Kwa Nini Ushirikiano Ni Muhimu?
Kwa Nini Ushirikiano Ni Muhimu?
“Hakuna kiumbe anayejitegemea. Kila kiumbe ana uhusiano na viumbe wengine kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.”—“Symbiosis—An Introduction to Biological Associations.”
“MFUMO wa viumbe.” Huo ni ufafanuzi unaofaa kwelikweli, kwani uhai umefanyizwa kwa mtandao wa viumbe wanaoshirikiana na kutegemeana! Wanadamu ni sehemu ya mfumo huo. Ili kuthibitisha hilo, unahitaji tu kutazama mwili wako. Bakteria nyingi zisizoweza kuonekana hufanya kazi ndani ya mfumo wako wa umeng’enyaji na kukusaidia uwe na afya nzuri kwa kuharibu viumbe wanaoweza kukudhuru na kukusaidia kumeng’enya chakula na kutokeza vitamini muhimu. Kwa upande mwingine, wewe huandalia bakteria hizo chakula na mazingira yanayofaa.
Kuna ushirikiano kama huo kati ya wanyama, hasa wale wanaocheua kama vile ng’ombe, mbawala, na kondoo. Sehemu ya kwanza ya tumbo lao lililogawanywa katika sehemu nyingi, ina mfumo halisi wa ikolojia wa bakteria, kuvu, na protozoa. Kupitia uchachushaji, viumbe hao wadogo huvunja-vunja selulosi, ambayo ni wanga wenye nyuzinyuzi ulio katika mimea, na kutokeza virutubisho mbalimbali. Hata wadudu fulani ambao hula selulosi, kama vile jamii za mbawakawa, mende, samaki-sanduku, mchwa, na nyigu, hutumia bakteria ili kumeng’enya chakula.
Inapendeza kuona ushirikiano wa karibu kama huo kati ya viumbe wasiofanana lakini wanaoishi pamoja. * “Mapatano kama hayo ni muhimu kwa ukuzi wa kila kiumbe,” anasema Tom Wakeford katika kitabu chake Liaisons of Life. Ebu fikiria kidogo kuhusu udongo kwani viumbe wengi walio duniani hutoka kwenye udongo.
Udongo Ni Kama Kiumbe Hai!
Biblia inasema kwamba udongo una nguvu. (Mwanzo 4:12) Maneno hayo ni ya kweli, kwa kuwa kuna uhai mwingi ndani ya udongo wenye rutuba. Udongo ni mazingira yanayofaa kwa ukuzi kwani una viumbe wengi wadogo. Huenda kilogramu moja tu ya udongo ikawa na bakteria zaidi ya bilioni 500, kuvu bilioni moja, na viumbe milioni 500 hivi wenye chembe nyingi kama vile wadudu na minyoo. Viumbe hao wadogo hushirikiana kuvunja-vunja vitu vinavyotokana na viumbe hai, kama vile majani makavu na kinyesi cha wanyama huku wakitokeza nitrojeni ambayo wao huibadili ili iweze kufyonzwa na mimea. Pia wao hubadili kaboni kuwa kaboni dioksidi na vitu vingine ambavyo mimea huhitaji ili kutengeneza chakula.
Mikundekunde, kama vile alfalfa, klova, njegere, na soya, ina uhusiano wa pekee na bakteria kwa kuwa huziruhusu “zivamie” mizizi yao. Lakini badala ya kuharibu mimea hiyo, bakteria huchochea mizizi itokeze vifundo vidogo. Bakteria hukaa na kukua hapo hadi ziwe na ukubwa wa zaidi ya mara 40 ya ukubwa wao wa kawaida. Kazi yao ni kubadili nitrojeni kuwa vitu ambavyo mikundekunde inaweza kutumia. Nazo bakteria hupata chakula kutoka kwa mimea hiyo.
