Je, Makongamano Yametimiza Chochote?
Je, Makongamano Yametimiza Chochote?
“Serikali ulimwenguni kote lazima ziungane ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Wanasayansi wengi wanakubali kwamba tusipochukua hatua yoyote, tutaendelea kukumbwa na njaa, ukame, na watu wengi zaidi watahama maeneo wanamoishi na hilo litachochea mizozo miaka nenda miaka rudi.”—Rais wa Marekani Barack Obama.
BAADHI ya wanasayansi wanasema kwamba Dunia inaugua. Ina homa. Kwa maoni yao, huenda hali ya joto duniani inakaribia kufikia kile kiwango hatari zaidi ambapo joto likiongezeka kidogo tu, “kutakuwa na badiliko lenye kutia hofu katika mazingira ambacho kitafanya kiwango cha joto ulimwenguni kiongezeke kwa kiwango kikubwa zaidi,” linaripoti gazeti la Uingereza The Guardian.
Tulijipata jinsi gani katika hali hii? Je, inaweza kurekebishwa? Je, kwa kweli wanadamu wanaweza kutatua tatizo la kuongezeka kwa joto ulimwenguni—kutia ndani matatizo mengine mengi na makubwa zaidi yanayowakumba wanadamu?
Wanasayansi wengi wanaamini kwamba utendaji wa wanadamu ndio tatizo kubwa, tangu wakati wa ule mvuvumuko wa kiviwanda na baada ya hapo watu wakaanza kutumia nishati za asili kwa wingi zaidi, kama vile makaa-mawe na mafuta. Tatizo lingine linahusiana na watu kukata miti kupita kiasi. Misitu ndiyo mapafu ya mazingira yetu. Miti hufyonza gesi fulani zinazosababisha kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani. Hata hivyo, ukataji wa misitu kiholela husababisha gesi hizo ziongezeke katika angahewa. Ili kushughulikia matatizo haya, viongozi wa ulimwengu wamepanga makongamano ili kuzungumzia jinsi ya kuboresha hali ya hewa.
Mkataba wa Kyoto
Mkataba au makubaliano ya Kyoto ya mwaka wa 1997 yaliweka azimio jipya kuhusu utokezaji wa kaboni dioksidi. Kwa kutia sahihi mkataba huo, nchi za Muungano wa Ulaya na nchi nyingine 37 zilizoendelea zilikubali wajibu wa kupunguza utokezaji wa gesi hizo kwa wastani wa asilimia 5 chini ya kiwango walichotokeza mwaka wa 1990, na wangefanya hivyo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa 2008 hadi 2012.
Hata hivyo, Mkataba huo wa Kyoto, ulikuwa na upungufu fulani. Kwa mfano, Marekani ilikataa kutia sahihi. Pia, nchi kubwa zinazoendelea, kama China na India, hazikukubali kufuata viwango hususa vilivyowekewa. Ukweli ni kwamba Marekani na China pekee zinatokeza asilimia 40 ya kaboni dioksidi inayotokezwa ulimwenguni pote.
Kongamano la Copenhagen
Kongamano la Copenhagen, linaloitwa COP 15, lilipaswa kuchukua mahali pa ule Mkataba wa Kyoto na kuanzisha mikakati mipya ya kudumu, kuanzia mwaka wa 2012 na kuendelea. * Ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, wawakilishi kutoka mataifa 192, kutia ndani wakuu 119 wa nchi mbalimbali, walikusanyika mjini Copenhagen, Denmark, mnamo Desemba 2009 ili kuhudhuria kongamano hilo. COP 15 ilikumbwa na matatizo matatu yafuatayo:
1. Kufikia makubaliano ya kisheria. Je, nchi zilizoendelea zingekubali viwango vilivyowekwa vya kutokeza gesi, na je, nchi kuu zilizoendelea zingekubali kupunguza utokezaji wa gesi hizo?
2. Kugharimia tatizo lenye kuendelea. Nchi zinazoendelea zingehitaji mabilioni ya dola kwa miaka mingi ili kukabiliana na matokeo mabaya yanayoongezeka kutokana na kupanda kwa joto duniani na pia zingehitaji kubuni teknolojia ambazo hazidhuru mazingira.
3. Kukubaliana juu ya mfumo wa kudhibiti utokezaji wa gesi. Mfumo kama huo ungezuia nchi yoyote isipite kiwango cha gesi iliyoruhusiwa kutokeza. Pia, ungesaidia kuhakikisha kwamba nchi zinazoendelea zinatumia vizuri pesa za ufadhili.
