Jeshi Lasonga Mbele!
Jeshi Lasonga Mbele!
“Tunaishi Belize katika kijiji kinachoendelea kujengwa na ambacho kimezungukwa na mimea mingi. Asubuhi moja, mwendo wa saa tatu, nyumba yetu ilivamiwa na kikosi cha jeshi. Siafu wengi walimiminika ndani ya nyumba kupitia chini ya mlango na nyufa zote wakitafuta chakula. Hatukuwa na la kufanya ila kutoka nje na kuwapisha mabwana hao kwa saa moja au mbili hivi. Tuliporudi ndani, hatukuona hata mdudu mmoja.”
HILO NI JAMBO LA KAWAIDA kwa watu wengi wanaoishi katika nchi za ukanda wa joto kama Belize, nao hufurahi. Kumbe hiyo ni njia ya kuondoa wadudu kama mende ndani ya nyumba. Na siafu hao hawaharibu nyumba.
Siafu hao hufanya shughuli zao kama wanajeshi. * Badala ya kujenga vichuguu, wadudu hao wanaohama-hama wakiwa mamia ya maelfu hutengeneza makao ya muda. Siafu wengi ajabu huunganisha miguu yao pamoja ili kumzunguka malkia wao na mayai yake. Siafu wengine hutumwa kutafuta chakula, kama vile wadudu na viumbe wadogo kama mijusi. Wao hujipanga katika mstari mrefu wanapofanya hivyo. Siafu wanaoongoza hushambulia kutoka pembeni ili kunasa windo. Wakati huo, siafu walio mbele hawahisi harufu yoyote mbele yao inayopaswa kuwaongoza, na hivyo wao husitasita na kusimama. Siafu walio nyuma huendelea kusonga mbele na kuwasukuma baadhi ya siafu walio mbele. Msukumano huo hufanya kundi hilo lionekane ni kana kwamba linasonga huku na huku.
Siafu hao huendesha shughuli zao kila baada ya siku 36. Wao husonga mbele wakitafuta chakula kwa siku 16, kisha wanatua kwa siku 20 ili malkia atage mayai. Baada ya hapo, wao huhisi njaa na inawabidi waanze mwendo tena. Wanaposonga mbele, wao hujipanga katika mistari yenye upana wa meta 10. Buibui, nge, mbawakavu, vyura na mijusi hukimbia mbele ya siafu hao ili kujiokoa huku ndege wakiwafukuza. Ndege hao huwawinda viumbe hao wanaokimbia lakini hawawadhuru siafu.
Kwenye Mithali 30:24, 25, NW, wadudu kama hao hutajwa kuwa wenye “hekima ya kisilika,” na bila shaka wao ni kati ya viumbe wenye kustaajabisha sana.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Makala hii inazungumzia siafu aina ya Eciton wa Amerika ya Kati na ya Kusini.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Siafu
[Hisani]
© Frederick D. Atwood
[Picha katika ukurasa wa 31]
Wanaunganisha miguu yao pamoja ili kufanyiza daraja
[Hisani]
© Tim Brown/www.infiniteworld.org