Uzuri wa Ziwa Kubwa Zaidi Amerika ya Kati
Uzuri wa Ziwa Kubwa Zaidi Amerika ya Kati
INGAWA Nikaragua ni nchi ndogo, ina ziwa kubwa zaidi katika Amerika ya Kati—Ziwa Nikaragua. Jambo la kushangaza ni kwamba huenda Ziwa Nikaragua likawa ndilo ziwa pekee la maji baridi lenye samaki wanaopatikana baharini kama vile papa, chuchunge, na tarpon. Wanasayansi wanaamini kwamba wakati mmoja ziwa hilo lilikuwa ghuba iliyoungana na Bahari ya Pasifiki lakini mlipuko wa volkano ukalitenganisha na bahari. Maji yalipoacha kuwa ya chumvi, samaki walijipatanisha na mazingira yao mapya.
Ziwa hilo lenye urefu wa kilomita 160 na upana wa kilomita 70 hivi, liko mita 30 hivi juu ya usawa wa bahari. Kuna zaidi ya visiwa 400 kwenye Ziwa Nikaragua na visiwa 300 hivi viko kwenye Rasi ya Asese, karibu na mji wa Granada ulioko upande wa kaskazini wa ziwa hilo. Vinaitwa Visiwa Vidogo vya Granada.
Kisiwa kikubwa kwenye ziwa hilo ni Kisiwa cha Ometepe kilichoko katikati. Kisiwa hicho cha Ometepe kilicho na urefu wa kilomita 25 na upana wa kilomita 13, kimefanyizwa kwa milima miwili ya volkano iliyounganishwa kwa shingo ya nchi. Mlima mrefu zaidi wa volkano wenye kilele kilicho na umbo la pia unaitwa Concepción, una kimo cha mita 1,610 juu ya usawa wa ziwa hilo. Huo ni mlima wa volkano hai na unaonekana wazi kabisa upande wa kaskazini wa kisiwa hicho. Mlima ule mwingine unaitwa Madera, nao una kimo cha mita 1,394 na ni volkano isiyotenda. Ukiwa umefunikwa kwa mimea, Mlima Madera una wangwa wenye ukungu ndani ya bonde la mlima huo.
Ziwa Nikaragua ni moja kati ya sehemu ambazo watalii hupenda kutembelea katika eneo hilo. Wao huenda kuona uzuri wa asili wa kitropiki na maeneo ya kiakiolojia ya ustaarabu wa kale. Lakini kuna kitu kingine kuhusu uzuri wa Ziwa Nikaragua ambacho watu wanapaswa kujifunza.
Kijiji Kinachoelea Juu ya Maji
Visiwa Vidogo vya Granada vina mimea mingi ya tropiki na wanyama wengi wa mwituni. Maua maridadi kabisa hukua katika misitu ya visiwa hivi vya volkano. Kwenye fuo za ziwa hilo, utawaona ndege maridadi wa majini kama vile korongo, yangeyange-mkuu, furukombe, mbizi, na mnandi. Kandokando ya misitu hiyo kuna viota vilivyojengwa na ndege wakubwa wanaoitwa Montezuma oropendolas vikining’inia kwenye miti mikubwa vikipeperushwa huku na huku kwa sababu ya upepo unaotoka kwenye ziwa.
Watu wanaishi katika baadhi ya visiwa hivyo vidogo. Kwenye visiwa hivyo utapata nyumba za wavuvi wa eneo hilo na nyumba za matajiri za kuishi wakati wa likizo. Pia, kuna shule na makaburi kwenye visiwa hivyo na vilevile mikahawa na baa. Visiwa hivyo vinafanana na kijiji kinachoelea juu ya maji.
Kila asubuhi mashua yenye rangi ya bluu na nyeupe husafiri kutoka kisiwa kimoja hadi kingine kuwabeba wanafunzi wa shule. Duka linaloelea husafiri kutoka kisiwa kimoja hadi kingine likiwa na matunda na mboga za kuuza. Shughuli za kila siku hutia ndani wanaume kutayarisha nyavu zao na wanawake kufua nguo ziwani.
Mashahidi wa Yehova pia wanafanya kazi kwa bidii katika visiwa hivyo. Wanawatembelea watu wa eneo hilo kwa kutumia mashua ili wazungumze nao kuhusu habari njema za Ufalme wa Mungu. (Mathayo 24:14) Eneo hilo lisilo la kawaida lilikuwa na tatizo moja: Mikutano ya kujifunza Neno la Mungu, Biblia, ingefanyiwa wapi? Ili kutii himizo la Biblia “bila kuacha kukusanyika pamoja,” Mashahidi wa Yehova walibuni njia ya pekee—Jumba la Ufalme la kwanza linaloelea nchini Nikaragua!—Waebrania 10:25.
Jumba la Ufalme Linaloelea
Wenzi fulani ambao ni watumishi wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova walihamia kwenye Visiwa Vidogo vya Granada Novemba (Mwezi wa 11) 2005. Miezi michache baadaye, walipowakaribisha watu kwa ajili ya Ukumbusho wa kifo cha Kristo, walishangaa kuona watu 76 wakihudhuria. Hilo liliwasadikisha wenzi hao kwamba wanapaswa kufanya mikutano ya Kikristo kwa ukawaida katika eneo hilo. Kwa kuwa haikuwa rahisi kupata mahali panapofaa kufanyia mikutano hiyo, mapainia hao waliamua kutafuta mbinu nyingine. Waliamua kujenga Jumba la Ufalme linaloelea, linaloweza kupelekwa maeneo mbalimbali ambako watu wanapatikana.
