Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Asilimia 76.3 ya watu wazima waliohojiwa nchini Ujerumani, walisema kwamba kuchezea wengine kimahaba ni “zoea ambalo halina madhara yoyote” na “haimaanishi kwamba anayemchezea mwingine anavutiwa naye kimahaba.” Karibu nusu ya waliohojiwa walisema kwamba ni sawa tu kwa mtu aliyeoa au kuolewa kumchezea kimahaba mtu asiyemjua.—APOTHEKEN UMSCHAU, UJERUMANI.
Utafiti uliofanywa katika nchi nzima huko Urusi unaonyesha kwamba asilimia 48 ya Warusi wanaamini kwamba mashambulizi ya kigaidi yamekuwa “jambo linalotarajiwa kabisa” na ni “hali ya kawaida ya maisha.”—KOMMERSANT, URUSI.
“Wakijaribu kutumia mbinu ambayo wanajeshi walitumia zamani walipokuwa wakivamia mji wenye kuta ndefu,” hivi karibuni wafanyabiashara ya magendo nchini Mexico walijaribu kukwepa ulinzi wa mpakani kwa kutumia “manati makubwa” yaliyofungwa kwenye lori yaliyo na mpira wenye nguvu, ili warushe dawa za kulevya kaskazini na kuzivusha juu ya mpaka wa Marekani.—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, MAREKANI.
Wakati ambapo mambo yanaonyesha kuwa watu katika jiji la New York wamepunguza kiasi cha uvutaji wa sigara, wanakula vizuri zaidi, na wanaendesha baiskeli zaidi, takwimu fulani ambayo haijabadilika ni kuhusu idadi ya mimba zinazotolewa. “Mimba mbili kati ya tano” katika mji wa New York hutolewa. Kiwango hicho “hakijabadilika kwa zaidi ya miaka kumi.”—THE NEW YORK TIMES, MAREKANI.
Watu wanaodhibiti wadudu wasumbufu walipigwa na butwaa walipoitwa wamkamate mbweha kwenye orofa ya 72 ya jengo refu linaloendelea kujengwa katikati mwa mji wa London. Mnyama huyo “aliyeishi kwa kutegemea makombo ya chakula yaliyoachwa na wajenzi,” aliachiliwa huru katika eneo la karibu.—THE TELEGRAPH, LONDON.
Makasisi wa Urusi Wanaweza Kugombea Vyeo vya Kisiasa
“Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Othodoksi nchini Urusi limeruhusu makasisi wao kugombea vyeo vya kisiasa katika hali za pekee ili kulinda kanisa dhidi ya mafarakano na mambo mengine yanayotisha moja kwa moja kugawanya kanisa,” linasema shirika la habari liitwalo RIA Novosti. Kulingana na taarifa ya maaskofu hao, hali kama hizo zinaweza kutokea wakati kuna uhitaji wa “kukabiliana na uvutano mbalimbali, kutia ndani watu wanaotaka kusababisha mafarakano na wale wanaotoka katika madhehebu mengine, ambao wangependa kutumia mamlaka yao ya kisiasa kulipiga vita Kanisa Othodoksi.”
Matatizo Mapya ya Kisheria
Mbinu mpya za kusaidia wenzi wa ndoa wasio na uwezo wa kuzaa ili wapate mtoto, ambazo hazikuwahi kufikiriwa kuwa zinaweza kufanya kazi, zimetokeza matatizo mapya ya kisheria. “Kila mwaka, watoto wengi huzaliwa kutokana na mimba iliyotungwa kwa mbegu za uzazi za kike au za kiume ambazo zimekuwa kwenye hifadhi kwa miezi au miaka kadhaa,” linaeleza jarida linaloitwa The Wall Street Journal. “Katika visa fulani, mzazi mmoja, hasa baba, mara nyingi huwa tayari amekufa.” Nchini Marekani, watoto fulani ambao ni mayatima hupewa malipo ya kila mwezi kutoka kwa mfumo wa Huduma za Kijamii. Lakini sheria zinatofautiana katika kila jimbo kuhusiana na kama malipo hayo yanapaswa kutolewa ikiwa mtoto anazaliwa baada ya mzazi mmoja kufa. “Teknolojia imesonga sana kiasi cha kwamba sheria zilizowekwa haziwezi kukabiliana na hali mpya zinazotokezwa,” anasema mwanasheria wa mji wa Minnesota anayeitwa Sonny Miller.