Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wafuaji wa Nguo Wenye Bidii wa Abidjan

Wafuaji wa Nguo Wenye Bidii wa Abidjan

Wafuaji wa Nguo Wenye Bidii wa Abidjan

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI CÔTE D’IVOIRE

TULIKUWA tukisafiri kutoka Abidjan, Côte d’Ivoire, kuelekea magharibi huku tukifurahia mandhari ya jiji hilo lenye shughuli nyingi la Afrika Magharibi. Kwa ghafula, tukaona jambo la kupendeza. Tuliona eneo kubwa lenye nyasi lililokuwa limefunikwa na nguo nyingi zenye rangi maridadi. Kwa nini nguo hizo zilikuwa zimetandazwa? Marafiki wetu wa Côte d’Ivoire walitueleza sababu. Hiyo ni kazi ya fanico.

Jina fanico linarejelea kikundi cha wafuaji wa nguo wenye bidii. Kutoka macheo hadi machweo, mamia ya wanaume na wanawake wachache wenye nguvu hutafuta riziki kwa kufua nguo kwa mkono katika Mto Banco. Jina lao limetokana na maneno ya Kidyula au Kijula fani na ko. Neno fani linamaanisha “kitambaa” au “nguo,” na ko linamaanisha “kufua.” Kwa hiyo neno la Kidyula fanico linamaanisha “mtu anayefua nguo.”

Kazi ya Mfuaji

Asubuhi moja tuliwatembelea fanico kazini ili kujua mengi kuhusu kazi yao. Wana shughuli nyingi kama nini! Tayari walikuwa wameanza kazi. Mto Banco ulikuwa na tairi nyingi kubwa zilizokuwa zimetiwa mawe. Kando ya kila tairi, kulikuwa na mfuaji aliyesimama huku maji yakimfika kiunoni au mapajani. Wafuaji hao walikuwa wakifanya bidii kutia sabuni ndani ya maji, kufua, na kufikicha nguo.

Kabla ya mapambazuko, mfuaji huenda nyumba kwa nyumba ili akusanye nguo chafu. Baadhi ya wateja wake huishi kilomita tatu hivi kutoka mtoni. Yeye huweka nguo zote katika mkokoteni au anazibeba kichwani. Kisha anaelekea kwenye Mto Banco. Anapofika yeye husalimiwa katika lugha mbalimbali, kwa kuwa fanico wanaofanya kazi hapa wanatoka sehemu mbalimbali za Afrika. Wengine wamekuwa hapa kwa miaka mingi kama vile Bw. Brama, mfuaji mwenye misuli ambaye ana umri wa miaka zaidi ya 60. Wao hufanya kazi mwaka mzima isipokuwa siku tatu.

Kufua nguo ni kazi ngumu. Tulimtazama mwanamume mmoja akishusha mzigo wake wa nguo chafu. Nguo hizo zilikuwa nyingi sana hivi kwamba zingemchosha mama wa nyumbani. Alifungua mzigo huo na kuanza kuziweka nguo hizo majini. Kisha akatengeneza povu kwa kipande kikubwa cha sabuni ya mafuta ya chikichi, na kupigapiga nguo hizo moja baada ya nyingine kwenye jiwe. Nyakati nyingine alitumia brashi kuondoa madoa sugu. Mtu hulipa pesa ngapi ili afuliwe nguo? Shati ni senti 7 na shuka ni senti 14 hivi za Marekani. Hiyo ndiyo sababu fanico hufua nguo nyingi sana ili kupata riziki.

Ikiwa ungeona rundo kubwa la nguo wanazofua, huenda ungejiuliza, ‘wanawezaje kukumbuka nguo fulani ni ya nani?’ Tulifikiri huenda wanatumia mbinu ya siri ya kutia nguo alama kama ile inayotumiwa na kikundi cha wafuaji nguo huko India. Hata hivyo, mbinu inayotumiwa na fanico ni tofauti sana na ile ya wafuaji wa India, ingawa ina matokeo mazuri pia.

Kwa kuwa yule aliyetutembeza anajua habari zaidi, alitueleza mbinu ambayo fanico hutumia. Kwanza kabisa, mfuaji anapokusanya nguo, anaangalia kimo cha kila mtu katika familia ili aweze kukumbuka nguo fulani ni ya nani. Hatii alama yoyote kwenye nguo. Kisha, anafunga fundo sehemu moja ya kila nguo ya familia fulani, kwa mfano anaweza kufunga fundo kwenye mkono wa kushoto, wa kulia, kola, au kwenye mkanda wa nguo. Anapofua, anahakikisha kwamba hachanganyi nguo za familia moja na nyingine. Hilo lilionekana kuwa jambo gumu sana kwetu. Hivyo, tulimuuliza fanico mmoja iwapo amewahi kupoteza au kumpelekea mtu nguo zisizo zake. Alishangaa na kusema: ‘La. Fanico hawezi kupoteza nguo kamwe!’

