Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mwone na Umsikie “Mfalme wa Saa”

Mwone na Umsikie “Mfalme wa Saa”

Mwone na Umsikie “Mfalme wa Saa”

MOTO ulipoharibu Jumba la Kifalme la Westminster mnamo 1834, wanasiasa wa Uingereza walianzisha shindano. Ni nani atakayechora ramani bora zaidi ya jengo jipya la Bunge? Mchoro ulioshinda wa Sir Charles Barry, ulikuwa wa jumba la kifalme lenye muundo wa Kigothi lenye madoido mengi lililokuwa na mnara wenye saa yenye pande nne. Wizara iliyosimamia mali za kifalme na za serikali iliidhinisha ujenzi wa “Mfalme wa Saa, [saa] kubwa kuliko zote ulimwenguni.”

Saa hiyo ni mojawapo ya vitu vinavyojulikana sana huko London, na sauti ya kengele yake inatambuliwa ulimwenguni pote. Jina la saa hiyo ni Big Ben—ingawa mwanzoni jina hilo liliwakilisha tu kengele yake kubwa. Saa hiyo inayojulikana sana ulimwenguni pote imebuniwa kwa ustadi sana.

Kazi Kubwa

Ujenzi wa mnara huo wa saa wenye kimo cha mita 96 ulianza mnamo 1843. Miaka mitatu baadaye fundi alianza kutafutwa ambaye angejenga saa sahihi sana hivi kwamba haingepoteza zaidi ya sekunde moja kila saa. Hiyo ilikuwa kazi kubwa sana. Kwa kuwa saa hiyo ingewekwa kwenye mnara mrefu sana bila kufunikwa, mikono yake ingeweza kupigwa na upepo, theluji, na barafu—na hata hua wangetua juu yake! Mambo kama hayo yangeathiri pinduli ya saa hiyo ambayo ilipaswa kusonga bila hitilafu ili kudumisha wakati sahihi. Huku wataalamu wakijadili jinsi ambavyo wangeweza kutatua matatizo hayo, mtaalamu wa saa Edmund Beckett Denison alitokeza mchoro uliowavutia, na fundi stadi wa saa akapewa kazi ya kuijenga.

Baada ya miaka miwili saa hiyo ilikuwa tayari, lakini ilikaa katika karakana ya fundi huyo kwa miaka mingine mitano ikisubiri ujenzi wa mnara huo ukamilike. Wakati huo, Denison alibuni kifaa kilicholinda pinduli isitatizwe na chochote na hivyo kudumisha usahihi wa saa hiyo.

Big Ben Atokea

Kwa kuwa ubuni wa saa hiyo ulikuwa umekamilika, hatua iliyofuata ilikuwa kutengeneza kengele zake. Karakana moja huko kaskazini mashariki mwa Uingereza ilitengeneza kengele hiyo. Ilikuwa kubwa kuliko ilivyotazamiwa na ilikuwa na uzito wa zaidi ya tani 16! Kengele hiyo ilikuwa nzito sana hivi kwamba iliharibu sitaha ya meli iliyopaswa kuipeleka London. Mwishowe, meli hiyo ilifunga safari. Ilipofikishwa kwenye nchi kavu, kengele hiyo ilisafirishwa katika gari la pekee lililokokotwa na farasi weupe 16. Kisha, ikaning’inizwa mbele ya Bunge ili ijaribiwe.

Kengele nyingi kubwa zina majina, na kengele hiyo kubwa iliitwa Big Ben. Kwa nini? Hakuna anayejua. Wengine wanasema kwamba huenda ilipewa jina la Sir Benjamin Hall, mwanamume mkubwa aliyefanya kazi kwenye Bunge. Wengine wanasema ilipewa jina la Benjamin Caunt, mwanandondi wa uzani wa juu aliyekuwa maarufu wakati huo. Popote ambapo jina Big Ben lilitoka—ambalo sasa haliwakilishi kengele hiyo peke yake—linatumiwa kurejelea saa yote pamoja na mnara wake.

Kuharibika Mara Mbili

Nyundo ya kwanza iliyotumiwa kupiga kengele ya Big Ben ilionwa kuwa nyepesi sana, kwa hiyo, ikabadilishwa na nyundo yenye uzito wa kilogramu 660. Hata hivyo, baada ya kujaribiwa kwa miezi kadhaa hitilafu ikatokea. Kengele hiyo ilipata ufa ambao haungeweza kurekebishwa. Kwa hiyo, kengele hiyo ilihitaji kuondolewa. Chuma chake kiliyeyushwa na kutumiwa kutengeneza kengele nyingine iliyokuwa na uzito wa tani 13.7. Kwa mara nyingine tena, umati ulikusanyika kando ya barabara wakati gari la kukokotwa lililobeba kengele hiyo mpya lilipopita likielekea kwenye majengo ya Bunge.

