Jinsi Unavyoweza Kuishi Milimani
Jinsi Unavyoweza Kuishi Milimani
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BOLIVIA
WATU wengi huenda likizoni kwenye milima kwa sababu wanapenda utulivu na mandhari yenye kupendeza ambapo wanaweza kufurahia kutembea, kupanda milima, na kuteleza kwenye theluji. Pia, mamilioni ya watu huishi kwenye mabonde na nyanda zilizo kwenye milima iliyo juu ya mawingu. Lakini kuishi milimani kunaweza kuathiri afya, magari, na hata upishi. Matatizo hayo husababishwa na nini na yanaweza kushughulikiwaje? Je, kuna watu wengi wanaoishi milimani?
Sehemu nyingi za milimani zina maendeleo ya kiuchumi. Mamilioni ya watu wa Mexico City huishi kwenye mwinuko wa zaidi ya meta 2,000 juu ya usawa wa bahari. Denver, Colorado, nchini Marekani; Nairobi, Kenya; na Johannesburg, Afrika Kusini, ni majiji ambayo yako katika mwinuko wa zaidi ya meta 1,500. Mamilioni ya watu wa Himalaya wanaishi kwenye mwinuko wa zaidi ya meta 3,000. Katika
milima ya Andes, majiji makubwa kadhaa yako kwenye mwinuko wa meta 3,300 juu ya usawa wa bahari, na watu hufanya kazi katika migodi iliyo kwenye mwinuko wa meta 6,000. Kwa kuwa wengi wanaishi milimani, kumekuwa na uhitaji wa kufanya uchunguzi kuhusu jinsi mwili unavyozoea hali hizo. Mambo yaliyogunduliwa yanaweza kuongeza uthamini wako juu ya jinsi mwili wako ulivyoumbwa kwa njia ya ajabu.Mambo Unayopaswa Kutazamia
Watu wengi huhisi kama Doug alivyohisi alipofika kwenye milima ya Andes. Anasema: “Nilihisi kizunguzungu ghafula na karibu nizimie nilipokuwa nikibeba masanduku yetu kwenye uwanja wa ndege. Ingawa tatizo hilo lilikwisha, katika majuma mawili ya kwanza niliumwa na kichwa na sikulala vizuri. Ghafula ningeamka nikihisi kwamba ninakosa hewa. Kisha, kwa miezi kadhaa sikuwa na hamu ya chakula, nilichoka upesi, na nililala sana.” Katty anaongeza hivi: “Sikuamini mambo ambayo watu walikuwa wakisema kuhusu matatizo yanayosababishwa na kuwa milimani. Sasa ninaelewa.”
Kulingana na madaktari, Doug alikosa usingizi kwa sababu ya matatizo ya kupumua. Tatizo hilo huwapata watu wanapofika milimani. Lakini huenda ukawa na wasiwasi tatizo hilo likikupata. Mara kwa mara, unapokuwa usingizini, unaweza kushindwa kupumua kwa sekunde kadhaa. Wakati mwingine, jambo hilo linaweza kufanya uamke ghafula ukijaribu kupumua.
Watu wengine hawana tatizo hata kidogo wanapofika milimani. Watu wengine huathiriwa wanapokuwa kwenye milima yenye urefu wa meta 2,000. Karibu nusu ya watu wanaopanda milima kwa mara ya kwanza huathiriwa na mwinuko wa meta 3,000. Hata wakazi wa milimani wanaporudi baada ya juma moja au mawili tu kutoka katika maeneo ya chini, wao hupatwa na matatizo hayohayo mara nyingi. Kwa nini?
Kwa Nini Milima Huathiri Mwili Wako?
Matatizo mengi husababishwa na ukosefu wa oksijeni. Kwa sababu shinikizo la hewa angani hupungua kadiri unavyopanda, kwenye meta 2,000 juu ya usawa wa bahari oksijeni hewani hupungua kwa asilimia 20 hivi, na kwenye meta 4,000 oksijeni unayopumua hupungua kwa asilimia 40. Ukosefu wa oksijeni huathiri utendaji mwingi wa mwili. Utendaji wa misuli hupungua, mfumo wa neva hushindwa kustahimili mifadhaiko, na mfumo wa kusaga chakula hushindwa kufyonza mafuta. Kwa kawaida mwili wako unapohitaji oksijeni nyingi, unapumua zaidi. Kwa hiyo, kwa nini isiwe hivyo unapofika milimani?