Pia kuvu hutimiza sehemu muhimu katika ukuzi wa mimea. Kwa kweli, karibu kila mti, kichaka, na nyasi hushirikiana kwa siri, chini ya ardhi na kuvu. Viumbe hao pia “huvamia” mizizi, ambapo wao hufyonza maji na madini muhimu, kama vile chuma, fosforasi, potasiamu, na zinki. Na kwa kuwa kuvu haziwezi kujitengenezea chakula kwa sababu hazina chanikiwiti, hizo hufyonza wanga kutoka kwenye mmea.
Mmea mmoja unaotegemea sana kuvu ni okidi. Upatano wao huanza na mbegu za okidi zilizo kama vumbi ambazo huhitaji msaada ili kuota. Pia kuvu husaidia mmea huo unapokomaa kwa kuimarisha mizizi yake midogo. Wakeford anasema kwamba kuvu “hufanyiza mfumo mkubwa wenye nguvu wa kukusanya chakula ambao hutimiza mahitaji ya okidi kikamili. Kwa upande mwingine, huenda [kuvu] wakapata vitamini na kiasi kidogo cha nitrojeni kutoka kwenye mmea huo. Hata hivyo, ukarimu wa okidi una mipaka. Mmea huo hudhibiti kuvu kwa kutumia dawa za asili za kuua kuvu, endapo kuvu watajaribu kupanda kutoka kwenye makao yao ya kawaida ndani ya mizizi ili kukua kwenye shina la okidi.”
Mimea inayotokeza maua haishirikiani tu ndani ya udongo; hiyo pia hupatana kwa njia inayoweza kuonekana.
Ushirikiano Husaidia Katika Uzalishaji
Nyuki anapotua juu ya ua, yeye huanza kushirikiana na ua hilo. Nyuki huyo hupata nekta na chavua na wakati huohuo ua hupata chavua kutoka kwenye maua mengine ya aina hiyo. Upatano huo huwezesha ua kuzaa. Baada ya kuchavushwa, maua huacha kutengeneza chakula. Wadudu hujuaje kwamba wakati wa kula umekwisha? Maua “huwajulisha” kwa njia mbalimbali. Huenda yakapoteza harufu, yakaangusha petali, au yakakua kuelekea upande tofauti au kubadili rangi, labda kuwa na rangi hafifu. Huenda jambo hilo likatusikitisha, lakini kufanya hivyo huwasaidia sana nyuki wanaofanya kazi kwa bidii kwani sasa wanaweza kuelekeza jitihada zao kwenye mimea ambayo bado haijanyauka.
Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya wachavushaji, hasa nyuki, imepungua sana katika maeneo fulani. Hali hiyo inatia wasiwasi kwani karibu asilimia 70 ya maua hutegemea wadudu kwa ajili ya uchavushaji. Isitoshe, asilimia 30 ya
vyakula tunavyotumia hutokana na mazao yaliyochavushwa na nyuki.Chungu Shambani
Kuna chungu fulani ambao pia hushirikiana na mimea. Ili kupata makao na chakula, huenda wadudu hao wakachavusha mmea, wakatawanya mbegu zake, wakaandaa virutubisho, au kuulinda dhidi ya wanyama au wadudu wanaokula mimea. Aina fulani ya chungu hujenga makao yao ndani ya miiba ya mti wa mgunga na wanapozunguka mti huo wao huharibu miche inayoweza kuudhuru. Mgunga hushukuru kwa kuwapa chungu nekta tamu.
