Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Mtu wa Msituni” wa Indonesia

“Mtu wa Msituni” wa Indonesia

“Mtu wa Msituni” wa Indonesia

AKIWA amejishikilia kwenye tawi lililoonekana kuwa dhaifu sana kutegemeza mwili wake mkubwa, mnyama huyo alitukazia macho. Tulimtazama huku tukiwa na wasiwasi. Hakuonekana kama anajali, lakini sisi tulistaajabu. Tulisimama hapo na kutazamana na orangutangu, mnyama mkubwa zaidi ulimwenguni kati ya wanyama wanaoishi juu ya miti!

Orangutangu ni wa jamii ya sokwe wakubwa. Wanyama hao watulivu huishi peke yao katika misitu mikubwa ya Borneo na Sumatra. Visiwa hivyo ni kati ya visiwa viwili vikubwa zaidi Kusini-Mashariki mwa Asia. Jina orangutangu linatokana maneno mawili ya Kiindonesia, orang na hutan, yanayomaanisha “mtu wa msituni.”

Je, ungependa kujifunza mengi zaidi kuhusu sokwe hao wakubwa wenye manyoya mekundu? Basi njoo tuelekee Borneo kuwatembelea katika mazingira yao.

Tunakutana na Orangutangu

Ili tuwaone orangutangu, tulifunga safari hadi kwenye Mbuga ya Taifa ya Tanjung Puting, ambako kuna wanyama wa kila aina. Watu huenda huko hasa kuwaona orangutangu wengi sana wanaoishi huko.

Safari yetu ilianza kwenye bandari ndogo ya Kumai, ambako tulipanda mashua ya mbao yenye injini inayoitwa klotok. Tulisafiri kwenye mto huo kuingia ndani ya msitu huo. Miti mingi ya mitende ilikua kwenye ukingo wa mto huo na mamba hatari sana walijificha ndani ya maji hayo matulivu. Kelele za ajabu zilisikika ndani ya msitu huo na kutusisimua.

Tuliposhuka kutoka kwenye mashua hiyo, tulijipaka dawa ya kuzuia wadudu na tukaingia msituni. Baada ya dakika chache tu, tulimwona orangutangu wa kwanza, yule wa kiume aliyetajwa mwanzoni. Manyoya yake mekundu yaling’aa kama shaba nyekundu yalipopigwa na jua la alasiri. Misuli yake ilimfanya aonekane kama mnyama mwenye kustaajabisha!

Orangutangu wa kiume waliokomaa wanaweza kufikia kimo cha mita 1.7 na uzito wa kilogramu 90 hivi. Wale wa kike ni nusu ya uzito huo. Orangutangu wa kiume waliokomaa wana mashavu makubwa sana yanayofanya nyuso zao zionekane kuwa za mviringo. Pia wana kifuko kooni kinachoning’inia ambacho wao hutumia kunguruma. Nyakati nyingine wao hunguruma mfululizo kwa kutumia sauti nzito sana inayoweza kuendelea kwa dakika tano na kusikika zaidi ya kilomita mbili! Orangutangu wa kiume hunguruma hasa ili kuwavutia wale wa kike na kuwatisha orangutangu wengine wa kiume.

Wanaishi Juu ya Miti

Tulipokuwa tukitembea tuliwaona orangutangu waruka kutoka mti mmoja hadi mwingine. Miguu na mikono yao ina nguvu, inaweza kunyumbulika, na imejipinda. Vidole gumba vya mikono ni vifupi, lakini vidole vile vingine vyote ni virefu. Wao hushika matawi bila tatizo na kusonga kwa madaha, bila haraka.

Orangutangu hujua jinsi ya kujificha kwenye majani mengi ya msitu. Wakiwa chini wao hutembea polepole sana na wanadamu wanaweza kuwashinda kwa urahisi.

Wanyama hao huishi maisha yao yote juu ya miti, nao ndio sokwe pekee wanaofanya hivyo. Jua linapotua wao hutafuta mti wenye matawi yenye nguvu, wanakusanya matawi madogo, na kujenga kitanda chenye starehe, mita 20 juu ya ardhi. Ili wajikinge na mvua, nyakati nyingine wao hutafuta matawi na kujenga kitu kama paa, jambo ambalo sokwe wengine hawafanyi. Kazi hiyo yote huchukua dakika tano tu!

Pia orangutangu hupata matunda juu ya miti, na hicho ndicho chakula wanachopenda zaidi. Wana kumbukumbu nzuri sana na wanajua ni wakati gani na ni wapi watakapopata matunda yaliyoiva. Pia wao hula majani, maganda ya miti, matawi madogo, asali, na wadudu. Nyakati nyingine orangutangu hutumia kijiti kutoa asali au wadudu walio ndani ya mashimo kwenye miti. Kwa ujumla, orangutangu hula zaidi ya aina 400 za chakula!

Tulipoendelea na safari yetu, tulijionea jambo lingine lenye kushangaza—tuliwakuta orangutangu wakila ndizi nyingi sana. Wanyama hao walitunzwa na wanadamu kisha baadaye wakaachiliwa warudi msituni. Kwa kuwa hawajui jinsi ya kujitunza kabisa kama orangutangu wengine wanaoishi msituni, wao hupewa chakula kuongezea kile wanachojitafutia.

