Tamasha Kubwa Zaidi ya Maputo Ulimwenguni!
Tamasha Kubwa Zaidi ya Maputo Ulimwenguni!
KWA siku tisa kila Oktoba, eneo la Albuquerque, New Mexico, Marekani, huwa na msongamano mkubwa wa magari. Madereva hupunguza mwendo au kusimama ili waone maputo mengi yenye rangi mbalimbali yakipaa kwenye anga jangavu katika majira ya kupukutika kwa majani. Ni maonyesho ya kila mwaka ya Tamasha ya Kimataifa ya Maputo ya Kodak Albuquerque ambapo zaidi ya wageni 800,000 huja kuyatazama.
Inaeleweka ni kwa nini magari huenda polepole. Hebu wazia maonyesho hayo yanavyokuwa! Mamia ya maputo—yenye urefu wa meta 15 hadi 25—yakipaa pamoja katika upepo wa asubuhi, halafu yanaelea hewani juu ya Mto Rio Grande na jiji la Albuquerque. Kule nyuma, tunaona Milima ya Sandia yenye urefu wa meta 3,000 ambayo inafanya mandhari hiyo ipendeze zaidi.
Maonyesho hayo yamepanuka sana tangu yalipoanzishwa kwenye maegesho ya magari mnamo mwaka wa 1972 yakiwa na maputo 13 tu. Kufikia mwaka wa 1978, kulikuwa
na timu 273 za kurusha maputo, na ilikuwa tamasha kubwa zaidi ya maputo ulimwenguni. Katika mwaka wa 2003, maputo zaidi ya 720 yalitumiwa. Kulikuwa na timu za maputo kutoka majimbo mengi ya Marekani na nchi nyingine 20. Waandishi wa habari kutoka mashirika mengi na wapiga-picha wengi walifanya maonyesho hayo kuwa “tamasha inayopigwa picha zaidi ulimwenguni.” Katika mwaka wa 2000, wakati wa sherehe za milenia mpya, zaidi ya maputo 1,000 yalitumiwa—karibu asilimia 20 ya maputo yote yanayojulikana ulimwenguni.Jinsi Maputo Hayo Yanavyofanya Kazi
Maputo mengi kwenye tamasha hiyo huinuliwa kwa hewa iliyopashwa joto na majiko ya gesi ya propani kwenye mdomo wa maputo. Maputo yametengenezwa kwa kitambaa kilichopakwa kemikali fulani inayoyafanya yasivuje gesi. Kikapu kinachombeba rubani na abiria kimeunganishwa na puto. Puto huingizwa hewa katika hatua mbili. Kwanza, feni kubwa hupuliza hewa baridi ndani ya puto likiwa limetandazwa chini. Halafu jiko la propani hupuliza hewa yenye joto ndani ya puto hilo. Hewa hiyo yenye joto huinua puto, lakini huwa limefungiliwa chini hadi rubani anapokuwa tayari kung’oa nanga. Mara tu puto linapokuwa angani, rubani anaweza kulifanya lipae kwa kuongeza hewa yenye joto. Anapotaka kushuka, anaacha hewa ipoe au kufungua mwanya juu ya puto ili hewa yenye joto itoke.
Kwenye tamasha hiyo, maputo yenye hewa yenye joto huwa na propani ya kutosha kuyawezesha kubaki hewani kwa saa chache, kwa kawaida kwenye urefu usiozidi meta 600. Hivyo marubani na watu wanaofuatilia mwendo wa maputo hayo wakiwa chini lazima watafute mahali salama pa kutua. Wao hutafuta sehemu iliyo wazi, isiyo na nyaya za stima na sehemu iliyo mbali na barabara zenye shughuli nyingi.
Maputo mengine katika tamasha hiyo huwekwa gesi ya heli au hidrojeni. Maputo hayo yanaweza kukaa hewani kwa muda wa siku kadhaa tofauti na maputo ya hewa yenye joto. Marubani wanaotumia maputo yenye gesi hushindana ili waone ni nani atakayepaa juu zaidi, wakisafiri urefu wa meta 3,000 hadi 4,500 angani.
Maputo hayawezi kuelekezwa. Badala yake yanafuata upepo. Hata hivyo, rubani stadi anaweza kudhibiti puto kwa kwenda juu na chini ili puto lipate hewa ya kulielekeza upande unaofaa. Kwa sababu hiyo, eneo la Albuquerque linafaa urushaji wa maputo. Eneo hilo lina pepo zinazopita chini ambazo husukuma maputo na pepo zinazopita juu ambazo huyarudisha chini.
Tukio Lenye Kusisimua
Zaidi ya watu 2,000 hujitolea ili kufanikisha tamasha hiyo na kuhakikisha kuna usalama. Msimamizi wa tamasha hiyo huwa na daraka la kuelekeza mamia ya maputo. Ni kama kuelekeza ndege katika uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi. Hebu wazia jinsi inavyokuwa! Mchanganyiko wa rangi mbalimbali na maumbo mengi huwasisimua sana watu wazima kwa watoto. Tazama! Puto moja linafanana na chura, lingine kama dubu, na lingine kama sungura! Pia kuna maputo yanayofanana na mtoto wa dinosa, ng’ombe mkubwa anayeelea hewani, nguruwe wawili wanaoruka, samaki anayeitwa Sushi, mwanasesere, mkebe mkubwa wa soda, kiatu cha mpanda-farasi, kichala cha pilipili-hoho, na mengine mengi sana.
Kwa kuwa kuna maputo ya rangi na maumbo mbalimbali katika anga jangavu la buluu, mpiga-picha anaweza kupiga picha mpaka achoke! Kunakuwa na umaridadi wa pekee wakati wa jioni—giza linapoanza kuingia, mamia ya maputo huelea angani, kila moja likiwa na jiko linalowaka kama mshumaa katika taa ya karatasi.
Huenda wengi wetu wasiweze kujionea tamasha hiyo ya maputo au kupata fursa ya pekee ya kusafiri ndani ya puto. Lakini unapofikiria mandhari hiyo, akili yako inaweza kuwazia jinsi maputo hayo yanavyoelea katika anga la Albuquerque wakati wa majira ya kupukutika.
[Picha katika ukurasa wa 18]
1. Watu wanne hadi nane hufuatilia mwendo wa puto wakiwa chini
2. Jiko la propani linaingiza hewa yenye joto katika puto ili lipae
3. Usiku, maputo hutoa mng’ao wenye rangi
4. Maumbo mbalimbali ya maputo
[Hisani]
Photos 1 and 2: Raymond Watt/Albuquerque International Balloon Fiesta