Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matetemeko Makubwa Zaidi Yanatazamiwa

Matetemeko Makubwa Zaidi Yanatazamiwa

Matetemeko Makubwa Zaidi Yanatazamiwa

TANGU vifaa vinavyoweza kupima nguvu ya tetemeko la nchi vilipobuniwa, wanasayansi wamerekodi mamia ya matetemeko makubwa ya nchi. Matetemeko yanayotukia mbali na maeneo ambayo yana watu wengi hayasababishi wasiwasi mwingi na hata hayatangazwi na vyombo vya habari. Kwa upande mwingine, uharibifu mkubwa unaweza kutokea tetemeko la nchi linapopiga jiji kubwa. Wanadamu watakaokufa na mali zitakazoharibiwa hutegemea hasa idadi ya watu na matayarisho ambayo wamefanya ili kukabiliana na misiba ya asili.

Januari 12, 2010, Haiti ilikumbwa na moja kati ya matetemeko mabaya zaidi katika historia inapokadiriwa ni watu wangapi waliokufa na mali iliyoharibika. Lakini halikuwa tetemeko la kwanza wala halikuwa tetemeko kubwa peke yake kutukia mwaka huu. Maelezo yafuatayo yanaonyesha matetemeko fulani ya nchi yaliyotokea katika miezi ya kwanza ya mwaka wa 2010 ambayo yalipimwa na kuonekana kuwa yenye nguvu kama lile lililoharibu mji mkuu wa Haiti au yenye nguvu zaidi.

Januari 3: Kipimo cha 7.1 Kwenye Richter, Visiwa vya Solomon

Tetemeko hilo kubwa, ambalo mwanzoni lilikadiriwa kuwa zaidi ya 7.1 kwenye Richter, lilisababisha tsunami yenye “kimo cha mita 2 hadi 3 ya maji ya bahari.” Loti Yates, mkurugenzi wa Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Misiba alieleza kwamba watu waliokuwa ndani ya ndege iliyokuwa ikipaa juu ya visiwa hivyo waliona sehemu za visiwa hivyo zikiwa “zimefunikwa kabisa kwa maji.” Kulingana na Yates, katika kijiji cha Bainara kilicho kwenye Kisiwa cha Rendova, nyumba 16 zilibomolewa kabisa na nyingine nyingi zikaharibiwa kwa kiasi fulani.

Tetemeko hilo la nchi lilitanguliwa na tetemeko lingine dogo lenye kipimo cha 6.6 kwenye Richter. Wengi walishtuka wakati tetemeko hilo dogo lilipopiga na wakakimbilia milimani. Kwa kufanya hivyo, waliokoka wakati tsunami iliyotokezwa na tetemeko hilo kubwa zaidi ilipopiga saa mbili hivi baadaye.

Februari (Mwezi wa 2) 26: Kipimo cha 7.0 Kwenye Richter, Visiwa vya Ryukyu, Japani

Tetemeko hilo la nchi lilipiga saa 11:31 alfajiri, na lilianzia hasa kilomita 80 kutoka Naha, Okinawa, kwenye moja ya Visiwa vya Ryukyu, Japani. Maonyo ya tsunami yalitolewa lakini baadaye yakafutwa. Mwanamke fulani ambaye ameishi huko Okinawa kwa zaidi ya miaka 90 anasema kwamba hajawahi kusikia tetemeko lingine lenye nguvu kuliko hilo.

Februari 27: Kipimo cha 8.8 Kwenye Richter, Chile

Tangu mwaka wa 1900, hilo ndilo tetemeko la tano lenye nguvu zaidi. Tetemeko lenye nguvu zaidi lilitokea pia nchini Chile katika mwaka wa 1960—lilikuwa na kipimo cha 9.4 kwenye Richter. Tetemeko hilo, pamoja na lile lenye kipimo cha 7.7 kwenye Richter lililoharibu mji mkuu wa Chile katika mwaka wa 1985, lilifanya nchi hiyo iimarishe sheria zake za ujenzi.

Kwa sababu hiyo, majengo kadhaa huko Santiago na katika majiji mengine yaliyoathiriwa na tetemeko la nchi lililotokea mwaka huu yalibomoka. Hata hivyo, maelfu ya watu walijeruhiwa na mali zao zikapotea. Inasemekana kwamba huenda watu 500 hivi walikufa, karibu nusu yao wakifa katika tsunami iliyopiga ufuo wa Chile.

Aprili (Mwezi wa 4) 4: Kipimo cha 7.2 Kwenye Richter, Baja California, Mexico

Chanzo chake kilikuwa kilomita 18 kutoka Guadalupe Victoria, Mexico, na kilomita 47 kutoka Mexicali. Eneo hilo ni la mbali na sehemu yake kubwa haina watu. Hata hivyo, watu katika majiji na miji mingi ya Mexico na kusini mwa Marekani walisikia tetemeko hilo.

Mei 9: Kipimo cha 7.2 Kwenye Richter, Sumatra Kaskazini, Indonesia

Tetemeko hilo la chini ya maji lilitukia saa sita hivi mchana kilomita 217 hivi kutoka Banda Aceh, jiji lililoko upande wa kaskazini zaidi mwa Indonesia. Watu wengi walikimbia nje ya nyumba zao na kwa muda fulani wakakataa kurudi kwa sababu ya woga. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyekufa.

Mengine Yanatazamiwa

Kutokana na historia ya matetemeko makubwa kupiga sayari yetu, ni jambo linalopatana na akili kutazamia mengine katika miaka ijayo. Shirika la Marekani la Uchunguzi wa Jiolojia linasema wazi hivi: “Matetemeko makubwa yataendelea kutokea kama vile yamekuwa yakitokea.”

Kwa kupendeza, gazeti moja lilisema hivi: “Matetemeko ya nchi ya hivi karibuni . . . hayawezi kuzuiwa na mwanadamu yeyote na yanatukumbusha kwamba uwezo wa mwanadamu una mipaka. Hilo halimaanishi kwamba hatupaswi kuchukua hatua tunapoweza kufanya hivyo . . . , lakini linamaanisha kwamba tunapaswa kuendelea kutazamia misiba mikubwa zaidi ya asili ambayo hatuwezi kuizuia.”

Wanafunzi makini wa Biblia wanalazimika kufikiria kuhusu unabii wa Biblia unaotaja matetemeko ya nchi moja kwa moja kuwa ishara ya siku za mwisho za mfumo huu wa mambo.—Mathayo 24:3, 7; Marko 13:8; Luka 21:11.

[Ramani katika ukurasa wa 20, 21]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Baadhi ya matetemeko yenye kipimo cha 7.0 au zaidi kwenye Richter kuanzia Januari hadi Mei

Mexico

Haiti

Chile

Japani

Indonesia

Visiwa vya Solomon