NCHI NA WATU
Kutembelea Belize
BELIZE ni nchi ndogo yenye vitu vingi, kama vile misitu mikubwa na maji ya bahari yanayozunguka visiwa kadhaa kwenye pwani ya nchi hiyo. Lakini kuna mambo mengine ya kushangaza nchini Belize.
Kuna aina nyingi za ndege na wanyama katika nchi hiyo. Kati yao ni ndege mwenye rangi nyingi aitwaye toucan (Ramphastos sulfuratus) na mnyama wa jamii ya kifaru aitwaye tapir (Tapirus bairdii)—mwenye pua ndefu na awezaye kwenda kwa kasi kwenye nchi kavu na majini! Pia, kuna chui aina ya jaguar (Panthera onca). Belize ndiyo nchi ya kwanza ulimwenguni kuwa na hifadhi ya chui aina ya jaguar.
Zamani Belize ilikuwa sehemu ya Wamaya. Wahispania walifika kwenye eneo hilo katika karne ya 16 lakini hawakuwashinda kabisa Wamaya. Baadaye, Waingereza walichukua eneo hilo na mwaka wa 1862 wakalitangaza rasmi kuwa koloni lao (British Honduras). Nchi ya Belize ilipata uhuru mwaka wa 1981.
Wabelize wanapendeza kama tu nchi yao. Kati ya wenyeji wa asili ni Wakrioli, Wahindi wa Mashariki, Wagarifuna, Wamaya, na Wamestizo. Watu hao ni wenye adabu na urafiki. Watoto wanapozungumza na watu wazima mara nyingi wao huwaita “Bwana” au “Bibi” na hujibu kwa kusema “Ndiyo Bibi” au “Hapana Bwana.”
Nchini Belize, kuna makutaniko ya Mashahidi wa Yehova wanaozungumza Lugha ya Ishara ya Marekani, Kikrioli cha Belize, Kiingereza, lahaja ya Kijerumani, Kichina (Mandarin), Kimaya (Mopán), na Kihispania. Mwaka wa 2013, angalau mtu 1 kati ya 40 alijiunga na Mashahidi kuadhimisha Ukumbusho wa kifo cha Kristo.
JE, WAJUA? Tumbawe la Belize lina urefu wa kilomita 290. Tumbawe hilo la Belize, ni sehemu ya tumbawe la pili kwa ukubwa duniani. Tumbawe kubwa zaidi linapatikana nchini Australia.