Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
“Inashangaza kwamba mwaka baada ya mwaka, Biblia ndicho kitabu kinachouzwa sana nchini Marekani—hata ingawa asilimia 90 za nyumba tayari zina angalau nakala moja. . . . Nakala milioni 25 hivi huuzwa kila mwaka.”—THE WALL STREET JOURNAL, MAREKANI.
“Kila mwaka, watu milioni 4.5 hivi ulimwenguni pote huumwa na nyoka, na makadirio fulani yanaonyesha kwamba angalau watu 100,000 hufa baada ya kuumwa na nyoka, na wengine 250,000 hulemaa kabisa.”—CHUO KIKUU CHA MELBOURNE, AUSTRALIA.
‘Katika mwaka wa 2008, barua-pepe bilioni 210 hivi zilitumwa kila siku.’—NEW SCIENTIST, UINGEREZA.
Kelele za Barabara Huathiri Kumbukumbu
“Watu walio na chumba cha kulala karibu na barabara kubwa, reli, au uwanja wa ndege huenda wakawa na tatizo la kukumbuka habari za zamani na kujifunza vitu vipya, hata kama kelele hizo hazivurugi usingizi wao.” Ndivyo alivyosema Ysbrand van der Werf wa Taasisi ya Sayansi ya Neva ya Uholanzi. Mtu anapokosa usingizi, uwezo wake wa kukumbuka na kujifunza huathiriwa. Hilo pia hutukia “usingizi wake mzito unapokatizwa . . . bila yeye kuamka,” linasema gazeti la Uholanzi de Volkskrant. Ili ufanye kazi vizuri, sehemu ya ubongo ambayo ni muhimu kwa kumbukumbu inahitaji usingizi mzito ambao hauvurugwi na “mambo yanayoleta mfadhaiko kama vile kelele na mwangaza.”
Fataki Husababisha Matatizo ya Kupumua
Huenda fataki zikaonekana kuwa zenye kupendeza sana, lakini vipande vinavyobaki angani vinaweza kuwa hatari kwa afya yako. Ili zitokeze mmweko wenye rangi mbalimbali, fataki nyingi huwa na chumvi ya metali kama vile strontiamu ambayo hutokeza rangi nyekundu na bari ambayo hutokeza rangi ya kijani. Watafiti wa Austria waliochunguza theluji iliyoanguka kabla na baada ya maonyesho ya fataki ya wakati wa sherehe za Mwaka Mpya, waligundua kwamba kiwango cha bari katika theluji hiyo kiliongezeka mara 500 hivi. Kwa kuwa sumu inayotokana na bari hubana njia za kupitisha hewa, watafiti wanasema kuwa kuvuta moshi wa fataki kunaweza kuongeza magonjwa ya mfumo wa kupumua kama vile pumu.
Tabo za Upepo Zinawaua Popo
Gazeti Scientific American linaripoti kwamba huko Alberta, Kanada, popo hupatikana wakiwa wamekufa chini ya tabo za upepo. Jambo hilo limewashangaza sana watafiti kwa sababu popo wana uwezo mzuri sana wa kutambua mawimbi ya sauti na pia wana ustadi wa kuruka. Hata hivyo, wachunguzi wamegundua kwamba asilimia 92 ya popo waliochunguzwa walikuwa wakivuja damu kwa ndani na hivyo wakakata kauli kwamba mfumo dhaifu wa kupumua wa popo hauwezi kukabiliana na kushuka ghafula kwa shinikizo la hewa ambalo husababishwa na visu vya tabo vinavyozunguka. Miisho ya visu hivyo inaweza kuzunguka kwa mwendo wa kilomita 200 kwa saa. Popo wanaohama-hama ambao hula wadudu ndio hasa huathiriwa, na inahofiwa kwamba huenda tabo za upepo zikawaua popo wengi hivi kwamba mazingira yataathiriwa.