Kwa upande mwingine, chungu fulani hupendelea kufuga wadudu. Wadudu hao huwatolea chungu umajimaji mtamu wanapoguswa kwa wororo na vipapasio vyao. Kitabu Symbiosis kinasema hivi kuhusu wadudu hao: “Chungu huwachunga wadudu hawa kama ng’ombe, wakiwakamua kwa ajili ya chakula na kuwalinda dhidi ya wavamizi.” Kama vile mfugaji huweka ng’ombe wake zizini usiku, mara nyingi chungu huwabeba wadudu hao hadi kwenye makao yao salama jioni na kuwarudisha “malishoni” asubuhi, hasa kwenye majani machanga yenye
lishe. Na hatuzungumzi kuhusu wadudu wachache tu. Chungu wanaweza kuwa na “makundi” yenye maelfu ya wadudu katika nyumba moja!Wakiwa bado viwavi, jamii fulani ya vipepeo hutunzwa pia na chungu. Kwa mfano, kipepeo mwenye rangi ya samawati hushirikiana na chungu wanaoitwa koyokoyo. Kwa kweli, kipepeo huyo hawezi kukua na kukomaa kabisa bila msaada wao. Anapokuwa kiwavi, yeye hutoa umajimaji wenye sukari ambao hunywewa na chungu. Baadaye, kipepeo anapoibuka kutoka kwenye kifuko chake, yeye huacha makao ya chungu akiwa salama.
Kuishi na Wanyama Hatari
Kama ungekuwa ndege, je, ungeleta nyoka kwenye kiota chako? Huenda ukasema, “siwezi kamwe!” Hata hivyo, aina fulani ya bundi hufanya hivyo. Nyoka huyo ni wa jamii fulani ya birisi. Badala ya kudhuru makinda wa ndege hao, nyoka huyo hula chungu, nzi, na wadudu wengine pamoja na viluwiluwi vyao. Ripoti moja katika gazeti New Scientist ilisema kwamba vifaranga waliolelewa na nyoka huyo “hukua haraka zaidi na wana uwezekano mkubwa wa kuendelea kuwa hai” kuliko wale ambao hawakulelewa na nyoka huyo ambaye husafisha kiota.
Ndege anayeitwa water dikkop hashirikiani na nyoka; yeye hujenga kiota chake karibu na kile cha mamba wa Nile, mnyama ambaye hula ndege fulani! Hata hivyo, badala ya kuliwa, ndege huyo huwa mlinzi wa mamba. Hatari ikitokea karibu na kiota chake au cha mamba, ndege huyo atatoa sauti ya kuonya. Ikiwa mamba hayuko, vilio hivyo vitamfanya arejee nyumbani kwa kishindo.
Kuondolewa Wadudu na Kusafishwa
Je, umewahi kuwaona ndege kama vile mchungi au wala-kupe wakiwa mgongoni mwa paa, ng’ombe, twiga, au ng’ombe-dume wakidonoa-donoa ngozi yao? Badala ya kuwasumbua, ndege hao huwasaidia wanyama hao kwa kula viroboto,
kupe, na wadudu wengine ambao wanyama hao hawawezi kuwaondoa. Wao pia hula ngozi zilizooza na mabuu. Wala-kupe pia hutoa sauti na kuwaonya wanyama hao kunapokuwa na hatari.Kwa kuwa viboko hukaa majini kwa muda mrefu, wao husafishwa na “rafiki” zao wenye manyoya na mapezi. Kiboko anapokuwa majini, samaki anayeitwa black labeo, ambaye ni jamii ya kambare, husafisha mwani, ngozi iliyokufa, wadudu, au kitu chochote kinachokwama juu ya mnyama huyo. Hata wao husafisha meno na fizi za viboko! Jamii nyingine za samaki pia husaidia kwa kusafisha vidonda na nyingine hutumia pua zao ndefu kupenya na kula katikati ya vidole vya miguu vya kiboko na sehemu nyingine zisizofikika kwa urahisi.
Bila shaka, samaki ni mwenye kuvutia, hivyo anahitaji kuondolewa uchafu unaokwama juu yake, kama vile wanyama wenye magamba na bakteria, kuvu, na viroboto, na vilevile tishu zilizoharibika au zenye ugonjwa. Ili kusafishwa, kwa kawaida samaki wa baharini huenda mahali pa kusafishiwa. Wanapofika huko, goby wenye rangi nyangavu, laburida, na uduvi huwasafisha samaki hao vizuri kabisa, na palepale wanapata chakula. Huenda samaki wakubwa wakasafishwa na kikundi kikubwa cha viumbe hao!