Haieleweki vizuri jinsi mwili wako unavyodhibiti kiasi cha hewa unachopumua. Lakini unapopumua sana kwa sababu ya kutumia nguvu nyingi, haimaanishi kwamba jambo hilo limesababishwa na ukosefu wa oksijeni. Badala yake, inaonekana kaboni-dioksidi iliyojikusanya kwenye damu kwa sababu ya utendaji wa misuli ndiyo inayokufanya upumue zaidi. Unapokuwa milimani unapumua zaidi, lakini hilo halilipii upungufu wa oksijeni.
Ni nini kinachosababisha maumivu ya kichwa? Msemaji mmoja katika Kongamano la Kwanza la Ulimwengu Kuhusu Tiba na Magonjwa ya Milimani huko La Paz, Bolivia, alieleza kwamba dalili nyingi za ugonjwa unaosababishwa na kuwa milimani huletwa na kukusanyika kwa umajimaji ubongoni. Kwa watu wengine, hilo husababisha shinikizo kichwani. Yaelekea kwa sababu ya ukubwa wa fuvu la kichwa, watu wengine hawapatwi na matatizo hayo. Hata hivyo, mara chache hali hiyo inaweza kuhatarisha uhai. Misuli inapolegea, unaposhindwa kuona vizuri, unapopata maono, na kuchanganyikiwa, unapaswa kumwona daktari mara moja na kuondoka kwenye eneo hilo.
Tahadhari
Athari za kuwa milimani huzidi siku ya pili au ya tatu, kwa hiyo siku chache kabla na baada ya kufika ni vizuri kula vyakula vyepesi, hasa usiku. Badala ya kula vyakula vyenye mafuta mengi, unapaswa kula vyakula vyenye wanga, kama vile wali, shayiri, na viazi. Huenda ikafaa kufuata shauri hili, “Kula kiamsha-kinywa
kama mfalme, lakini chakula cha jioni kama maskini.” Pia, epuka kutumia nguvu nyingi, kwa kuwa hiyo inaweza kusababisha ugonjwa mbaya wa milimani. Kwa kuwa vijana wengi hupuuza shauri hilo, wao ndio huumia zaidi.Pia inafaa “uvae kofia, na ujipake mafuta yanayozuia miale ya jua,” kwa kuwa hakuna angahewa la kutosha kuzuia miale hatari ya jua. Miale hiyo inaweza kuwasha au hata kuharibu macho yako, kwa hiyo tumia miwani mizuri ya jua. Hewa ya mlimani hukausha machozi na kuwasha macho. Kwa hiyo, unywe maji mengi.
Madaktari wamewashauri watu wenye shinikizo la juu la damu, anemia selimundu, ugonjwa wa moyo au mapafu au wanene kupita kiasi wachunguzwe vizuri na madaktari kabla ya kuamua kutembelea sehemu za milimani. * Ikiwa una mafua makali, ugonjwa wa kupumua, au nimonia, huenda ikafaa kuahirisha safari yako kwa sababu unapokuwa milimani ukiwa na magonjwa hayo au ukifanya mazoezi mengi, yanaweza kusababisha hatari ya maji kujikusanya mapafuni. Matatizo ya kupumua yanaweza kufanya hata watu ambao wameishi mlimani kwa miaka mingi kukosa oksijeni na hivyo kupata magonjwa hatari. Kwa upande mwingine, mara nyingi watu wanaougua pumu hufurahia kuishi milimani. Kikundi kimoja cha madaktari Warusi kililiambia Kongamano la Kwanza la Ulimwengu Kuhusu Tiba na Magonjwa ya Milimani kwamba wao huwapeleka milimani wagonjwa wenye matatizo fulani kama sehemu ya matibabu.
Kuishi Milimani
Hakuna haja ya kuogopa kuishi milimani. Kwa kweli, sehemu fulani za milimani, kama vile Milima ya Caucasus, inajulikana kwa kuwa na watu ambao wameishi miaka mingi isivyo kawaida. Wengine wamevumilia kuishi milimani kwa miaka mingi. Msomaji mmoja wa Amkeni! huko Andes anasema hivi: “Niliishi na kufanya kazi kwa miaka 13 kwenye migodi iliyo katika mlima wa meta 6,000 karibu na kilele cha volkano. Haikuwa rahisi kuvunjavunja mawe ya salfa kwa nyundo. Hata hivyo, kila jioni tulicheza mpira wa miguu!” Mwili wa mwanadamu una uwezo wa ajabu wa kubadilika kupatana na hali, jambo ambalo linaonyesha hekima ya hali ya juu ya Muumba. Mwili wako unakabilianaje na ukosefu wa oksijeni milimani?
