Je, Ni Kazi Ya Ubuni?
Uwezo wa Samaki wa Kuogelea Katika Vikundi
Kila mwaka aksidenti za magari huua watu zaidi ya milioni moja na kujeruhi angalau watu milioni 50. Hata hivyo, mamilioni ya samaki wanaweza kuogelea pamoja katika vikundi bila kugongana hata kidogo. Samaki hao hufaulu jinsi gani, na wanaweza kutufundisha nini kuhusu kupunguza aksidenti za magari?
Fikiria hili: Samaki ambao huogelea katika vikundi hujifunza kuhusu mazingira yao kupitia macho na mstari wa chembe za hisi ulio ubavuni mwao (lateral line). Wanatumia hisi hizo kutambua mahali samaki wengine walipo karibu nao, kisha wanatenda kwa njia zifuatazo:
-
Kusafiri sambamba na wengine. Wanasonga kwa mwendo sawa na samaki walio kando yao na kudumisha umbali unaofaa kutoka kwao.
-
Kukaribia. Wao huwakaribia samaki walio mbele yao.
-
Kuepuka kugongana. Wanabadili upande wanaoelekea ili kuepuka kugusana na samaki wengine.
Kwa kutegemea tabia hizo tatu za samaki wanaoogelea katika vikundi, watengenezaji wa magari nchini Japani wamebuni magari kadhaa madogo ya roboti yanayoweza kusonga katika kikundi bila kugongana. Badala ya macho, roboti hizo zinatumia teknolojia ya mawasiliano; badala ya mstari wa chembe za hisi, zinatumia leza inayotambua umbali. Kampuni hiyo inasadiki kwamba teknolojia hiyo itawasaidia kutokeza magari “yasiyoweza kugongana” na “kusaidia mazingira yasiharibiwe na pia kusiwe na msongamano wa magari.”
“Tumeiga tabia ya kikundi cha samaki wanaoogelea pamoja [kwa] kutumia teknolojia ya elektroniki ya kisasa zaidi,” anasema Toshiyuki Andou, injinia mkuu wa mradi wa kutokeza magari ya roboti. “Sisi tulio katika ulimwengu uliojaa magari, tunaweza kujifunza mengi kutokana na tabia ya vikundi vya samaki wanaoogelea pamoja.”
Una maoni gani? Je, uwezo wa samaki wa kuogelea katika vikundi ulijitokeza bila akili yeyote? Au ulibuniwa?