Tapioca—Chakula Kitamu cha Wabrazili
Tapioca—Chakula Kitamu cha Wabrazili
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Brazili
NCHINI Brazili, neno tapioca linaweza kurejelea vyakula vinavyopikwa kwa mhogo. Mojawapo ya vyakula hivyo ni mkate wa kawaida. Mikate hiyo inafanana na chapati nyembamba za maji na mara nyingi huitwa chapati za tapioca. Inapikwa kwa unga laini unaoitwa polvilho doce au goma, ambao hutokana na mihogo.
Baada ya kukunwa na kusagwa mihogo hutoa umajimaji mweupe unaofanana na maziwa. Umajimaji huo huachwa ili machicha yatulie. Kisha umajimaji huo humwagwa, nayo machicha, ambayo ni wanga mzito hukaushwa juani.
Tapioca kilikuwa chakula kikuu cha wenyeji wa Brazili. Baadaye, masetla Wareno waliona kwamba wanaweza kutumia tapioca badala ya mkate. Hata hivyo, miaka michache iliyopita wapishi wabunifu Wabrazili walivutiwa na tapioca nao wakaanza kuitumia kwenye mikahawa yao na ikaanza kupendwa.
Ili kuwapendeza watu wenye mapendezi mbalimbali, wapishi hao walianza kupika chapati nyembamba za maji za aina mbalimbali, na kutumia ustadi wao wa pekee kufanya chapati hizo zipendeze zaidi. Leo chapati nyembamba za maji za tapioca zinapendwa sana, na zimefanya mapishi ya Brazili yavutie. Mikahawa mingi imekuwa mashuhuri kwa sababu ya kupika chapati nyembamba za maji.
Mbona usijaribu kupika chapati hizo? Familia na rafiki zako watapendezwa na ladha yake nzuri.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]
Kupika Chapati Nyembamba za Maji za “Tapioca”
Kupika chapati nane:
Vikombe 3 vya polvilho doce, maji kikombe 11⁄2, na chumvi kidogo
Maagizo: Ukitumia bakuli lenye ukubwa wa kadiri, nyunyiza maji na chumvi kwenye polvilho doce, kisha uchanganye kwa vidole. Ongeza maji kidogo-kidogo huku ukikanda mchanganyiko huo kwa vidole hadi uwe kama vidonge vyenye chengachenga ambavyo unaweza kuvitengeneza katika umbo la mpira bila kunata kwenye vidole. Kisha pitisha mchanganyiko huo kwenye kichungi. Sasa uko tayari kupika chapati nyembamba.
Pasha moto kikaango kisichonata chenye unene wa sentimeta 20 kwa moto wa kadiri. Mwaga sehemu moja ya nane ya mchanganyiko huo kwenye kikaango, na kuutawanya kwa kutumia upande wa nyuma wa kijiko. Upike kwa dakika mbili hadi nne, au hadi mchanganyiko huo ushikane na kufanyiza keki iliyo bapa, isiyonata kwenye kikaango. Geuza upande wa pili kwa kijiko cha plastiki na kuupika kwa dakika moja. Fanya hivyo na mchanganyiko uliobaki. Weka chapati zilizoiva pamoja.
Chapati hizo nyembamba za tapioca zinaweza kuandaliwa kwa njia tofauti kwa kuzitia vitu mbalimbali. Ukitaka kuziandaa kwa ajili ya kifungua-kinywa, zipake siagi zikiwa bado moto, kisha ongeza vijiko viwili vikubwa vya nazi iliyosagwa. Au unaweza kumwaga maziwa mazito yenye sukari juu ya chapati hizo, uongeze nazi, uzikunje na kuziandaa.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mihogo
[Picha katika ukurasa wa 24]
Tapioca yenye nazi na maziwa mazito yenye sukari