Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Ngoma Inayotoa Milio Elfu Moja”

“Ngoma Inayotoa Milio Elfu Moja”

“Ngoma Inayotoa Milio Elfu Moja”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI SENEGAL

“HUTOA sauti ya mngurumo, sauti ya mkwaruzo, sauti kali na sauti kama ya king’ora. Hutoa minong’ono na huimba. . . . Ni ngoma inayotoa midundo mbalimbali, ngoma inayotoa milio elfu moja.” Ni nini kilichomsisimua mwandishi huyo? Ni ngoma ya Kiafrika inayoitwa djembe.

Ngoma ya djembe hutumiwa sana kucheza ngoma za kitamaduni za makabila fulani ya Afrika Magharibi. Kwa kawaida, ngoma hiyo huchezwa hasa wakati wa matukio mbalimbali ya kitamaduni huko vijijini, kama vile wakati wa arusi, watu wanapokufa, watoto wanapozaliwa, wakati wa sherehe, wakati wa mavuno, na hata nguo mpya zinaponunuliwa.

Ngoma za djembe huwa na ukubwa na maumbo mbalimbali. Muundo wa ngoma hizo hutofautiana katika nchi ya Burkina Faso, Guinea, Mali, na Senegal. Ngoma hizo hutengenezwa kutokana na gogo. Uwazi hufanyizwa katika gogo hilo, kisha linachongwa katika umbo la ngoma. Ngoma nyingine huwa na mapambo machache, lakini nyingine hupambwa kwa michongo mingi.

Fundi wa ngoma akiisha kufanyiza uwazi katika gogo, yeye hulitumia kutengeneza ngoma nzuri sana. Kwanza kabisa, fundi wa ngoma huchonga gogo hilo lenye uwazi na kulipiga msasa hadi linapokuwa na ukubwa wa kutosha kiasi cha kutoa sauti inayotakikana. Huenda fundi huyo pia akapaka mawese ndani ya gogo hilo na kulianika juani ili likauke. Hivyo, ubao huo hudumu kwa muda mrefu.

Sehemu ya juu ya djembe hutengenezwa kutokana na ngozi ya mbuzi ambayo huunganishwa na pete ya chuma. Pete hiyo imeunganishwa kwa kamba na pete nyingine mbili. Fundi wa ngoma hukaza kamba hizo kulingana na sauti anayotaka. Anapoendelea kuikaza ngozi, yeye hucheza ngoma anayopenda ili ahakikishe kwamba imekazika vilivyo.

Waafrika na wageni kutoka nchi za nje huvutiwa na ngoma ya djembe. Ama kweli, unapowaona wanamuziki stadi wakicheza muziki wa kienyeji kwa kutumia ala hiyo, hutaisahau “ngoma inayotoa milio elfu moja.”