Je, Unamjua Kiruka Njia?
Je, Unamjua Kiruka Njia?
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FINLAND
KINDI hupatikana karibu sehemu zote za dunia. Hata hivyo, ni wachache walio kama kindi wa Siberia ambaye huruka, na kwa kawaida huitwa kirukanjia. * Je, kweli mnyama huyo mdogo huruka? Kirukanjia ni kiumbe wa aina gani, na kwa nini ni vigumu sana kumwona?
Wao Hurukaje?
Ingawa kindi wote wanaoishi kwenye miti huruka kutoka mti mmoja hadi mwingine, hakuna anayeweza kumshinda kirukanjia. Wanyama hao wadogo wanaweza kuruka umbali wa meta 80! Lakini yeye hufanyaje hivyo?
Kirukanjia ana utando unaomsaidia kuruka ambao unaweza kumshangaza injinia yeyote wa ndege. Kitabu The World of the Animals kinasema hivi: “Sehemu ya mbele ya utando huo hutegemezwa na tishu zinazoanzia kwenye mkono wake. Ingawa utando huo huonekana kana kwamba una tabaka mbili tu za ngozi, kuna tabaka moja nyembamba ya misuli ambayo huwawezesha virukanjia hao wajipinde ili waweze kuruka.”
Kirukanjia anaponyiririka hewani, yeye huonekana kuwa bapa kabisa. Anapokuwa ametua, yeye huonekana kama amevaa koti kubwa sana la manyoya la rangi ya kijivu.
Kirukanjia anawezaje kuruka bila kugonga chochote? Mkia wake hutumika kama usukani, na kumwongoza anaporuka. Kabla ya kutua kwenye mti, kirukanjia hufungua parachuti yake ya mfano kwa kugeuka na kusimama wima. Ni mara chache sana kirukanjia hukosea na kuanguka.
Jambo jingine ambalo humsaidia kirukanjia ni kwamba yeye ni mwepesi. Kirukanjia aliyekomaa ana uzito wa gramu 150 hivi naye ana urefu wa sentimeta 20 hivi bila kutia ndani mkia wake. Ana masikio madogo ambayo hayana manyoya, kwa hiyo hayamzuii kuruka.
Anaweza Kuruka Usiku
Kirukanjia ana macho ya pekee yanayofanana na vito vikubwa vyeusi. Tofauti na kindi wengine, kirukanjia huruka usiku. Hivyo, anahitaji kuona vizuri ili kupata chakula anachopenda, yaani, aina fulani ya ua linaloitwa catkin na majani ya miti inayopukutika na machipukizi ya misonobari. Kwa kuwa wakati wa baridi kali chakula hupungua, kirukanjia hukusanya maua ya catkin na kuyahifadhi katika matawi na mashimo yaliyo katika miti wakati wa majira ya kupukutika kwa majani.
Virukanjia wengine husahau kulala alasiri kwa sababu ya kucheza sana wakati wa majira ya kuchipua. Isitoshe, majira hayo huwa wakati ambapo virukanjia hujamiiana. Kirukanjia wa kike anapovutiwa na sarakasi za kirukanjia wa kiume, yeye huanza kujenga kiota. Kiota kinaweza kuwa cha ndege au tundu katika mti. Kwa kawaida, virukanjia huwa na viota vingi. Vingine hutumiwa kama mahali pa kuhifadhia chakula navyo vingine hutumika kama vyumba
vya ziada. Virukanjia fulani hata hujenga viota katika banda. Hata hivyo, tofauti na kindi wengine, virukanjia hawapatikani jijini!Mwishoni mwa majira ya kuchipua au mapema wakati wa kiangazi, kirukanjia wa kike huzaa watoto wawili au watatu. Yeye hutumia muda wake mwingi kuwalisha, hata wakati wa mchana. Watoto hao wanapozaliwa wanatoshana na ncha ya kidole chako; lakini kabla majira ya kupukutika kwa majani kwisha, watakuwa wamenyiririka kutoka kwenye kiota!
Kwa Nini Hawaonekani kwa Urahisi?
Kwa nini virukanjia hawaonekani kwa urahisi? Sababu moja ni kwamba viumbe hao wadogo ambao huruka usiku husonga polepole kwenye matawi ya miti yaliyoshikana nao hawaonekani kwa urahisi. Isitoshe, virukanjia hupendelea kuishi kwenye misitu yenye miti mbalimbali inayopatikana eno la Bahari ya Baltiki kupitia msitu wa Urusi hadi Bahari ya Pasifiki.
Misitu mikubwa ya Siberia inatuhakikishia kwamba virukanjia wataendelea kuwepo. Hata hivyo, wanyama hao, sawa na wanyama wengine wanaojenga nyumba zao katika mashimo ya miti wamepoteza makao yao kwa sababu ya ukataji wa miti. Huko Finland, virukanjia wanaoishi sehemu ya magharibi wanalindwa na sheria iliyowekwa na Muungano wa Ulaya. Kuonekana tu kwa kirukanjia juu ya matawi ya mti au kuonekana kwa kinyesi chake kunaweza kufanya ujenzi wa jengo fulani uahirishwe au ukomeshwe kabisa.
Bila shaka, virukanjia huendelea na shughuli zao kwa furaha bila kujua hasara ambayo vinyesi vyao vinaweza kutokeza. Kwa kweli, hakuna kitu chochote ambacho hukatiza shughuli zao za kawaida. Giza linapoingia katika misitu iliyo kaskazini, maelfu ya vikuranjia hutoka kwenye matundu yaliyoko kwenye miti. Mikia mirefu yenye manyoya inatikisika, matawi machanga yanayumba-yumba, nao virukanjia wanaanza shughuli zao tena!
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Kindi huyo ni mmoja kati ya zaidi ya aina 30 za kindi wanaoruka. Wengi wao kutia ndani kindi wanaoruka ambao wanatoshana na paka huishi katika misitu ya Kusini-Mashariki mwa Asia. Kwa kawaida, kindi wanaoishi Afrika hawaorodheshwi kati ya virukanjia ingawa wanafanana sana. Sehemu pekee inayowatambulisha ni mkia wao ambao una manyoya kwenye ncha tu na sehemu ya chini.
[Picha katika ukurasa wa 23]
“Catkin,” chakula kinachopendwa na virukanjia
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kitoto cha kirukanjia wa Siberia
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]
Ilya Lyubechanskii/BCIUSA.COM
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Squirrels: Benjam Pöntinen
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Squirrels: Benjam Pöntinen