Samaki anayetaka kusafishwa anaweza kuonyesha hivyo kwa njia nyingi. Kwa mfano, wengine husimama kwa njia isiyo ya kawaida wakiweka kichwa chini na mkia juu. Au huenda wakafungua kinywa na mashavu yao, kana kwamba wanasema: “Ingieni tu. Sitawauma.” Viumbe hao wanaosafisha hukubali bila wasiwasi, hata ikiwa mteja wao ni hatari, kama vile kungamorei au papa. Wanaposafishwa, wateja fulani hubadili rangi, labda ili kufanya wadudu waonekane kwa urahisi zaidi. Katika maji yasiyo na samaki ambao huwasafisha wengine, samaki wa baharini “huathiriwa na wadudu haraka na kuwa wagonjwa,” kinasema kitabu Animal Partnerships. “Lakini mara tu samaki ambaye husafisha anapoingizwa katika maji hayo, yeye huanza kufanya kazi ya kuwasafisha na ni kana kwamba wao hujua ni nini kinachoendelea kwani wao hupanga foleni mara moja ili wasafishwe.”
Kadiri tunavyojifunza ndivyo tunavyochochewa na kicho kuhusu upatano na kutegemeana kwa viumbe. Kama wanamuziki katika okestra, kila kiumbe hutimiza sehemu yake ili kuchangia upatano uliopo katika uhai, kutia ndani uhai wa mwanadamu, na kufanya uwezekane na ufurahishe. Bila shaka, huo ni uthibitisho wa kwamba kuna Mbuni Mkuu mwenye akili nyingi!—Mwanzo 1:31; Ufunuo 4:11.
Chanzo Pekee cha Ukosefu wa Upatano
Inasikitisha sana kwamba mara nyingi wanadamu ndio hawashirikiani na viumbe wengine. Tofauti na wanyama ambao huongozwa hasa na silika, wanadamu huathiriwa na mambo mbalimbali, kama vile upendo na sifa nyingine nzuri, na vilevile chuki na pupa yenye ubinafsi.
Kwa kuwa inaonekana kwamba wanadamu huongozwa hasa na pupa yenye ubinafsi, wengi wana wasiwasi kuhusu wakati ujao wa dunia yetu. (2 Timotheo 3:1-5) Lakini wanakosa kumfikiria Muumba. Kutimizwa kwa kusudi la Mungu kwa dunia kutarudisha upatano unaofaa kati ya viumbe na vilevile ushirikiano usio na kifani kati ya viumbe wote, kutia ndani wanadamu.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Viumbe hushirikiana katika njia tatu: njia ya kwanza viumbe wote wawili hunufaika; njia ya pili kiumbe mmoja hunufaika bila kumdhuru kiumbe yule mwingine; na njia ya tatu kiumbe mmoja hunufaika na kumdhuru yule mwingine. Makala hii itazungumzia mifano kuhusu ushirikiano ambao viumbe wote wawili hunufaika.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Viumbe Wawili Katika Mmoja
Yale madoa makavu ya rangi ya kijivu au ya kijani ambayo wewe huyaona mara nyingi kwenye miamba au katika miti huenda yakawa ni kuvumwani. Vitabu fulani husema kwamba huenda kuna aina 20,000 hivi za kuvumwani! Huenda kuvumwani wakaonekana kuwa kiumbe kimoja, lakini kwa kweli ni muungano wa kuvu na mwani.
Kwa nini viumbe hao wawili huungana? Kuvu haiwezi kujitengenezea chakula. Kwa hiyo kwa kutumia nyuzi zisizoonekana kwa macho, kuvu huungana na mwani, ambayo hutumia usanidimwanga kutengeneza sukari. Baadhi ya sukari hiyo huvuja kwenye kuta za mwani, na kufyonzwa na kuvu. Nao mwani hupokea unyevu kutoka kwa kuvu na kulindwa kutokana na mwangaza mkali wa jua.