Baada ya miezi kadhaa, mnara huo ulikuwa tayari. Vikundi kadhaa vilifanya kazi bila kupumzika ili kuinua Big Ben na kuiweka mahali pake. Mwishowe, kengele hiyo kubwa iliunganishwa na kengele ndogo nne zilizotoa sauti kila baada ya robo saa. Mitambo mingine mizito ya saa hiyo ikainuliwa baada yake. Hatimaye, “Mfalme wa Saa” alionekana kuwa tayari kuanza kazi yake.

Mnamo Julai (Mwezi wa 7) 1859, kengele hiyo iliyoitwa Big Ben ilianza kusikika baada ya kila saa. Lakini ilifanya hivyo kwa muda mfupi tu. Mwanzoni mwa Oktoba (Mwezi wa 10), kengele hiyo kubwa ilipata ufa tena! Haingeweza kuondolewa kwenye mnara huo. Badala yake, wafanyakazi waliigeuza hivi kwamba nyundo yake haikupiga ufa huo. Kisha ili kuzuia isiharibike tena wakati ujao, nyundo hiyo ilibadilishwa na nyingine nyepesi. Baada ya miaka mitatu Big Ben ilianza tena kufanya kazi! Ufa huo bado upo, nao unafanya kengele hiyo itokeze sauti fulani ya kipekee.

Matukio ya Pekee

Mnamo 1924, Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, liliweka mikrofoni kwenye mnara wa saa hiyo na kuanza kutangaza sauti ya Big Ben kwa ukawaida ili kuonyesha wakati unaopaswa kufuatwa na nchi yote. Miaka minane baadaye, wasikilizaji katika maeneo yote ya Jumuiya ya Madola ya Uingereza walikuwa wakisikiliza sauti hiyo, na leo pia sauti ya Big Ben inasikika ulimwenguni pote kupitia Idhaa ya Dunia ya BBC.

Ingawa saa hiyo pamoja na kengele zake ziliokoka Vita vya Pili vya Ulimwengu, saa hiyo iliharibika mnamo 1976 kutokana na kuchakaa kwa chuma katika kifaa kinachowezesha sauti itokezwe. Hata hivyo, kengele yenyewe haikuharibika sana na baada ya majuma kadhaa ikaanza tena kutoa sauti baada ya kila saa. Kazi ya kurekebisha saa yenyewe ilichukua miezi tisa.

Kwa muda mrefu, Big Ben ilikuwa ndiyo saa kubwa zaidi ulimwenguni, na bado ndiyo saa sahihi zaidi ya umma. Kwa kuwa ubuni wake umeigwa sana, unaweza kusikia sauti yake katika saa nyingine ndogo au kubwa katika nchi nyingi. Si ajabu basi kwamba Big Ben imekuwa ishara ya kutambulisha nchi ya Uingereza pamoja na mji wake mkuu. Hiyo kwa kweli ni “Mfalme wa Saa”!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

KUHAKIKISHA INADUMISHA WAKATI

Mara tatu kila juma, mtaalamu hupanda ngazi 300 kupitia ngazi iliyojipinda ili akatie saa hiyo majira kwa mkono. Mtaalamu huyo huhakikisha kwamba saa hiyo inafuata wakati sahihi. Pinduli yake yenye urefu wa mita 4 hubembea baada ya kila sekunde mbili. Sehemu fulani ndogo ya saa hiyo huwa imewekelewa sarafu fulani za kale. Ikiwa saa hiyo inapoteza muda mtaalamu huyo huongeza sarafu moja. Iwapo inazidi, anaondoa sarafu moja.

[Picha]

Sarafu za kale husaidia kudumisha wakati

[Hisani]

Winding clock: AP Photo/Lefteris Pitarakis; coins on ledge: Parliamentary copyright images are reproduced with the permission of Parliament

[Picha katika ukurasa wa 19]

Kengele yenye uzito wa tani 13.7 (Big Ben) hutoa sauti baada ya kila saa

[Hisani]

Popperfoto/Getty Images