanyama-vipenzi zinaweza kuzidisha kiasi cha dawa hizo kwenye zulia mara 400. Vichafuzi hivyo vinaweza kubaki kwa miaka mingi. Kwa kuwa dawa za kuua wadudu waharibifu na kemikali aina za PAH hubadilika kuwa mvuke, hizo huelea hewani kisha hutua tena kwenye mazulia au kwenye sehemu nyingine.
Mara nyingi watoto wachanga hucheza sakafuni kisha huweka vidole vyao mdomoni. Kwa hiyo, vichafuzi hivyo huwaathiri hasa watoto. Kwa kuwa miili ya watoto wachanga huvunja kemikali haraka kuliko ya watu wazima, watoto hupumua kiasi kikubwa cha hewa kuliko watu wazima hata ingawa wao si wazito sana.
Baadhi ya watafiti wanafikiri kwamba kwa kuwa siku hizi nyumba nyingi zina mazulia, huenda ikawa hilo limesababisha watoto wengi zaidi kuugua ugonjwa wa pumu, mizio, na kansa. Roberts anasema hivi: ‘Kiasi cha mavumbi yaliyomo ndani ya nyumba iliyowekwa zulia kila mahali ni mara kumi hivi ya kiasi cha mavumbi yaliyomo ndani ya nyumba iliyowekwa mazulia madogo tu kwenye sehemu chache.’
Roberts anapendekeza kwamba ili mazulia yasisababishe madhara ni lazima uyasafishe kwa mashine inayovuta vumbi kabisa. Kisha, kila juma, kwa kipindi cha majuma kadhaa, safisha sehemu iliyoko karibu na mlango wa kuingia na wa kutoka mara 25, maeneo yanayokanyagwa sana mara 16, na sehemu nyingine zilizobaki mara 8.
Baada ya kufanya hivyo, unaweza kufanya tu nusu ya utaratibu huo uliopendekezwa, na hivyo yaelekea utaweza kupunguza vumbi nyumbani mwako. Roberts anapendekeza pia: “Weka zulia zito la kufutia miguu kwenye milango ya kuingia nyumbani mwako na ufute viatu mara mbili kabla ya kuingia.”