Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kusini Mashariki mwa Asia

Kulingana na shirika la Hazina ya Wanyama wa Pori Ulimwenguni, kati ya mwaka wa 1997 hadi 2011, aina nyingi za mimea na wanyama ziligunduliwa, kutia ndani nyoka mwenye macho ya rangi nyekundu (Trimeresurus rubeus), viumbe hao wamegunduliwa kwenye eneo la Greater Mekong, lililo katika nchi za Kambodia, Laos, Myanmar, Thailand, Vietnam, na jimbo la Yunnan, China. Viumbe vilivyogunduliwa mwaka wa 2011, vilitia ndani aina 82 za mimea, reptilia 21, samaki 13, amfibia 5, na mamalia 5.

Ulaya

Kulingana na gazeti la The Moscow Times, biashara haramu ya kusafirisha binadamu ni tatizo kubwa katika “eneo lote la Umoja wa Ulaya.” Watu wengi huuzwa kwa ajili ya kutumiwa kingono, kazi ya kulazimishwa, na hata “biashara haramu ya viungo vya binadamu.” Biashara hiyo inasababishwa hasa na umaskini, ukosefu wa ajira, na ubaguzi wa kijinsia.

New Zealand

Utafiti kuhusu madhara ya kutazama televisheni kwa watoto na vijana wanaobalehe unaonyesha kwamba kutazama kwa muda mrefu hufanya “wasipende kuchangamana na watu wanapokuwa watu wazima.” Hivyo, watafiti wanapendekeza kwamba watoto watazame “vipindi vinavyofaa kwa muda usiozidi saa 1 au 2 kwa siku.”

Alaska

Karibu vijiji vyote vya “Wenyeji wa Asili wa Alaska” viko pwani au karibu na mito, na asilimia 86 ya vijiji hivyo huathiriwa na mafuriko na mmomonyoko wa udongo. Utafiti unaonyesha kwamba ongezeko la joto linasababisha kuyeyuka kwa ukingo wa barafu kwenye ufuo, na hivyo kufanya vijiji vikabili hatari ya vimbunga.

Ulimwenguni

Licha ya jitihada za kutokeza nishati isiyo na uchafu, kama vile nishati ya upepo na jua, “kwa kawaida nishati inayozalishwa leo ni chafu kama tu ilivyokuwa miaka 20 iliyopita,” anasema Maria van der Hoeven, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati.