Kuchunguza Bustani za Kisasa za Wanyama
MIAKA elfu tatu iliyopita, maliki wa China alitengeneza bustani aliyoiita Bustani ya Ujuzi. Bustani hiyo ilikuwa na wanyama wengi na ilikuwa na eneo lenye ukubwa wa ekari 1,500 hivi. Zamani hizo, bustani hizo zilikuwa chache sana.
Hata hivyo, leo mamilioni ya watu ulimwenguni pote wanaweza kutembelea bustani za wanyama. “Katika ulimwengu ambamo mazingira ya asili yanatoweka na idadi ya watu inazidi kuongezeka mijini, watu wengi wanatembelea bustani hizo ili kujionea wanyama na kujifunza,” kinasema kitabu Zoos in the 21st Century.
Wanyama Katika Bustani za Kisasa
Bustani za wanyama huwapa wageni fursa ya kujionea baadhi ya wanyama wenye kustaajabisha na wanaovutia ulimwenguni katika mazingira yanayofanana na yale ya asili. Unaweza kuona vipepeo wenye rangi za kupendeza wakipepea katika bustani ya maeneo yenye joto au pengwini wakicheza kwenye barafu katika mazingira yanayofanana na yale ya Antaktiki.
Unaweza kutembea katika mazingira yanayofanana na yale ya misitu ya ikweta na ukaona baadhi ya wanyama na ndege wanaoishi katika mazingira hayo. Au huenda ukaingia katika chumba chenye giza ili uone baadhi ya wanyama ambao huwa watendaji usiku. Katika baadhi ya bustani hizo huenda hata ukaona ndege wakiruka au pomboo wakifanya sarakasi. Zamani wanyama wakali walifungwa ndani ya vizimba lakini siku hizi wanafungiwa katika maeneo ya wazi yaliyo na mitaro mipana inayowatenganisha wanyama hao na watu.
Suala Linalobishaniwa
Baadhi ya wanaharakati wa haki za wanyama wanasema kwamba wanyama hawapaswi kutolewa mwituni na kufungiwa katika mazingira yasiyo ya asili. Wanaharakati hao wanasema kwamba bustani hizo zinazuia wanyama kutembea kwa uhuru na pia zinavuruga tabia zao.
Katika kujibu madai hayo, watu wanaotunza bustani za wanyama wanasema kwamba bustani hizo zinatimiza fungu muhimu katika kuwahifadhi wanyama na kuwaelimisha watu. “Lengo letu ni kuwafundisha watu jinsi ya kuwaheshimu wanyama,” anaeleza Jaime Rull, kutoka Bustani ya Faunia, Madrid, Hispania. “Tunataka kuwachochea wageni wanaotembelea bustani yetu wawe na tamaa ya kutunza mazingira ya wanyama kwani watatoweka maeneo hayo yasipotunzwa.” Utafiti fulani unaonyesha kwamba bustani nyingi zimefanikiwa kuwahamasisha watu waone uhitaji wa kulinda wanyama wanaokabili hatari ya kutoweka.
Inaonekana kwamba baadhi ya aina za wanyama wanaokabili hatari ya kutoweka kama vile panda mkubwa wanapendwa sana na watu. “Watu wote wanaotembelea hapa wanataka kuwaona panda wetu wawili,” anasema Noelia Benito, wa Hifadhi ya Wanyama ya Madrid. “Wanyama hao maarufu wamekuwa kama alama ya
mapambano yetu ya kuhifadhi wanyama wanaokabili hatari ya kutoweka. Tunatumaini kwamba panda hao watazaana, ingawa panda hawakubali kuzaa na panda yeyote tu.”Tofauti na panda, wanyama wengine huzaana kwa urahisi katika bustani za wanyama kwa sababu ya mazingira yaliyoboreshwa na matibabu wanayopata. Kwa kuwa wanyama wengi wamefanikiwa kuzaana katika bustani hizo, hilo limesaidia kujibu maswali ya wachambuzi wanaosema kwamba bustani hizo hazipaswi kujihusisha katika biashara ya kununua au kuuza wanyama wanaokabili hatari ya kutoweka kutoka katika mazingira yao ya asili. Zaidi ya kuhakikisha kwamba kuna wanyama katika bustani yao, bustani nyingi hujaribu kuzalisha wanyama wanaokabili hatari ya kutoweka wakiwa na lengo la kuwarudisha katika mazingira yao ya asili.
Chanzo kikuu cha kutoweka kwa wanyama ni kupotea kwa makao yao ya asili. Kwa hiyo, bustani za wanyama zimejihusisha sana katika kufadhili programu za kuhifadhi mazingira, zikishirikiana kwa ukaribu na hifadhi za wanyama-pori katika nchi zenye joto. *
Kujifunza Kuhusu Viumbe wa Asili
Kwa sababu watoto wengi huvutiwa na wanyama, familia nzima inapotembelea bustani ya wanyama wakati wa mwisho juma au wa likizo, wazazi wanaweza kutumia pindi hiyo kuwafundisha watoto kuhusu uumbaji wa Mungu. Wakiwa familia, wanaweza kustaajabia maajabu hayo ya uumbaji.
Tangu zamani, wanadamu wamevutiwa sana na wanyama. Tunapaswa kuwachochea watoto wetu wasitawishe upendezi huo kwa kuwa viumbe hutusaidia kuufahamu vizuri zaidi utu wa Muumba. Kutembelea bustani za wanyama pia kunaweza kutusaidia tuwaheshimu na kuwafahamu zaidi viumbe hao wanaoishi katika sayari yetu.
^ fu. 12 Inaonekana kwamba jitihada zinazofanywa na bustani za wanyama kuwalinda simbamarara huko Asia, komba wa Madagaska, na nyani wa Afrika zimefanikiwa.