Inawezekana Kuepuka Vita vya Nyuklia?
Inawezekana Kuepuka Vita vya Nyuklia?
“Wao wenyewe watajilisha na kulala wakiwa wamejinyoosha, wala hakutakuwa na mtu yeyote anayewatetemesha.”—Sefania 3:13.
KILA MTU anatamani ulimwengu usio na tisho la nyuklia. Hata hivyo, wengi hukosa tumaini wanapoona hali za ulimwengu huu. Gazeti The Guardian Weekly linasema kwamba “wazo la kudhibiti, kupunguza, na hatimaye kumaliza kabisa silaha za nyuklia limepuuzwa na Marekani na jumuiya ya kimataifa.”
Hata hivyo, wengine wanapendezwa na jitihada za mataifa kuhusiana na jambo hilo. Kwa mfano, inakadiriwa kwamba Marekani pekee ilitumia dola bilioni 2.2 kwa mwaka mmoja kuzuia vita vya nyuklia. Hizo ni pesa nyingi sana. Hata hivyo, wengi wanakasirika wanapojua kwamba taifa hilohilo hutumia dola bilioni 27 kila mwaka kujitayarisha kwa vita vya nyuklia.
Vipi kuhusu mikataba ya amani? Je, jitihada hizo zinaweza kuleta tumaini?
Mikataba ya Kudhibiti Silaha za Nyuklia
Tangu kuanzishwa kwa mabomu ya nyuklia, mikataba kadhaa imefanywa ili kudhibiti silaha za nyuklia. Mikataba hiyo ni kama vile Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia, Mashauriano ya Kudhibiti Silaha za Nyuklia, Mashauriano ya Kupunguza Silaha za Nyuklia, na Mkataba wa Kukomesha Majaribio ya Silaha. Je, mikataba hiyo imefanikiwa kumaliza tisho la nyuklia?
Mkataba wowote hutegemea uaminifu wa makundi yanayohusika. Kwa mfano, Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia uliotiwa sahihi mwaka wa 1970 ambao ulikuwa na wanachama 187 kufikia Desemba 2000, unaweza kufaulu ikiwa nchi zenye silaha za nyuklia na zisizo na silaha hizo, zilizotia sahihi mkataba huo, zitautii. Ingawa mkataba huo unakataza nchi zisizo na silaha za nyuklia kuzitengeneza au kuzinunua, unataka nchi zenye silaha za nyuklia
zimalize silaha zao. Je, mkataba huo umefanikiwa? Katika makala “Maswali Ambayo Huulizwa Mara Nyingi Kuhusu Silaha za Nyuklia,” Carey Sublette alisema kwamba “ingawa Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia una kasoro zake, umefanikiwa kuzuia kuenea kwa teknolojia ya nyuklia na silaha zinazodhibitiwa na mkataba huo.”Sublette anasema kwamba ingawa mkataba huo umefanikiwa kwa kiasi fulani, “haujafaulu . . . kushawishi mataifa kadhaa yasiunde silaha hizo, na nyakati nyingine yamefaulu kuziunda.” Hata hivyo, anasema kwamba mataifa yameweza kuunda silaha kisiri kwa kukiuka Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia. Kufanikiwa kwa mkataba wowote kunategemea uaminifu wa makundi yanayohusika. Je, tunaweza kuamini ahadi za wanadamu? Jibu ni wazi kama tunavyoona katika historia ya wanadamu.
Basi tunaweza kupata wapi tumaini?
Kufikiri kwa Njia Tofauti
Katika Desemba 2001, washindi 110 wa Tuzo ya Nobeli walikubali na kutia sahihi hati inayosema hivi: “Tumaini pekee la wakati ujao linategemea jitihada za pamoja za kimataifa zinazoongozwa na demokrasia. . . . Ili kuishi katika ulimwengu tuliobadili, ni lazima tujifunze kufikiri kwa njia tofauti.” Hata hivyo, ‘njia hiyo tofauti’ ya kufikiri ni gani? Je, kuna sababu ya kuamini kwamba wale wanaotishia amani ya ulimwengu kwa silaha zao za nyuklia watajifunza kufikiri kwa njia tofauti?
Biblia inashauri hivi: “Msiweke tegemeo lenu katika watu wenye vyeo, wala katika mtu wa udongo, ambaye hana wokovu wowote.” (Zaburi 146:3) Kwa nini? Biblia inajibu hivi: “Njia ya mtu wa udongo haimo katika uwezo wake. Mwanadamu anayetembea hana uwezo wa kuongoza hatua yake.” (Yeremia 10:23) Naam, sababu kuu ni kwamba mwanadamu hana uwezo kuitawala dunia kwa amani. Kama Biblia inavyosema, “mwanadamu amemtawala mwanadamu kwa kumuumiza.”—Mhubiri 8:9.
Ni nani anayeweza kuitawala dunia ikiwa wanadamu hawawezi? Biblia inaahidi kwamba kutakuwa na amani chini ya serikali inayotegemeka na yenye uwezo. Biblia inaita serikali hiyo Ufalme wa Mungu, na bila kujua, mamilioni ya watu wamesali kwa ajili ya serikali hiyo wanapotoa ile Sala ya Bwana: “Baba yetu uliye mbinguni, . . . ufalme wako na uje. Mapenzi yako na yatendeke duniani kama ilivyo mbinguni.” (Mathayo 6:9, 10) Mfalme wa Ufalme huo ni Yesu Kristo, ambaye ni Mkuu wa Amani. Biblia inasema hivi kuhusu utawala wake: “Hakutakuwa na mwisho kwa habari ya wingi wa huo utawala wa kifalme na kwa amani.”—Isaya 9:6, 7.
Hata kama “watu wenye vyeo,” yaani wanasiasa, na serikali haziwezi kujifunza kufikiri kwa njia tofauti, wewe unaweza. Mashahidi wa Yehova wamewasaidia mamilioni kupata ujumbe wa tumaini wa Biblia kupitia funzo la Biblia bila malipo. Ukipenda habari zaidi, tafadhali wasiliana na wachapishaji wa gazeti hili au uwatembelee kwenye Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova katika eneo lenu.
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Chini ya serikali ya Ufalme wa Mungu, hakutakuwa na tisho la vita vya nyuklia ulimwenguni