Ingawa ndugu huyo pamoja na mke wake hawakuwa wamewahi kubuni au kujenga chombo chochote kinachoelea, walianza ujenzi. Wao pamoja na wengine sita walifanya kazi hiyo kwa mwezi mmoja. Mahali hapo pa kukutania pangekuwa chelezo kilichojengwa kwa mabomba ya chuma yaliyoshikiliwa kwa mapipa 12 yaliyojazwa upepo ili yaelee. Kila moja ya mapipa hayo linaweza kubeba lita 150 hivi
za maji. Sakafu ingekuwa ya mbao na turubai lingetumiwa kama paa. Wafanyakazi hao walisali kila siku kuhusu kazi yao kwa kuwa hakuwa na hakika ikiwa jumba hilo lingeelea. Lakini lilielea!Jumba hilo jipya la Ufalme lilianza kutumiwa kwa mara ya kwanza mwezi Juni 10, 2006 (10/6/2006). Siku iliyofuata, Jumba hilo lilivutwa hadi upande mwingine wa kisiwa ili kufanya mkutano huohuo. Mikutano hiyo miwili ilihudhuriwa na watu 48, ingawa ilibidi watu fulani watembee kwa nusu saa kupitia msitu ili kuhudhuria. Wote walifurahi kuwa na mahali pao pa ibada!
Kwa kweli kukutana katika Jumba hilo la Ufalme kunawafanya watu wajihisi wako nyumbani. Hotuba inapoendelea, wasikilizaji wanaweza kusikia maji yakipigapiga miamba au wanaweza kusikia tumbili akilia kwa mbali. Baada ya muda fulani wakazi wengi wa kisiwa hicho walizoea kuliona Jumba hilo. Walipunga mikono yao Jumba hilo lilipokuwa likihamishwa kutoka eneo moja hadi lingine. Kila juma, zaidi ya watu 20 huja kwenye Jumba hilo la Ufalme linaloelea kwa ajili ya ushirika wa Kikristo na ili wafundishwe Biblia. Jinsi Jumba hilo limethibitika kuwa baraka!
Kisiwa cha Ometepe
Kilomita 50 hivi kuelekea kusini ya Granada, kuna kisiwa cha Ometepe. Tangu zamani watu wamefurahia kuishi kwenye kisiwa hicho kwa sababu ya mazingira yake mazuri na udongo wenye rutuba. Kwa kweli, ukulima nchini Nikaragua ulianza katika kisiwa hicho. Leo, kuna watu 42,000 hivi kwenye kisiwa cha Ometepe ambao huvua samaki na kulima mahindi, ndizi, kahawa, na mazao mengine. Pia, kuna wanyama wengi wa mwitu wenye kupendeza. Kuna kasuku wengi wenye kupiga kelele, magpie-jay wakubwa wakipigapiga mabawa yao yenye manyoya ya bluu na meupe, na tumbili wenye nyuso nyeupe wanaoitwa capuchin wanaopendwa na wengi.
Pia, kuna watangazaji wengi wa habari njema za Ufalme wa Mungu ambao huwahubiria wakazi wa Ometepe. Mnamo 1966, watu 8 walibatizwa, lakini idadi ya Mashahidi imeongezeka kufikia 183, walio katika makutaniko manne yenye maendeleo mazuri. Kila kutaniko lina Jumba lake la Ufalme lililojengwa mahali panapofaa. Leo, kuna Shahidi 1 kwa kila wakazi 230 kwenye kisiwa hicho.
Kwa miaka mingi Mashahidi wa Yehova huko Ometepe wamekabili matatizo mengi. Kwa mfano, mnamo 1980 wapinzani waliteketeza Jumba la Ufalme huko Mérida. Jumba lingine lilijengwa mwaka wa 1984. Jumba hilo lilitumiwa hadi mwaka 2003 wakati Jumba jipya maridadi lilipojengwa, na washiriki 60 wa kutaniko hilo walifurahi sana.
Katika jiji la Moyogalpa, Jumba la Ufalme ambalo linaweza kutosha watu wengi kukiwa na uhitaji lilijengwa. Mashahidi wa eneo hilo pamoja na marafiki zao kutoka sehemu zote za ziwa hilo hukutana hapo mara kwa mara kwa ajili ya makusanyiko makubwa. Wakati wa makusanyiko hayo Ziwa Nikaragua huwa mahali pazuri pa kuwabatiza wanafunzi wapya wa Yesu Kristo.—Mathayo 28:19.
Je, Hazina Hizo Zitahifadhiwa?
Ziwa Nikaragua lilionekana kana kwamba haliwezi kuchafuliwa labda kwa sababu ya ukubwa wake. Lakini leo ziwa hilo linahitaji kulindwa. Maji yake yanachafuliwa na uchafu kutoka kwenye mashamba na viwanda na kutoka katika maeneo yaliyokatwa miti.
Haijulikani ikiwa serikali na wakazi wa eneo hilo wataweza kuzuia uchafuzi huo. Hata hivyo, Muumba atahakikisha kwamba hazina zote za dunia, kutia ndani maziwa yake yenye kung’aa, visiwa vyake maridadi, na wanyama wake wa mwituni wenye kupendeza wanatunzwa vizuri ili wawe urithi wa wanadamu waaminifu. Biblia inatuambia hivi: “Waadilifu wenyewe wataimiliki dunia, nao watakaa milele juu yake.”—Zaburi 37:29.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mikutano ya Biblia hufanyiwa katika Jumba hili la Ufalme linaloelea