Unapokuwa milimani, moyo na mapafu yako huanza kufanya kazi haraka. Kisha umajimaji ulio kwenye damu hupungua, hivyo kukusanya chembe nyekundu za damu zinazobeba oksijeni. Muda si muda, damu nyingi
hupelekwa ubongoni inakohitajika zaidi. Baada ya saa chache tu, uloto huanza kutengeneza chembe nyekundu za damu ambazo zinaweza kufanya mwili uhitaji oksijeni nyingi zaidi. Hiyo inamaanisha kwamba ingawa inachukua miezi kadhaa ili mwili wako uzoee hali za milimani, baada ya siku chache mpigo wako wa moyo na kupumua hurudia hali ya kawaida.Matatizo ya Magari na Upishi
Si mwili wako tu unaokosa oksijeni. Gari lako linaweza kulegea pia. Ijapokuwa fundi anaweza kurekebisha mfumo wa kuchanganya mafuta na hewa, injini yako haitakuwa na nguvu kama kawaida. Vipi jikoni?
Baadhi ya matatizo yanayoweza kumhuzunisha mpishi ni keki isiyofura, mkate usioshikana, na maharagwe na mayai yasiyoiva. Kwa nini jambo hilo hutokea, na unaweza kufanya nini?
Matatizo ya upishi hutokea mara nyingi zaidi unapooka mikate na keki. Kiasi kidogo cha hewa milimani hufanya gesi zinazolainisha unga uliokandwa kupanuka zaidi kuliko kwenye usawa wa bahari. Mapovu madogo kwenye unga uliokandwa hufanya mkate au keki kuachana au hata vibaya zaidi mapovu hayo yanaweza kupasuka na kufanya keki isifure. Lakini ni rahisi kusuluhisha tatizo hilo. Ikiwa utatumia mayai kuoka keki, usiyakoroge kupita kiasi. Tumia chachu kidogo iwapo inahitajika. Kitabu The New High Altitude Cookbook kinapendekeza kwamba watu walio kwenye mwinuko wa meta 600 wapunguze chachu kwa asilimia 25, na wale wanaoishi kwenye mwinuko wa meta 2,000 wapunguze kwa asilimia 75.
Unapooka mikate ya hamira, hakikisha kwamba unga uliokandwa haufuri sana na kuwa mara mbili ya ulivyokuwa. Tumia mayai makubwa ili keki isivunjike-vunjike kwani mayai hufanya unga ushikane. Kwa upande mwingine, kwa kuwa sukari nyingi sana hudhoofisha keki, tumia kidogo tu kwani kiasi kidogo cha hewa hufanya sukari ijikusanye kwenye mchanganyiko kwa kufyonza maji haraka. Ama kweli, mapishi mengi huhitaji maji mengi kwa kuwa hewa kavu ya milimani hufyonza maji kwenye chakula.
Karibu vyakula vyote huchukua muda mrefu kuiva. Kwa mfano, kuchemsha yai huchukua dakika moja zaidi kwenye mwinuko wa meta 1,500 na dakika tatu zaidi kwenye mwinuko wa meta 3,000. Sufuria inayotumia mvuke inafaa zaidi. Kwa hakika, unahitaji sufuria hiyo kupika maharagwe na njegere ukiwa milimani.
Kwa hiyo, usiogope kutembelea milimani. Huenda ukahemahema kwa muda fulani, keki yako ikawa kama chapati, na gari unaloendesha kwenda polepole kama kobe, lakini ikiwa una afya njema, huenda utafurahia matembezi yako.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 16 Madaktari fulani hupendekeza dawa ya acetazolamide ili kuwasaidia kupumua wanapokuwa milimani. Dawa nyingine za ugonjwa wa milimani hutangazwa, lakini madaktari fulani hawazipendekezi.
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 12, 13]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Baadhi ya Milima na Majiji ya Ulimwengu Yaliyo Kwenye Mwinuko
—9,000 meters
Mount Everest, Nepal na China 8,850 meta
—7,500 meters
—6,000 meters
Mount Kilimanjaro, Tanzania
5,895 meta
Aucanquilcha, Chile
5,346 meta
Mont Blanc, France
4,807 meta
—4,500 meters
Potosí, Bolivia
4,180 meta
Puno, Peru
3,826 meta
Mount Fuji, Japan
3,776 meta
La Paz, Bolivia
3,625 meta
—3,000 meters
Trongsa Dzong, Bhutan
2,398 meta
Mexico City, Mexico
2,239 meta
Mount Washington,
New Hampshire, United States
1,917 meta
Nairobi, Kenya
1,675 meta
Denver, Colorado, United States
1,609 meta
—1,500 meters
—Usawa wa bahari—
[Picha katika ukurasa wa 10]
La Paz, Bolivia 3,625 m
[Picha katika ukurasa wa 10]
Johannesburg, South Africa 1,750 m