Kuutazama Ulimwengu
Marekani
Kila siku, zaidi ya watu 20 waliowahi kutumikia katika jeshi la Marekani wanajiua. Kila mwezi, wanajeshi wa zamani wapatao 950 wanaotunzwa na Wizara ya Marekani ya Wanajeshi Waliostaafu hujaribu kujiua.
China
“Karibu nusu ya wanawake walio chini ya umri wa miaka 30 waliohama eneo la nyumbani kwao kwenda kufanya kazi katika miji mingine wamepata mimba kabla ya ndoa, na hilo limeongeza idadi ya akina mama [Wachina] wasio na wenzi ikilinganishwa na ilivyokuwa kizazi kimoja tu kilichopita,” linaripoti gazeti China Daily. Pia inasemekana kwamba Wachina “wameanza kuwakubali . . . wenzi wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa.”
Ugiriki
Inaonekana kwamba malaria imerudi tena nchini Ugiriki. Ugonjwa huo ulikuwa umeangamizwa nchini humo katika mwaka 1974. Inasemekana kwamba ugonjwa huo umerudi kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi na pia kwa sababu ya kupunguzwa kwa kiasi cha pesa kinachotengwa kwa ajili ya matibabu ya umma.
India
Utafiti ulionyesha kwamba licha ya mabadiliko katika jamii, bado asilimia 74 ya watu waliohojiwa wanapendelea ndoa za kupangwa badala ya kujichagulia mwenzi. Pia asilimia 89 wanapendelea kuishi pamoja na watu wa ukoo badala ya kuishi na familia yao tu ambayo inafanyizwa na baba, mama na watoto.
Italia
“Kanisa [Katoliki] linalemewa, hata katika nchi zenye utajiri za Ulaya na Amerika. Utamaduni wetu umezeeka, makanisa yetu ni makubwa, makao yetu ya watawa hayana watu, mfumo wa usimamizi wa kanisa haufanyi kazi vizuri, desturi zetu na mavazi ya makasisi wetu yamekuwa na madoido mengi zaidi. . . . Kanisa limeachwa nyuma kwa miaka 200.”—Mahojiano na kardinali Mkatoliki Carlo Maria Martini, yaliyochapishwa baada ya kifo chake na gazeti la Corriere della Sera.