Wadudu Wanaoliwa—Mlo Ambao Hatutausahau
Wadudu Wanaoliwa—Mlo Ambao Hatutausahau
MIMI, mke wangu pamoja na marafiki wetu kadhaa tumealikwa tule mlo katika mtaa wenye utulivu huko Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
“Karibuni! Natumai mna njaa!” wanatuambia tunapowasili. Hata kabla ya kuingia, tunanusa harufu nzuri ya vitunguu, vitunguu saumu, vikolezo, na tunawasikia marafiki wetu wakizungumza kwa msisimko. Ella, ambaye ndiye mkaribishaji wetu anatueleza kuhusu chakula tulichoandaliwa.
Ella anatuambia hivi: “Wadudu ni chanzo muhimu sana cha protini kwa ajili ya watu wengi huku Afrika ya Kati. Lakini hatuli wadudu kwa sababu hatuna chakula kingine; tunawala kwa sababu wana ladha nzuri.” Anaendelea kusema, “Leo tutakula makongo—viwavi.”
Jambo hilo halikupaswa kutushangaza. Ingawa huenda watu fulani wasifurahie kula wadudu, katika nchi zaidi ya 100, baadhi ya wadudu huonwa kuwa chakula kitamu sana.
Karamu Msituni
Aina mbalimbali za wadudu huliwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Wakati wa majira ya mvua, kumbikumbi wanaoitwa bobo hupatikana wakirukaruka juu ya vichuguu, na katika maeneo ya mjini wao hupatikana mahali palipo na mwangaza wa umeme. Baada ya mvua kubwa kunyesha jioni, watoto hukimbia na kuwajaza kwenye vikapu—mara nyingi wao huwatupa mdomoni mwao wakicheka kwa furaha. Kumbikumbi hao huliwa baada ya kukaushwa juani, wakiwa wamekaangwa kwa chumvi, na wakiwa wametiwa pilipili au huenda wakachanganywa na kuchemshwa pamoja na mchuzi au maandazi ya aina fulani.
Kindagozo ni panzi wenye rangi ya kijani ambao hupatikana katika nchi hiyo wakati wa kiangazi.
Watu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati huwakaanga au kuwachemsha katika maji baada ya kuwaondoa miguu na mabawa.Aina mbalimbali za viwavi huliwa nchini kote. Tulialikwa kufurahia viwavi vya Imbrasia. Nondo mkubwa mwenye rangi ya kahawia hutaga mayai yake kwenye mti wa mbambakofi. Baada ya mayai kuanguliwa, wanakijiji hukusanya viwavi vinavyotoka na kuviosha. Kisha viwavi hivyo huchemshwa pamoja na nyanya, vitunguu, na vikolezo vingine ikitegemea kile ambacho familia ingependa kula. Huenda baadhi ya viwavi hivyo vikakaushwa kwa njia mbalimbali ili vihifadhiwe. Vinaweza kuhifadhiwa kwa miezi mitatu hivi ili viliwe baadaye.
Ni Salama na Wana Lishe
Ingawa si wadudu wote wanaoweza kuliwa, wengi ni salama ikiwa wametolewa katika maeneo ambayo hayajanyunyiziwa dawa za kuua wadudu au mbolea na ikiwa wanatayarishwa vizuri. Hata hivyo, watu ambao hupata tatizo wanapokula samaki wenye magamba, wanapaswa kuepuka kula wadudu kwa kuwa wote wako katika jamii moja ya arithropoda. Tofauti na samaki wengi wenye magamba ambao hula vitu vilivyooza, wadudu wengi wanaoweza kuliwa hula tu majani na mimea ambayo wanadamu hawawezi kumeng’enya.
Ingawa viwavi ni wadogo, kiwango chao cha virutubisho ni chenye kustaajabisha. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, kiasi cha protini kilicho katika viwavi waliokaushwa ni mara mbili zaidi ya kile kilicho katika nyama ya ng’ombe. Wataalamu wa vyakula wamegundua kwamba wadudu ni chanzo cha lishe bora katika nchi zinazoendelea.
Ikitegemea mtu anakula aina gani ya viwavi, gramu 100 tu ya viwavi inatosha kumwandalia mwanadamu kiasi cha madini muhimu ambayo anahitaji kila siku mwilini kama vile kalisi, chuma, magnesi, fosforasi, potasiamu, na zinki, pamoja na vitamini nyingi. Pia, unga uliotengenezwa kutokana na viwavi unaweza kupikwa kama uji ambao huwa ni lishe bora kwa watoto wenye utapiamlo.
Mbali na kupata lishe, kuna faida nyingine za kula wadudu. Kufanya hivyo pia kunalinda mazingira. Pia, mtu hahitaji kutumia maji mengi na zoea hilo halitokezi kiasi kikubwa cha gesi zinazoongeza joto duniani. Kwa kuongezea, kukusanya wadudu kwa ajili ya chakula ni njia ya asili ya kudhibiti wadudu waharibifu.
Mlo Mkuu
Tulipokuwa tukisubiri kwa hamu mlo huo wa pekee, tulikumbuka kwamba agano la Sheria ambalo taifa la kale la Israeli lilipewa lilisema kwamba nzige ni viumbe safi. Watumishi wa Mungu wa kweli, kama vile Yohana Mbatizaji, walikula nzige. (Mambo ya Walawi 11:22; Mathayo 3:4; Marko 1:6.) Hata hivyo, huenda tukasita kula kitu fulani ambacho hatujazoea.
Ella alirudi kutoka jikoni akiwa na mlo mkuu ambao ulikuwa ukifuka moshi ulionasa uangalifu wa kila mmoja wetu. Mezani tulikuwa tumeketi na wenyeji wanane wa Afrika ya Kati ambao walitabasamu kwa uchangamfu, na mbele yetu kulikuwa na bakuli mbili kubwa zilizojazwa viwavi. Kwa kuwa tulikuwa wageni, sisi ndio tuliopewa heshima ya kupakuliwa kwanza na tulitiliwa chakula kingi.
Tunaweza kusema hivi: “Ukipata nafasi ya kufurahia mlo kama huo ambao si ghali, ni mtamu, na wenye lishe, usisite! Ni mlo ambao hutausahau.”
[Picha katika ukurasa wa 27]
Makongo au viwavi ambao hawajapikwa
[Picha katika ukurasa wa 27]
Kindagozo au panzi waliopikwa