Mwanasayansi mmoja alisema kwa mzaha kwamba kuvumwani ni “kuvu ambao wamegundua ukulima.” Nao wanajua sana kazi hiyo kwa kuwa kuvumwani “hufunika uso wa dunia mara kumi zaidi ya misitu ya mvua ya tropiki,” kinasema kitabu Liaisons of Life. Wako kila mahali kutoka Aktiki hadi Antaktiki na hata wao huishi kwenye migongo ya wadudu!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Matumbawe Huonyesha Maajabu ya Ushirikiano
Matumbawe hufanyizwa na chechevule na miani. Kwa kuwa miani hujaza sehemu zote za chembe za chechevule, miani hufanya matumbawe yawe na rangi nyangavu. Na mara nyingi miani huzidi chechevule kwa uzito, nyakati nyingine kwa zaidi ya mara tatu, na kufanya matumbawe yaonekane kuwa mimea badala ya wanyama! Hata hivyo, kazi kuu ya mwani huwa kutengeneza chakula, nao hutoa asilimia 98 ya chakula hicho kulipia makao. Chechevule wanahitaji chakula hicho ili kuendelea kuishi na pia kujenga matumbawe.
Miani hufaidika kutokana na ushirikiano huo kwa njia mbili hivi. Kwanza, wao hupata chakula kutokana na takataka za chechevule, yaani, kaboni dioksidi, nitrojeni, na fosfati. Pili, wao hulindwa na matumbawe magumu. Miani pia inahitaji mwangaza wa jua; kwa hiyo matumbawe hukua katika maji safi yanayopenya nuru vizuri.
Matumbawe yanapokabili mkazo, kama vile kuongezeka kwa joto la maji, chechevule huondoa miani na kupoteza rangi. Huenda yakafa kutokana na ukosefu wa chakula. Katika miaka ya hivi karibuni, wanasayansi wameona jinsi matumbawe yanavyozidi kupoteza rangi kwa kiasi kikubwa sana ulimwenguni.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Somo Kuhusu Kushirikiana
Eropleni mbili ziliruka angani kama ndege wawili waliofuatana karibukaribu. Lakini hiyo haikuwa safari ya kawaida; ilikuwa jaribio la kisayansi lililotegemea uchunguzi uliokuwa umefanyiwa ndege wanaoitwa mwari. Watafiti waligundua kwamba waari wanaoruka karibukaribu hupata nguvu zaidi za kupaa juu kutokana na waari walio mbele, na hivyo kupunguza mpigo wa moyo kwa asilimia 15 kuliko inavyokuwa wanaporuka mmojammoja. Je, eropleni zinaweza kunufaishwa na kanuni hiyo ya kupaa?
Ili kuona ikiwa hilo linawezekana, mainjinia waliweka katika ndege vifaa vya elektroniki vya hali ya juu ambavyo vingeweza kumruhusu rubani apunguze au kuongeza kwa sentimeta 30 umbali kati ya ndege yake na ile iliyokuwa mbele kwa meta 90 hivi. (Ona picha.) Matokeo yalikuwaje? Ndege yake ingeweza kusonga kwa urahisi kwa asilimia 20 kuliko kawaida na kupunguza kwa asilimia 18 kiasi cha mafuta ambacho kingetumiwa. Watafiti wanaamini kwamba utafiti huo unaweza kutumiwa katika ndege za kijeshi na za abiria.
[Hisani]
Jets: NASA Dryden Flight Research Center; birds: © Joyce Gross
[Picha katika ukurasa wa 5]
Sehemu ya kwanza ya tumbo la ng’ombe ina mfumo halisi wa ikolojia wa bakteria, kuvu, na protozoa (picha ndogo iliyoongezwa ukubwa)
[Hisani]
Inset: Melvin Yokoyama and Mario Cobos, Michigan State University
[Picha katika ukurasa wa 7]
Nyuki huwezesha maua yazae
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Ng’ombe na mchungi
[Picha katika ukurasa wa 10]
Uduvi msafishaji mwenye madoa-doa akiwa juu ya “anemone”
[Picha katika ukurasa wa 10]
Samaki anayeitwa “butterfly” akiwa pamoja na samaki mdogo msafishaji