Je, walifaulu kutatua matatizo hayo matatu? Kulikuwa na majadiliano makali hivi kwamba ikaonekana kwamba hawatafikia mkataa wowote. Katika dakika za mwishomwisho za mkutano huo, viongozi kutoka nchi 28 walikubaliana kutia sahihi ile hati inayoitwa Makubaliano ya Copenhagen. Makubaliano hayo yalipokewa shingo-upande kwa maneno haya: “Kongamano hili . . . linaitambua hati ya Makubaliano ya Copenhagen,” linasema shirika la habari la Reuters. Kwa maneno mengine, kila nchi itajiamulia ikiwa itafuata mkataba huo.
Tutazamie Nini?
Makongamano zaidi yameshafanywa au yamepangwa kuwa yatafanywa, lakini wengi wanashuku ikiwa yatatokeza suluhisho lolote. “Sayari yetu itaendelea kuungua kwa joto,” akasema mwandishi wa gazeti la New York Times Paul Krugman. Mara nyingi, manufaa za muda mfupi za kisiasa na kiuchumi hufanya wengi wasichukulie kwa uzito jinsi mazingira yanavyoathiriwa, na hilo huchochea mataifa yaendelee kufanya mambo kama kawaida. “Ukitaka kujua kwa nini ni vigumu kwa makubaliano kuhusu mazingira kufanikiwa, chunguza ni pesa ngapi zinazotokezwa,” anasema Krugman. Pia, aliandika kwamba mikakati inayohusu mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi yake ilisambaratishwa na “mambo mawili ya kawaida: pupa na woga [wa kisiasa].”
Kuongezeka kwa joto duniani kunafanana kwa njia fulani na kimbunga. Wataalamu wa hali ya hewa wanaweza kupima nguvu za kimbunga kwa kadiri fulani na kujua kwa usahihi kitaelekea upande gani—na hilo litawatahadharisha watu wanaoishi eneo ambako kitapita. Lakini wanasayansi wote, wanasiasa, na wanabiashara mashuhuri ulimwenguni hawana uwezo wa kusimamisha kimbunga. Inaonekana kuwa ndivyo ilivyo pia kuhusiana na kuongezeka kwa joto duniani. Ukweli huo wa mambo unatukumbusha maneno yanayopatikana kwenye andiko la Yeremia 10:23: “Njia ya mtu wa udongo haimo katika uwezo wake. Mwanadamu anayetembea hana uwezo wa kuongoza hatua yake.”
Mungu Ndiye Atakayekomesha Kuongezeka kwa Joto Duniani
Biblia inatuambia kwamba “Mfanyizaji wa dunia na Mtengenezaji wake . . . hakuiumba tu bila sababu.” (Isaya 45:18) Biblia pia inasema: “Dunia inadumu milele.”—Mhubiri 1:4, Zaire Swahili Bible.
Naam, Mungu hataruhusu dunia iharibiwe kiasi cha kwamba isiweze kukaliwa na watu. Badala yake, ataingilia mambo ya wanadamu na kukomesha utawala wao ulioshindwa kuongoza mambo na kuwaangamiza wale wanaoiharibu dunia. Wakati huohuo, atawahifadhi hai wote wanaofuata viwango vya juu vya maadili maishani na ambao wanajitahidi kwa dhati kumfurahisha. Methali 2:21, 22 inasema hivi: “Wanyoofu ndio watakaokaa duniani, na wasio na lawama ndio watakaobaki ndani yake. Nao waovu, watakatiliwa mbali kutoka duniani; nao wenye hila, watang’olewa kutoka ndani yake.”
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 10 Kongamano la Wanaohusika (The Conference of the Parties), COP, hupangwa kwa ukawaida na Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Muundo wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa.
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
Gesi inayoongeza joto duniani ni sehemu ya angahewa inayofyonza mnururisho unaotoka kwenye uso wa dunia. Gesi nyingi zinazopaa kwenye angahewa kutoka kwenye viwanda vya kisasa zinaongeza joto duniani. Zinatia ndani kaboni dioksidi, gesi za chlorofluorocarbon, methani, na oksidi nitrasi. Tani zaidi ya bilioni 25 za gesi ya kaboni dioksidi pekee hupaa angani kila mwaka. Ripoti zinaonyesha kwamba tangu enzi ya ustawi wa kiviwanda, kiwango cha kaboni dioksidi angani kimeongezeka kwa asilimia 40.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]
Earth: NASA/The Visible Earth (http://visibleearth.nasa.gov/); Barack Obama: ATTILA KISBENEDEK/AFP/Getty Images