Je, yeyote anaweza kwenda kwenye Mto Banco na kuanza kufua nguo? Bila shaka la! Kuna utaratibu unaofuatwa. Anayetaka kuwa fanico hupewa kipindi cha majaribio cha miezi mitatu, kipindi ambacho anafunzwa na fanico mwenye uzoefu. Huo ndio wakati anajifunza mbinu ya pekee ya kuweka mambo katika kumbukumbu. Iwapo hatafaulu kufanya hivyo, basi anahitaji kutafuta kazi kwingine. Lakini, ikiwa huyo fanico mpya ana ustadi, analipa kiasi kidogo cha pesa kisha anapewa tairi yake yenye jiwe, ambayo haitatumiwa na mtu mwingine yeyote.

Sabuni ya Mafuta ya Chikichi

Sabuni ni muhimu sana katika kazi ya mfuaji. Hivyo mfuaji mpya hufunzwa pia matumizi yanayofaa ya sabuni ya mafuta ya chikichi. Sabuni za aina tatu hutumiwa, nazo hutofautishwa kwa rangi zake. Sabuni nyeupe na ya manjano hutumiwa kwa nguo ambazo si chafu sana, nayo nyeusi hutumiwa kwa nguo chafu sana. Inakuwa nyeusi kwa sababu ya mafuta ya chikichi ambayo ndiyo kiambato kikuu. Kwa kuwa kila fanico hutumia vipande kumi vya sabuni kila siku, kuna watu wanaotengeneza sabuni karibu nao ambao huwauzia.

Tulitembelea mahali hapo sahili pa kutengenezea sabuni kwenye kilima karibu na mahali pa kufulia nguo. Kazi kubwa ya kutengeneza sabuni huanza saa 12 asubuhi. Tayari wafanyakazi huwa wamenunua vifaa vinavyohitajiwa katika soko la karibu, yaani, mafuta ya chikichi yaliyoganda, potasiamu haidroksaidi, chumvi, umajimaji wa sabuni uliochacha, mafuta ya nazi, na siagi ya kakao. Vitu vyote hivyo vinaweza kuvundishwa kwa bakteria. Wanavichemsha vitu vyote hivyo kwenye moto mkali wa kuni vikiwa kwenye pipa kubwa la chuma. Baada ya kuupika mchanganyiko huo kwa muda wa saa sita hivi, wanaumimina katika sinia na mabakuli na kungoja upoe. Saa kadhaa baadaye wanakata sabuni vipande vikubwa-vikubwa.

Halafu mwenye kutengeneza sabuni hubeba vipande vingi kichwani hadi chini ya kilima walipo fanico. Anawafikishiaje wafuaji sabuni ikiwa wana kazi nyingi ya kufua mtoni? Anateremka ndani ya maji yanayomfikia kiunoni akiwa na sabuni katika bakuli kubwa ya plastiki anayoacha ielee juu ya maji hadi kwa anayehitaji.

Mwisho wa Kazi

Fanico anapomaliza kufua nguo zote, anaenda kwenye kilima kilicho karibu na kuzianika kwenye nyasi au anazining’iniza juu ya kamba zilizotengenezwa kwa kutumia chochote kilicho karibu. Hilo hutokeza mandhari maridadi kama ile iliyotuvutia mwanzoni. Pia, huu ndio wakati mfuaji anaweza kupumzika kutokana na kazi yake ya siku hiyo. Baadaye alasiri, wakati ambapo nguo zote zimekauka, anazikunja kwa makini, labda hata anazinyoosha kwa pasi ya makaa. Jioni inapokaribia, anazikusanya nguo zote safi, zilizopigwa pasi na kuwapelekea wenye nguo.

Mwanzoni tulipoona safu hizo zote za nguo zilizoanikwa ili zikauke, hatukujua ni kazi nyingi kadiri gani iliyohitaji kufanywa. Tunafurahi sana kwamba tuliwatembelea fanico wa Abidjan, kwa kuwa sasa tunaelewa vizuri na kuthamini sana kazi ya wanaume na wanawake wote wafuaji ulimwenguni.

[Picha katika ukurasa wa 10]

 

CÔTE D’VOIRE

[Picha katika ukurasa wa 12]

Mtengenezaji wa sabuni akiuza vipande vya sabuni

[Picha katika ukurasa wa 10 zimeandaliwa na]

PhotriMicroStock™/C. Cecil