Paka wa Mwituni
Paka wa Mwituni
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA
MNYAMA mvamizi ananyemelea windo polepole, akiwa ameinamisha kichwa chake na kukaza macho. Anakunja miguu yake na kutua. Misuli yake iliyofunikwa na manyoya ya kahawia inatetemeka. Halafu, kama mshale unaofyatuka, anamrukia mnyama mwenye wasiwasi. Paka huyo anamshika mnyama huyo kwa kucha zake na kumfinyilia chini.
Pambano hilo la kufa na kupona linatukia Australia wala si Afrika. Mvamizi huyo ni paka mdogo wa mwituni wala si simba. Inakadiriwa kwamba nchini Australia kuna paka wa mwituni milioni 12 kwenye nyika za tropiki za rasi ya kaskazini, milima yenye baridi ya kusini, na jangwa la nyanda za kati.
Paka wa Mwituni
Paka wa mwituni wanafanana na paka wa nyumbani kwa sababu walitokana na paka wa nyumbani. Manyoya yao yana rangi zinazofanana, kama vile nyeusi, nyeupe, kijivu, manjano ya machungwa; na wana mabaka yanayofanana, milia, au rangi moja mwili mzima. Hata hivyo, paka wa mwituni wana misuli mikubwa shingoni na mabegani kuliko paka wa nyumbani. Paka wa kiume wana uzito wa kati ya kilogramu 3 na 6, na wa kike kati ya kilogramu 2 na 4. Paka wa nyumbani huwategemea wanadamu, lakini paka wa mwituni hujitegemea na hawapendi kukaribiwa na wanadamu.
Mwanzoni paka walipelekwa Australia na Wazungu wa kwanza kufika huko, na katika karne ya 19, walisambazwa kotekote katika bara hilo. Paka wengi walitorokea mwituni. Wengine waliachiliwa katika miaka ya 1880 katika jitihada ya kuzuia ugonjwa uliosababishwa na sungura ambao ulikuwa ukiharibu malisho. Muda si muda, paka hao walizoea kuishi mwituni na kuongezeka kuliko wanyama wengine wote walioingizwa Australia. Leo, paka wa mwituni wanapatikana katika pembe zote za Australia, kutia ndani visiwa vyake vingi vidogo.
Wanazoea Mazingira Mapya Haraka
Paka wa mwituni huzaana sana. Paka wa kike anaweza kuzaa watoto saba wakati mmoja kabla hajafikia umri wa mwaka mmoja. Kisha huzaa mara tatu kila mwaka, na kila mara huzaa watoto wanne hadi saba. Ataendelea kuzaa maisha yake yote ambayo huwa miaka saba au minane. Iwapo atazaa watoto watatu wa kike na watatu wa kiume kila mwaka, na watoto wake wa kike wazae kama yeye, katika kipindi cha miaka saba, paka mmoja wa mwituni anaweza kutokeza maelfu ya paka.
Hata hivyo, ili waishi katika hali ngumu ya hewa ya Australia, wanahitaji kufanya mengi zaidi ya kuzaana. Mara nyingi wao huwinda kunapokuwa na baridi usiku au mapema asubuhi. Wao hujikinga na joto la mchana kwa kulala kwenye magogo yenye mashimo au kwenye mashimo ya sungura. Isitoshe, paka hao wamehimili hali ngumu sana jangwani kwa kuwa si lazima wanywe maji kwani wanaweza kupata maji wanayohitaji kutoka kwenye minofu ya mawindo yao.
Paka wa mwituni pia hula vitu vingi. Ingawa wanapenda kula sungura, Shirika la Wanyama wa Pori na Mbuga za Kitaifa la New South Wales linasema hivi: “Paka hukamata na kula zaidi ya aina 100 za ndege wa Australia, aina 50 za wanyama na kangaruu, aina 50 za wanyama wanaotambaa, na aina nyingi za vyura na wanyama wasio na uti wa mgongo.” Nao hula sana. Paka wa kiume anaweza kula chakula chenye uzani wa kati ya asilimia 5 na 8 ya uzito wake kila siku. Paka wa kike anaweza kula chakula chenye uzani wa asilimia 20 ya uzito wake wakati anaponyonyesha. Katika kisiwa kimoja kilichojitenga, paka 375 wa mwituni walikula sungura 56,000 na ndege 58,000 wa baharini kwa mwaka mmoja tu.
Wanyama wengi wa Australia hawawezi kujitoa mikononi mwa paka wa mwituni. Kulingana na gazeti la mazingira Ecos, inadhaniwa kwamba kwa sababu paka wa mwituni ni wawindaji hodari, wamezuia “jitihada za kuzalisha wanyama waliomo hatarini katika eneo kame la Australia.”
Ni Mnyama-Kipenzi au Msumbufu?
Tangu wakati wa Misri ya kale, paka wamekuwa wanyama-vipenzi. Huko Australia, asilimia 37 ya familia wana angalau paka mmoja. Paka wengi hawaondolewi uwezo wao wa kuzaa, na nyakati nyingine paka wachanga wasiotakikana hutupwa vichakani, ambako hukua, huzaa, na kuongeza idadi ya paka wa mwituni.
Ili kuzuia mnyama-kipenzi asiwe msumbufu, shirika lililotajwa hapo juu linatoa madokezo yafuatayo: Hakikisha paka wako yuko nyumbani, hasa usiku. Mlishe vizuri. Mtambulishe kwa kumvisha kola, kibandiko, au kifaa maalumu cha elektroni. Mvishe paka kengele tatu kubwa ili kuonya wanyama wengine. Ondoa uwezo wake wa kuzaa. Jenga ua wa kumzuia paka asitoke nyumbani.
Unahitaji pesa na wakati ili utumie madokezo hayo. Lakini kwa kufanya hivyo, Waaustralia wanaopenda paka watafaidika.
[Picha katika ukurasa wa 20]
Mmoja wa paka milioni 12 wa mwituni nchini Australia
[Hisani]
Joel Winter/NSW National Parks and Wildlife Service, Australia
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]
With permission of The Department of Natural Resources and Mines