Maisha ya Familia ya Orangutangu

Tulitazama vitoto vyenye kuvutia vikiwa vimejishikilia kwa mama zao na wengine wachanga wakichezacheza kwa utukutu ardhini au juu ya miti. Orangutangu wa kike wanaweza kuishi kwa miaka 45. Wanapofikia umri wa miaka 15 au 16 wao huzaa mara moja kila baada ya miaka saba au nane. Orangutangu wa kike hawezi kuzaa zaidi ya mara tatu maishani. Hilo huwafanya kuwa wanyama ambao hawazaani sana duniani.

Mama na mtoto huwa na uhusiano wa karibu sana. Orangutangu wa kike hunyonyesha na kuwazoeza watoto wao kwa miaka minane au zaidi. Mwaka wa kwanza, mtoto huyo hubebwa na mama yake kila wakati. Baada ya mwaka huo haendi mbali na mama yake hadi mtoto mwingine anapozaliwa. Ikiwa ni wa kike ataanza kumtazama mama akimtunza ndugu au dada yake aliyetoka tu kuzaliwa.

Hata hivyo, orangutangu wa kiume hufukuzwa na mama punde tu mtoto mwingine anapozaliwa. Kisha, wataishi msituni peke yao katika eneo lenye ukubwa wa kilomita 15 hivi za mraba. Wao huwaepuka wengine wa kiume nao hukutana na wale wa kike wakati wa kuzaliana.

Kwa kawaida, orangutangu wa kike hukaa katika eneo dogo la msitu maisha yao yote. Mara kadhaa wao hula pamoja na orangutangu wengine wa kike kwenye mti mmoja, lakini hawashirikiani kwa ukaribu sana. Kujitenga kwa njia hiyo huwafanya orangutangu kuwa tofauti na sokwe wengine. Lakini ili tujifunze mengi zaidi kumhusu “mtu wa msituni,” tulihitaji kutembelea eneo lingine.

Sokwe Wanaokaribia Kutoweka

Katika mbuga hiyo ya wanyama kuna Kambi ya Leakey—kituo cha kuwatunza na kuwachunguza kilichopewa jina la mtaalamu wa tabia na utamaduni Louis Leakey. Katika kituo hicho watu wanaweza kuwakaribia orangutangu. Wengine walikuja kusimama karibu nasi na hata wakatufanyia sarakasi. Orangutangu mmoja wa kike alijaribu kunyakua koti la rafiki yangu! Tulifurahia kuwa karibu sana na wanyama hao wenye kupendeza.

Hata hivyo, Kambi ya Leakey hutoa onyo hili: Orangutangu wanatoweka polepole. Wanamazingira fulani wanasema kwamba hakuna matarajio ya wanyama hao kupatikana msituni katika miaka kumi hivi ijayo. Fikiria hatari tatu wanazokabili.

Ukataji wa miti. Karibu asilimia 80 ya makao ya orangutangu yameharibiwa katika miaka 20 iliyopita. Indonesia hupoteza angalau kilomita 51 za mraba kila siku, eneo linalolingana na viwanja vitano vya mpira kila dakika.

Uwindaji haramu. Wanadamu wanapoendelea kuharibu misitu, orangutangu hukabili hatari ya kuwindwa. Fuvu la orangutangu linaweza kuuzwa kwa dola 70 za Marekani katika biashara ya magendo. Wengine huwaua orangutangu kwa sababu ya kuharibu mimea yao. Wengine huwaua kwa ajili ya chakula.

Biashara ya wanyama-vipenzi. Katika biashara ya magendo, mtoto wa orangutangu anaweza kuuzwa kwa dola mia kadhaa kufikia maelfu ya dola za Marekani. Inakadiriwa kwamba watoto wa orangutangu 1,000 hivi huuzwa kila mwaka.

Serikali na mashirika ya kibinafsi hujitahidi kuwaokoa orangutangu ili wasitoweke. Jitihada hizo zinatia ndani kuanzisha vituo vya kuwatunza wanyama, kuwahamasisha watu kupitia programu za mafunzo, kuanzisha hifadhi za kitaifa, na kudhibiti ukataji wa miti usio halali.

Biblia inaonyesha kuwa hivi karibuni Mungu ‘atawaharibu wale wanaoiharibu dunia’ na kuifanya dunia yote iwe paradiso. (Ufunuo 11:18; Isaya 11:4-9; Mathayo 6:10) Wakati huo, maneno haya ya mtunga zaburi yatatimizwa: “Miti yote ya msituni na ishangilie.” (Zaburi 96:12) Wanyama kama vile orangutangu, “mtu wa msituni” wa Indonesia, wataishi bila kutishwa na wanadamu.

[Picha katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MALASIA

Borneo

INDONESIA

Sumatra

AUSTRALIA

[Picha katika ukurasa wa 16]

Orangutangu wa kiume ana mashavu makubwa

[Hisani]

© imagebroker/Alamy

[Picha katika ukurasa wa 17]

Orangutangu husonga kwa kasi juu ya miti lakini wao husonga polepole ardhini

[Hisani]

Top: © moodboard/Alamy; bottom: Orangutan in the Camp Leakey of Tanjung Puting National Park, managed by BTNTP, UPT Ditjen PHKA Dephut

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Orangutan in the Camp Leakey of Tanjung Puting National Park, managed by BTNTP, UPT Ditjen PHKA Dephut

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Orangutan in the Camp Leakey of Tanjung Puting National Park, managed by BTNTP, UPT Ditjen PHKA Dephut